The House of Favourite Newspapers

Mamia Wafurika TANESCO Kusaka Luku za Umeme

0

MAMIA ya wakazi wa Shinyanga wamemiminika katika ofisi za Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) mkoa wa Shinyanga na Wakala wa Luku Mfoy kwa ajili ya kupata huduma ya umeme kutokana na kuwepo kwa tatizo katika huduma ya manunuzi ya LUKU kupitia njia za kielektroniki.

Wakazi wa Shinyanga wameonekana wakiwa wamepanga foleni katika ofisi za TANESCO na Wakala Mfoy aliyepo katika eneo la Stendi ya Mabasi Mjini Shinyanga ili kupata huduma ya umeme huku wengine wakionekana kukata tamaa kutokana na foleni ndefu kufikia huduma hiyo.

Tayari Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameagiza kusimamishwa kazi kwa siku 10 watumishi watatu wa TANESCO akiwemo Meneja wa mfumo wa LUKU kwa kushindwa kutatua tatizo la LUKU lililojitokeza kwa siku tatu na kuleta usumbufu kwa wananchi.

Waliosimamishwa kazi ni Meneja wa TEHAMA na huduma za biashara wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Lonus Feruzi na Wasaidizi wake Frank Mushi na Idda Njau ili watoe maelezo kufuatia kuwepo kwa tatizo katika huduma ya manunuzi ya LUKU kupitia njia za kielektroniki na kusema endapo maelezo yao hayatojitosheleza wataondolewa kazini.

Kwa muda wa siku tatu, Wateja wa TANESCO wameshindwa kununua umeme wa LUKU kwa njia ya Kielekroniki hivyo kulilazimu Shirika hilo kuwaelekeza Wateja wake kununua umeme kwenye ofisi zake za Mikoa na Wilaya katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Leave A Reply