The House of Favourite Newspapers

Marioo Alianzia kwa Mama Ntilie Hadi Kuwa Staa

0

MIONGONI mwa wasanii wa muziki wa Kizazi Kipya walioliteka anga la Bongofleva hapa nchini ni Marioo. Haikuwa ajabu kuona Simba Sports Club ikimtumia msanii huyu kwenye tamasha la Simba Day kwani ukiwasha runinga yako au akisikiliza redio au tembelea kurasa za mitandao ya kijamii, kote huko utakutana na kazi ya Marioo.

 

Kipaji, uchapakazi na kutokata tamaa, ni kati ya mambo yanayomfanya kijana huyu kutokea katika maisha ya chini na kuwa gumzo kwenye gemu ya muziki wa kizazi kipya. Anasema alianza kazi hii kwa kuwaandikia wasanii wengi ngoma kali zilizotamba.

 

Sasa Marioo anafahamika kwa ngoma zake kali kama ‘Dar Kugumu’, ‘Manyaku’, ‘Ifunanya’, ‘Inatosha’, ‘Raha’, ‘Chibonge’ alioshirikishwa na Abbah Process na wimbo mpya alioshirikishwa hivi karibuni wa ‘Weka’ wa msanii nguli nchini, Dully Sykes.

 

Marioo ambaye jina lake halisi ni Omari Mwanga niliwahi kuzungumza naye na akasema alizaliwa mwaka 1995 jijini Dar es Salaam na akiwa bado mtoto mdogo, wazazi wake walimpeleka kuishi kwa bibi yake, Rufiji mkoani Pwani.

 

Anasema baada ya kumaliza elimu ya msingi na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari, alilazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja na ndipo alipoamua pia kujihusisha na muziki. Akifafanua zaidi alikuwa na haya ya kusema:

 

“Napambana sana kwenye muziki kwani kabla ya hapa nilishawahi kufanya kazi za kwa mama ntilie mgahawani,” anasema Marioo.

 

“Katika kipindi ambacho nimeanza kujitambua mama alinipeleka kwa bibi yangu Kibiti, huko nikasoma shule ya msingi na sekondari na nikaishia kidato cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali za maisha.

 

“Kwetu tupo watoto watatu, mimi ni wa mwisho. Baba yangu alikuwa kondakta na alishafariki dunia. Mama yangu yupo, naye alikuwa anafanya kazi kiwandani huko Vingunguti,” anasema Marioo.

 

Anasema kuingia kwake kwenye muziki kulitokana na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na changamoto za kifamilia. Anasema jina Mario (linatamkwa Marioo) limetokana na jina lake halisi ya Omari, akiitoa herufi ya kwanza “O” na kuipeleka mwisho wa jina.

 

Anasisitiza Marioo yake si ile inayotumiwa kimjini mjini ikimaanisha vijana wa kiume wanaopenda kuteleza kimaisha au maisha ya mteremko ya kulelewa na wanawake wenye vipato vikubwa.

 

Anasema baada ya mapambano ya muda mrefu katika muziki alipata bahati ya kujiunga na kituo cha kuendeleza vipaji vya muziki cha Tanzania House of Talent (THT), ambacho kilikuwa kinamilikiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba (marehemu).

 

Anasema huko alikutana na wasanii ambao tayari walitoka kimuziki na kufanya kazi nao, ikiwamo kuwatungia nyimbo.

 

Mbali na kuimba, Marioo ni mwandishi wa nyimbo za wasanii na ameandika baadhi ya ngoma kali zilizotamba kama ‘Banana’ ya Janjaro, ‘Nampa Papa’ ya Gigy Money, ‘Wasikudanganye’ ya Nandy, ‘Nabembea’ ya Ditto, ‘Pambe ya Christian’ Bella, ‘Mchakamchaka’ ya Shilole, ‘Bado’ ya Mwasiti na Billinas na nyingine.

 

Anasema hachagui aina ya nyimbo, anatumia beats ndiyo anaandika ngoma. Baada ya kuwaandikia nyuma ya pazia wasanii kadhaa nyimbo zilizotamba huku yeye akiwa hafahamiki, hatimaye akaamua ajitose kuimba. Na hakika ulikuwa ni uamuzi sahihi, kwani tangu hapo ametamba na kujulikana.

 

Hata hivyo, kati ya vitu anavyofurahia ni kufanya kazi na Dully Sykes kwani alikuwa anamfuatilia tangu siku nyingi katika muziki wake na ndiye aliyemsaidia kufika alipo sasa.

 

“Nakumbuka niliwahi kumsikilizisha kazi zangu kipindi cha nyuma na kuniahidi kunisaidia, nikakaa naye kwenye studio yake pia alinisaidia kama Sh500,000 niongezee kwenye kutengeneza video.” Anasema Marioo.

 

Hata hivyo, kutokana na kutoa nyimbo mfululizo, Marioo amekanusha habari za baadhi ya watu wanaodai ataishia kupotea kama wengine hasa Aslay ambaye aliachia nyimbo mfululizo hadi kuishia njiani.

 

Hata hivyo, Aslay aliibuka na kudai aliibiwa daftari lake la nyimbo na baada ya kulipata ndipo aliamua kutoa mfululizo ili mwizi wake asitumie mashairi yake hayo na baada ya kuisha sasa anatoa kwa wakati.

 

Anasema ngoma ya ‘Chibonge’ ambayo ameshirikishwa na Abbah Process imempa heshima ambayo hakuwahi kufikiria kama ataipata katika tasnia ya muziki.

 

“Kikubwa ambacho najivunia katika ngoma ya ‘Chibonge’ ni heshima niliyoipata. Wengi wamegundua uwezo wangu katika kuimba kupitia wimbo huu,” anasema Marioo.

 

Anasema ameweza kufanya vizuri kwenye muziki wake kutokana na nidhamu na ndio pia iliyomwezesha kufanya video bure kutoka kwa mtayarishaji Adam Juma ya wimbo wake wa kwanza wa ‘Dar Kugumu’.

 

“Nilikuwa nimemsindikiza mshkaji wangu mmoja kwenda kurekodi nyimbo zake. Katika mazingira hayo ya studio nikakutana na jamaa mmoja anaitwa Tunchi Master ambaye aliniambia huwa wanarekodi kwa Sh300,000 ila akaniambia nilipe nusu. Nikajichanga nikalipa nikafanya wimbo ila tatizo likawa kwenye ‘mixing’, alinizungusha sana,” anasema.

 

“Kuna siku Abbah aliusikia wimbo wangu akaupenda, akakubali kunifanyia ‘mixing’ na kuanzia hapo akaniambia niwe msanii wake, tukawa tunafanya kazi na ndio hivyo tukatoa wimbo wa ‘Chibonge’ na namshukuru sana kwani amenifanya kuwa msanii mkubwa sasa.”

 

Anasema kutokana na sasa kuingia kwenye kuimba na yupo chini ya Hanscana, anapowaandikia wasanii nyimbo zake huwatoza kuanzia Sh1 milioni.

 

“Kwa sasa siwezi kufanya kazi kwa ajili ya kujulikana, niliowapatia wanatosha, mtu anayehitaji wimbo ajipange kifedha ama tuandikishiane mkataba kwa ajili ya mapato yatakayopatikana kutokana na wimbo huo na sasa nawatoza Sh1 milioni,” anasema.

 

Kuhusu msanii Amber Lulu kuhusishwa na yeye anasema ukaribu wake naye ulitokana na shughuli zao za muziki lakini si kitu kingine.

 

“Nimejiwekea malengo katika muziki ambayo nimeanza kuyatimiza, hivyo sitaingia katika ulimwengu wa mapenzi mpaka sanaa itakaponilipa,” anasema Marioo.

MAKALA; ELVAN STAMBULI, BONGO

Leave A Reply