The House of Favourite Newspapers

Marefa Msituharibie Uhondo wa Dabi ya Kariakoo

0

LEO ndiyo leo pale Chang’ombe Wilaya ya Temeke, ni siku ambayo shuguli zote nchini husimama kwa dakika tisini kupisha shughuli moja tu na si nyingine ni mechi ya watani wa jadi Simba wakiwa wenyeji wa Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

 

Utamu wa mchezo huu huwa unachagizwa kwa kiasi kikubwa na upinzani wa timu hizi kuanzia nje ya uwanja ambapo tambo za mashabiki na wanachama wa mapacha hawa wa Kariakoo kwa kiasi kikubwa huwa zinanogesha mchezo huu mkubwa zaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Maandalizi ya vikosi vya timu zote mbili kuelekea mchezo huu yamezidi kunoga ambapo Simba wamejichimbia kule Bunju kwenye viwanja vya Mo Simba Arena huku Yanga wakijichimbia kule Avic Town ilipo kambi yao wakiendelea na maandalizi kuelekea mchezo huu.

Jambo lingine ambalo linakwenda kuinogesha dabi hii ni uwepo wa makocha wawili ambao wataviongoza vikosi vya Simba na Yanga kwenye mechi ya watani kwa mara ya kwanza, makocha hao ni Didier Gomes wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga ambao watakuwa na kazi ya kutoa maelekezo kwa wachezaji wao kwa dakika zote tisini kuhakikisha wanaondoka na matokeo kwenye mechi hiyo.

 

Kwa misimu mingi kwenye mechi za Simba na Yanga kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu waamuzi wanaopewa jukumu la kusimamia sheria 17 za soka kushindwa kuzitafsiri vyema na kusababisha kuharibika kwa ladha ya mchezo husika kwa ujumla.

 

Kwa mfano mechi ya mzunguko wa kwanza Yanga SC ilipata mkwaju wa penalti ambao kwa marejeo ya picha haikuwa penalti na hii ilitokana na mwamuzi kushindwa kuwa kwenye eneo la tukio kwa wakati, hivyo hivyo kwa upande wa Simba msimu uliopita Meddie Kagere aliangushwa nje ya eneo la hatari lakini mwamuzi aliamuru ipigwe penalti.

 

Hivyo basi waamuzi mnapaswa kuwa makini kwenye mchezo huu, tambueni mmepewa dhamana kubwa ya kusimamia sheria 17 ndani ya dakika tisini hivyo msiwe sehemu ya mchezo huu kupoteza ladha.

 

Simamieni sheria kwa kuzingatia haki na bila kupendelea upande wowote ili ambaye atastahili kupata matokeo apate kihalali na si kwa makosa ya waamuzi ambayo pia kwa kiasi kikubwa yanaweza kuwaharibia taswira yenu.

 

Ni lazima mtambue kuwa mmebeba jukumu zito ambalo mnapaswa kuwa makini kwani hii ni njia kwa nyie kupata fursa ya kuchezesha mechi kubwa kwenye mashindano makubwa barani Afrika, kwani kwa miaka mingi Tanzania tumekuwa tukishuhudia waamuzi kutoka nchi nyingine wakipata fursa hii adhimu na waamuzi wetu wakiishia kuchezesha mechi za ndani.Mwisho mashabiki wa Simba na Yanga tambueni mpira una matokeo yake hivyo msiende uwanjani na matokeo yenu mfukoni.

BESELA NA HUSSEIN MSOLEKA

Leave A Reply