The House of Favourite Newspapers

MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUINGIA KWENYE UCHUMBA

KUPATA mwenzi bora wa maisha siyo mchezo, lazima ubongo wako ufanye kazi sawasawa ili uweze kugundua kwamba mpenzi uliyenaye anafaa kuwa mchumba na baadaye kuwa mwenzi wako wa maisha.

 

Najua wengi wanapasuka vichwa, hawajui aolewe/amuoe nani; mwingine anajikuta akiwa katika uhusiano na wapenzi zaidi ya watatu na wote anawapenda lakini anashindwa kuelewa ni yupi hasa anafaa kuwa mwenzi wake. Ingawa ni kosa kubwa kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja, lakini hilo linatokana na kutojiamini, kukosa maamuzi na kushindwa kuwa na uhakika ni nani hasa kati ya hao ulionao anafaa kuwa mwenzi sahihi.

 

Kimsingi suala la kuishi pamoja siyo la kukurupuka. Lazima uwe makini ili usije ukafunga ndoa kesho halafu baada ya wiki tatu, ukaanza kulia! Matatizo katika ndoa yako unaweza ukayaepuka ikiwa ulikuwa makini katika kuchagua mchumba bora. Mchumba bora anapatikana kwa kutenga muda wa kutosha, kumchunguza sawasawa katika kipindi chote cha uchumba. Nini hasa unatakiwa kuchunguza kwa makini? Twende darasani…

 

DESTURI ZA KABILA LAKE…

Vijana wengi wa siku hizi hukurupukia ndoa, hawana muda wa kuwachunguza wapenzi wao vya kutosha. Wanakutana mjini, wanadanganya wanapendana na baada ya wiki tatu hadi nane unaambiwa wanaishi pamoja baada ya kufunga ndoa.

 

Lazima ujue ni kabila gani, desturi zao zikoje na amekulia katika malezi ya aina gani. Kukutana na mtu kisha baada ya muda mnaishi pamoja ni hatari. Vijana wengi wanakumbana na matatizo kutokana na kuruka kipengele hiki. Zamani wavulana walikuwa wanatafutiwa wachumba na wazee wao, lakini hivi sasa kutokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, vijana wamepewa uhuru wa kuchagua wenyewe wenzi wawapendao.

 

Hata hivyo uhuru huo unaonekana kusababisha matatizo kwa baadhi ya vijana. Ni vizuri kuishi na mtu unayemfahamu vizuri, familia yake, ukoo n.k, lakini kama ikitokea kwa bahati mbaya mmekutana mjini na mkapendana basi fanya uchunguzi wako kimya kimya ili umjue vizuri mpenzi wako.

 

Kuna baadhi ya makabila wana mila za kurithishana, wengine wanashea mapenzi. Mathalani wewe ni mwanamke umeolewa, ghafla anakuja kaka wa mumeo kutoka kijijini. Ndani ya wiki hiyo hiyo mumeo anapata safari ya ghafla, huku nyuma shemeji yako anataka kulala na wewe.

Kutokana na kumheshimu unamkatalia. Mumeo anaporudi unamweleza tukio zima lilivyokuwa, cha ajabu wala hakasiriki, sana sana anakulaumu kwa kumnyima ndugu yake unyumba! Kumbe hizo ni mila zao, lakini wewe ulikuwa hujui kabla, sasa katika hali kama hii utajisikiaje? Lakini ukumbuke kwamba kama ungemchunguza vizuri, ungejua mambo hayo na pengine usingeingia katika ndoa hiyo.

 

UNAYEMPENDA KWA DHATI

Hii isibaki kuwa hadithi za kufikirika, iwe yakini na moyo wako uzungumze hivyo, kuwa unampenda kwa mapenzi ya dhati! Utajuaje kama unampenda? Sema na moyo wako utakupa ukweli juu ya hilo, usikurupukie mapenzi, usije ukamuona msichana siku moja ukamtamani ukadhani unampenda, utakuwa unapotoka!

 

Mapenzi huanza moyoni, jiridhishe kwanza ndipo ukubali kumwingiza katika moyo wako. Kumbuka unapoamua kufunga ndoa na mtu ni ahadi ambayo mmeahidiana mbinguni na duniani. Ni ahadi ambayo inapaswa kutenganishwa na kifo tu, sio vinginevyo! Kamwe usifanye majaribio katika mapenzi, mapenzi hayajaribiwi. Kitu cha kuzingatia zaidi katika kipengele hiki ni kwamba, lazima awe anakuvutia zaidi.

 

Usipomuona kwa siku kadhaa moyo wako unakuwa hauna amani kabisa. Akitokea tu, moyo wako unafurahi na kuona kweli mpenzi unaye. Kuingia katika ndoa na mwenzi ambaye hakuvutii ni hatari maana baadaye unaweza ukajikuta unatamani kutoka nje ya ndoa. Usiruhusu hilo litokee. Jiridhishe kwanza, awe anakuvutia ndipo ufikirie suala la kuwa mchumba wako na baadaye ndoa.

 

Mada yetu itaendelea wiki ijayo, USIKOSE! Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Comments are closed.