The House of Favourite Newspapers

Marekani Yaiwekea Vikwazo Uturuki

0

SERIKALI ya Marekani imetangaza rasmi kuiwekea vikwazo Uturuki baada ya Ankara kutekeleza mpango wake wa ununuzi wa mfumo wa kijeshi wa ulinzi wa anga ujulikanao kama S-400 kutoka nchini Urusi.

 

Takribani mwaka mmoja na nusu baada ya Uturuki kununua mfumo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump  ametangaza rasmi vikwazo kwa taifa hilo ambalo pia ni nchi mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya nchi za Magharibi (NATO).

 

Chini ya sheria ya vikwazo iliyopitishwa na Bunge la Congress mwaka 2017 ijulikanayo kama Countering America’s Adversaries Through Sanctions Act (CAATSA), vikwazo vimelilenga shirika linalohusika na masuala ya ununuzi lililo chini ya Wizara ya Ulinzi ya Uturuki pamoja na maafisa wa ngazi za juu akiwemo rais wa shirika hilo.

 

Vikwazo hivyo vinamaanisha kuwa shirika hilo limefutiwa leseni za ununuzi wa bidhaa kutoka nchini Marekani likiwemo zuio la kupokea mkopo unaozidi dola milioni 10 kutoka katika benki za Marekani sanjari na zuio la mikopo kutoka katika mashirika ya fedha ya kimataifa kama vile World Bank.

Vikwazo pia vimejumuisha kuzifungia mali pamoja na viza kwa maafisa wa juu wa shirika hilo.

 

Leave A Reply