The House of Favourite Newspapers

MARIOO ANAVYOPINDUA BONGO FLEVA

MUZIKI ni ajira lakini pia ni biashara kubwa ndiyo maana nchini Nigeria wanaichukulia ‘serious’ tofauti na wengi wanavyoiona!  Kila mwaka wanazaliwa wasanii wapya ambao wanakuja kuwa wakubwa na kukimbiza ndani na nje ya nchi ndiyo maana huwezi kushangaa kuna kipindi wanaibuka hata watano au saba kwa mpigo na wote wakakubalika kinomanoma.

Tumeona kipindi wanaibuka Davido, Yemi Alade, Wizkid na nwengineo ambao leo hii ni wasanii wakubwa waliovutiwa kuingia hadi kwenye albamu ya Beyonce ya The Lion King. Kwa mwaka huu nchini humo kuna wasanii wengine wamezaliwa na tayari wameshaanza kusumbua katika soko la muziki ndani na nje ya nchi kama Maddtonic, Bella Alubo, Zlatan, Fire Boy DML, Rema na Singha.

Kibongobongo pia wasanii wengi wamekuwa wakizaliwa lakini siyo kwa kiwango cha kutoboa kimataifa, tumeona wasanii wachache kati yao wakiendelea kudumu kwenye gemu. Omary Ally Mwanga. Yes! Najua utashangaa kuliona hili japo mtaani huko Temeke alipokulia wanalitambua sana! Unaweza kumuita kwa jina jingine Marioo.

Ni zao jipya katika Muziki wa Bongo Fleva mwenye kipaji cha hali ya juu katika kuimba na kuandika mashairi. Marioo amejizolea umaarufu baada ya kuwatungia wasanii wengi wakubwa kama Nampa Papa wa Gigy Money, Pambe wa Christian Bella, Nabembea ya Ditto, Bado ya Mwasiti, Sawa ya Msami na Wasikudanganye ya Nandy.

Wachache wanalitambua hili kwamba hadi wale wakongwe kuna muda wanapungukiwa busara za kuandika mashairi na hivyo kuomba msaada ili kuendelea kupeta kimuziki. Ndio hivyo basi. imepata fursa ya kukutana na msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye pia Mungu amemjalia kipaji ambacho ni cha hadhi ya juu kuliko watu wanavyofikiria.

Kwao nyumbani, Temeke, mkoani Dar es Salaam, wazazi wake wanamuita Omary Ally Mwanga. Lakini kutokana na kipaji chake ambacho kwa sasa kinamueka mjini, ameamua kuwa na jina jingine maarufu kama Marioo.

Over Ze Weekend limefanya mahojiano na Marioo anayekimbiza na ngoma kibao kama Ifunanya, Wauwe, Yale, Inatosha na Chibonge ambapo amezungumza mengi kama ifuatavyo;

Over Ze Weekend: Jina la Marioo lilikuja vipi kwako?

Marioo: Ni jina langu la kazi lililotoka kwenye jina langu halisi la Omary. Nakumbuka kuna kipindi niliwahi kutengenezewa beat enzi hizo natoka kimuziki prodyuza akaniambia aniandike kwa jina gani kwenye wimbo wangu maana kuna Omary wengi kama Dimpoz na wengineo basi wakanitania au tukuite Marioo wote wakacheka kuanzia hapo nikawa naitwa Marioo.

Over Ze Weekend: Ilikuwaje ukaanza kuwaandikia wasanii mashairi?

Marioo: Mimi kuandika mashairi siyo kazi ngumu, ilikuja tu kama fursa na mimi nikaitumia nakumbuka nilikutana na Kapasta ambaye ni meneja wa wasanii akanikutanisha na Nandy nikamuandikia ile Wasikudanganye nikatoboa kuanzia hapo watu wakawa wananifuata wenyewe.

Hadi sasa napokea simu za watu wengi sana hususan wasanii na mameneja wao kwamba niwaandikie na mimi naona faraja kwa hilo na kwa hatua ambayo nimepiga na siwezi kuacha kwa sababu inaniingizia pesa nzuri.

Over Ze Weekend: Chaji yako ni shilingi ngapi unapowaandikia wasanii wakubwa?

Marioo: Kwa kila mashairi ninayoyaandaa kwa ajili ya msanii, gharama zinaanzia shilingi milioni 1.

Over Ze Weekend: Unaweza kutuambia siri ya wewe kutoboa kimuziki?

Marioo: Kikubwa kuwa na nidhamu. Mimi kwa mfano wimbo wangu wa kwanza kabisa wa Dar Kugumu, nimefanya video bure bila hata shilingi mia. Adam Juma aliamua tu kunisaidia baada ya kugundua kipaji changu na pia nidhamu kazini.

Over Ze Weekend: Tangu umetoka kimuziki, nyuma yake nani alikuwa akikusaidia?

Marioo: Wapo wengi tu kuna Abbah Process (prodyuza) amenisaidia sana hadi kufikia hapa nilipo leo pia kwa wasanii wakongwe Dully Sykes aliwahi kunisaidia sana.

Nakumbuka niliwahi kumsikilizisha kazi zangu kipindi cha nyuma na kuniahidi kunisaidia, nikakaa naye kwenye studio yake pia alinisaidia kama shilingi 500,000 niongezee kwenye kutengeneza video.

Over Ze Weekend: Wasanii wapi wa kubwa Bongo unatamani kuwaandikia ngoma?

Marioo: Hapana! Mtu yeyote akipendezewa ninachokifanya katika uandishi wangu na tukipa-tana vizuri nafa-nya.

Over Ze Weekend: Aina ipi ya ngoma ambayo huwezi kuiandika?

Marioo: Bahati nzuri mimi naandika miziki mingi kwa sababu natumia beats na mizuka ya beat ndiyo inanifanya niandike ngoma.

Over Ze Weekend: Madogo wapo wengi wanafanya vizuri ukiwemo wewe, kuna msanii yeyote tishio kwako anakuumiza kichwa?

Marioo: Wote wanaofanya vizuri wananiumiza kichwa kwa sababu natamani nifanye vizuri zaidi yao. Naweza kusema ni watu ambao tupo pamoja tunawasiliana kama kina Mabantu, Mbosso naamini wananchi wanaona ninachokifanya na wanakipenda.

 

Comments are closed.