Marekani yapeleka nyambizi nyingine Korea Kusini ikipeleka ujumbe dhidi ya vitisho vya Korea Kaskazini
Nyambizi hizi zimeongeza hatua ya washirika kuonyesha nguvu za kijeshi ili kukabiliana na vitisho vya nyuklia vya Korea Kaskazini.
Nyambizi hiyo ya USS Annapolis iliwasili katika bandari ya Kisiwa cha Jeju kiasi cha wiki moja baada ya nyambizi USS Kentucky kutia nanga katika bandari kuu ya Busan.
Kentucky ilikuwa ni nyambizi ya kwanza ya Marekani yenye silaha za nyuklia kuwasili Korea Kusini tangu miaka ya 1980. Korea Kaskazini imejibu kuwasili kwake kwa kufanya majaribio ya makombora ya balistiki na ya masafa marefu ikiwa ni kuonyesha kwa namna fulani kuwa inaweza kufanya mashambulizi ya nyuklia dhidi ya Korea Kusini na meli za kijeshi za Marekani.
Baina ya kurusha makombora hayo, waziri wa ulinzi wa Korea Kaskazini alitoa tishio lisilo la moja kwa moja akisisitiza kuwasili kwa nyambizi Kentucky huko Korea Kusini kunaweza kuwa ni sababu kwa Korea Kaskazini kutumia silaha za nyuklia dhidi yake.
Korea Kaskazini imekuwa ikitumia matamshi kama hayo siku za nyuma, lakini taarifa hiyo ilionyesha kwa kiwango gani mahusiano yamekuwa si mazuri hivi sasa.
Nyambizi Annapolis, ambayo kazi yake kubwa ni kuangamiza meli na nyambizi za maadui, inaendeshwa na vinu vya nyuklia lakini imebeba silaha za kawaida.
Nyambizi Annapolis hasa ilitia nanga huko Jeju kupakia mahitaji, lakini Jang Do Young, msemaji wa jeshi la Korea Kusini, alisema Majeshi ya Marekani na Korea Kusini wanafanya mazungumzo iwapo waandae mafunzo yanayohusisha nyambizi hizo.