The House of Favourite Newspapers

Mara: Polisi Wakamata Mangariba 11 kwa Tuhuma za Ukeketaji wa Watoto Zaidi ya 800

ngaribaMARA: Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya mkoani Mara, limefanikiwa kuwakamata mangariba 11 wilayani Tarime kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ukeketaji watoto wa kike zaidi ya 800 katika Wilaya ya Tarime kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, akizungumza kwenye hafla ya kuhitimu kwa watoto wa kike zaidi ya 300 kwenye mafunzo juu ya madhara ya ukeketaji baada kuzikimbia familia zao kwa kuogopa kukeketwa, amesema watoto hao wamekeketwa katika kipindi cha mwezi Desemba, mwaka jana na kwamba vyombo vya dola vinaendelea na msako wa mangariba wengine wanaodaiwa pia kuhusika kufanya ukatili huo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Sihaba Nkinga, akizungumza wakati wa hafla hiyo katika Kituo cha Masanga, Tarime, amesema kuwa kila mwaka duniani watoto wa kike zaidi ya milioni mbili wako katika hatari ya kukeketwa, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi hizo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma linalomiliki kituo hicho Padri Ernest Kamugisha, ameupongeza uongozi wa serikali wilayani Tarime kwa jinsi unavyopambana na vitendo hivyo vya ukeketaji kwa watoto wa kike,licha ya vikwazo vingi vinavyotolewa na wazee wa mila wakiwemo baadhi ya viongozi wa kiasiasa katika Wilaya ya Tarime.

Chanzo: ITV

Comments are closed.