The House of Favourite Newspapers

MAMBO MADOGO YANAVYOWEZA KUIVUNJA NDOA!

LEO tutaangalia mambo ambayo wewe unaweza kuyaona ni madogo madogo lakini hakika yanaweza kuivunja ndoa yako kama siyo kuiweka matatani.

KUWA BIZE SANA

Wanandoa wengi hawana muda wa kupumzika na wenza wao na kubadilishana mawazo. Hii ni kutokana na maisha ya sasa yanavyoenda. Tatizo hili au tabia hii inaweza kukusababishia mwenza wako kukukosa na kuona kuwa hana muda na wewe. Kwa maana hiyo inaweza kusababisha yeye kuvunjika moyo na kuizoea tabia ambayo kimahusiano inafifisha mapenzi.

KUDANGANYA

Hakuna anayependa kudanganywa hasa pale ambapo hapastahili lakini pia hakuna ambaye anapenda kuahidiwa kitu kisha asitimiziwe. Baadhi ya tulio kwenye uhusiano tunapenda kudanganya sana, kitu ambacho unaweza kukidharau lakini mwenza wako kikamuumiza sana.

KUKOSA IMANI NAYE

Kuwa na wasiwasi na mwenza wako kila wakati ni tabia mbaya ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuivunja ndoa. Ni sawa tu na kutokumuamini unayeishi naye. Jenga imani hata kama unatilia shaka jambo flani, lifanyie kazi kwa makini na usimuoneshe umpendaye kuwa una mashaka naye mara kwa mara.

KUCHUKULIA POA KILA KITU

Kama mwenza wako hakulalamikii kwa jambo baya unalomfanyia au unalomnyima ni rahisi kujisikia vibaya. Ni vizuri kama mwenza wako atafahamu unahitaji nini na unataka nini lakini usipolalamika atakushangaa kwani moja kwa moja atahisi huna upendo naye. Wanandoa wengi huhisi wanapendwa kama watalalamikiwa jambo, hasa wanandoa wanawake wao wakilalamikiwa na waume zao huamini wanapendwa.

TENDO LA NDOA

Mara nyingi wapendanao penzi hujengwa na tendo la ndoa hasa pande zote zikishiriki ipasavyo. Sasa ikitokea wewe ni mtu ambaye una tabia ya kupenda kupuuza tendo hilo hasa anapokuhitaji mpenzi au mumeo/ mkeo, unamkatisha tamaa mwenza wako. Kumbuka kuwa mahusiano bila ya tendo yataenda pabaya. Kuwa bize mara kwa mara na mambo yako au maisha yanayokufanya uwe na sababu ya kukosa muda wa kutosha wa kucheza na mwenza wako ni tatizo, kumbuka tendo ni muhimu kuliko chochote.

KUHUSUDU KAZI

Kuwa na kazi kwa ajili ya kuwaendeleza kimaisha ni muhimu hasa kwa maisha ya sasa lakini linapokuja suala la mahusiano au ndoa ukiendekeza kazi wakati wote unaweza kujikuta unavunja ndoa.

KUFUJA PESA

Pesa ni kitu muhimu sana kwa maisha ya binadamu lakini isipochukuliwa kwa umakini inaweza kuleta balaa. Usipoangalia pesa inaweza kukupa ‘stresi’, unaweza kuingia kwenye malumbano na mwenza wako sababu tu ya pesa. Kushindwa kwako kupanga bajeti vizuri, uchumi unaweza kushuka. Kukosekana kwa utunzaji mzuri wa pesa kunaweza kuwakosesha furaha ya ndoa. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unakuwa na matumizi mazuri ya pesa hata kama mnazo nyingi.

Amran Kaima- 0658 798787

Comments are closed.