The House of Favourite Newspapers

Mambo Ya Kufanya Kabla Ya Kuingaliia Kwenye Ndoa

DUNIA ya sasa si kama ya zamani. Ndoa zimekuwa hazidumu kama ilivyokuwa zamani. Hii yote imetokana na mmonyoko wa maadili ambao umeiondoa dhana halisi ya ndoa na watu kuifanya kama fasheni.

 

Uhalisia wa ndoa na maisha haupo. Watu sasa hivi wanaoana ilimradi tu kutimiza matamanio. Mwanamke umri umekwenda, anataka tu na yeye aitwe mke wa fulani, basi analazimika kuingia kwenye ndoa. Mwanaume anaoa kwa sababu anaona amechoka kujipikia chakula.

 

Watu wanaoana ili tu wafanye maonesho katika mitandao ya kijamii. Marafiki wajue kwamba fulani naye ameoa, hakuna tena maadili ya ndoa. Mtu ameolewa, lakini bado anatamani kutanga na dunia, mathalan aende klabu, ajirushe na marafiki.

 

Athari za maadili zilizoanzia kutoka kwa baadhi ya wazazi ndizo zilizosababisha majanga makubwa kwa kizazi cha sasa. Wazazi wamewapa uhuru sana vijana wao, matokeo yake wanajikuta wakitengeneza ‘bomu’ ambalo hulipuka muda wowote.

Changamoto za ndoa hawazijui. Hawana uvumilivu, wakikutana na magumu kidogo tu, hukimbilia kuachana. Kizazi kimejeruhiwa kwelikweli. Kila mwanamke unayekutana naye ameshakuwa sugu kwa kuumizwa. Ameshaongopewa ndoa kiasi cha kutosha. Amekutana na majambazi, wezi na watu wasiofaa katika jamii.

 

Kutokana na sarakasi hizo alizopitia, mwanamke haitamani tena ndoa. Anacholilia yeye kinakuwa ni kupata mtoto, maisha yaendelee. Mwanaume naye vivyo hivyo, ameshakutana na matapeli wa mapenzi kiasi cha kutosha. Haoni hata mke wa kumuoa, anabaki kuwa mhuni tu miaka yote.

 

Jamani tukubali tukatae, kuna vitu tunavikosea. Wengi wetu tunaingia kwenye ndoa pasi na kujua misingi yake. Hatujui kanuni zake. Hatujui nini tunapaswa kufanya kabla hatujajiingiza kwenye ndoa na ndiyo maana hata tukiingia tunaishia kuishi miaka miwili au mitatu, ndoa chali!

 

Badala ya kusikilizana, kwenye ndoa kila mmoja anajifanya mjuaji. Mwanaume anapambana kusaka kuwa kichwa cha familia, mwanamke naye anataka kuwa msemaji mkuu wa familia. Hakuna wa kumsikiliza mwenzake, nyumba inatawaliwa na ugomvi kila siku.

 

Ndugu zangu, kabla ya kuingia kwenye ndoa yakupasa kwanza ujitathmini. Ujue ujijue kwamba wewe ni nani na unataka kuingia kwenye ndoa ya aina gani. Una-taka kui-ngia kwenye ndoa, upo tayari kua-cha mambo ya kitoto? Upo tayari kuacha uhuni, starehe za kijingajinga?

 

Upo tayari kukutana na misukosuko? Unakwenda kwenye ndoa, umejiandaa kuwa baba? Umejiandaa kuihudumia familia? Upo tayari kushirikiana na mwenzako katika uzima na magonjwa? Unajua mikikimikiki ya ndugu wa pande zote mbili?

Ukijiridhisha wewe una hizo sifa, angalia na upande wa pili. Unayetaka kuanzisha naye uhusiano, je, ana sifa hizo? Ni mvumilivu? Anaweza kukabiliana na changamoto kama ulizojitathmini wewe? Kama hana ni bora kuachana naye mapema katika kipindi cha urafiki ili usije kujilamu baadaye.

 

Kubwa kuliko yote jitahidi uingie na mtu kwenye ndoa ambaye ana utu, ana hofu ya Mungu.

Eneo hili ni la kuwa makini, waswahili wanasema bora ukosee njia, lakini si kuoa. Hakikisha unakuwa mtu sahihi na unatafuta mtu sahihi vilevile. Mtu atakayeweza kuvumilia kipindi ambacho mtakuwa kwenye wakati mgumu.

 

Tafuta mtu ambaye tatizo lako litakuwa lake na lake litakuwa lako. Mtu asiye na tamaa za kijinga au mwenye hulka ya umalaya. Mtu ambaye kweli ameamua kwa dhati kuishi maisha ya ndoa na si kutamani sherehe.

 

Na Erick Evarist.

 

Comments are closed.