The House of Favourite Newspapers

Mambosasa: Baadhi ya Wafungwa Walioachiwa na JPM Wanafukua Silaha Zao

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limedai kuwa linazo taarifa kwamba baadhi ya wahalifu walioachiwa kwa msamaha wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wameanza kufukua silaha zao walizokuwa wamezificha ili zifanye kazi ya uhalifu katika maeneo mbalimbali huku akisema hawatasita kuwarudisha tena jela iwapo wataendelea na tabia za uhalifu.

Mambosasa ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuhusu matukio ya uhalifu, na kusema kwamba watu wanaoongoza kwa vitendo vya uhalifu ni wale waliotoka kwa msamaha wa rais, na kwamba wanatumwa na wenzao walio jela.
Akiendelea kuzungumzia suala hilo, Kamanda Mambosasa amesema watu hao wamekuwa wakirudi maeneo walioficha silaha kabla hawajakamatwa na kufungwa, na kuzichukua kuzitumia kwenye matukio ya uhalifu, huku wakiendelea kuwasiliana na wale ambao bado wako gerezani kujua wameweka wapi silaha ili kuzitumia kwenye kazi zao, na kisha kuwapelekea posho.
“Taarifa tulizonazo baada ya wahalifu wengine waliochiwa kwa msamaha wa rais, wachache hawataki kubadili tabia zao, wanakwenda kufichua silaha ambazo walizizika ardhini na sasa wanazifukua kwa ajili ya kuanza kuzitumia. Ninatoa onyo kwa mtu yeyote ambaye amepata msamaha, badala ya kumshukuru Mungu akabadili tabia akaanza kuishi kwa kufuata sheria za nchi, anaenda kufukua silaha mahali alipoficha kwa ajili ya kuendeleza vitendo vya uhalifu, niwaambie hawatabaki salama, tutawarudisha huko walikotoka”, amesema Mambosasa.
Kufuatia tukio hilo Kamanda Mambosasa amewataka watu waliopewa msamaha na Rais na kuwa huru, kuacha kabisa matendo maovu, na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano pale wanapohisi kuna mtu anafanya vitendo vya uhalifu.

‘Wafungwa Walioachiwa na JPM Wanafukua Silaha Zao’ – Mambosasa

Comments are closed.