The House of Favourite Newspapers

‘Masaji ni tiba kubwa kwa wanamichezo’

SUALA la massage ‘masaji’ ni kitu ambacho kimekuwa na taswira tofauti katika jamii ya Afrika ikiwemo Tanzania, wengi wamekuwa wakijua ni kitendo cha kujifurahisha lakini kiafya na kwa mtu wa michezo ni kitu muhimu na kina faida kubwa.

 

Happiness Charles Mtuya ni mtaalam wa masaji ambaye anamiliki kituo cha huduma hiyo, anafafanua kuhusiana na umuhimu wa huduma hiyo kwa wanamichezo na mtu mwingine yeyote na kutoa dhana kuwa ni kitu cha kujifurahisha tu ambacho kinafanywa na watu wenye fedha za ‘kupoteza’.

 

“Masaji ni ukandaji na usuguaji wa sehemu ya mwili kwa kutumia mikono au mashine maalumu. Huduma hii hutolewa kwa malengo mengi yakiwemo kuondoa maumivu katika sehemu fulani ya mwili, kulainisha misuli iliyokaza, kuondoa uvimbe, kuondoa uchovu wa mwili, kutibu jeraha, kurelax na kutibu saratani kwa kuondoa seli mfu.

“Kuna faida nyingi ambazo mwanamichezo anaweza kuzipata anapofanyiwa huduma hiyo na ndiyo maana mara kadhaa ninapopata nafasi nimekuwa nikitoa elimu kwa wanamichezo kufanya masaji, kwani hiyo ni sehemu ya tiba na ni kama mtu anavyolifanyia gari ‘service’, ndivyo mwili nao unatakiwa kupata huduma hiyo.

 

“Mwanamichezo anapokuwa kazini misuli inakuwa bize, inakaza, unapofanya masaji inakurahisishia kupitisha mzunguko wa damu na ndiyo maana unaona wachezaji wakubwa wa Ulaya ni kawaida kufanyiwa humuda hiyo kitu ambacho kwa hapa kwetu ni tofauti,” anasema Happiness anayemiliki kituo cha Biashara Happiness Massage Clinic.

Happiness (31) ambaye kituo chake kipo Ilala jijini Dar es Salaam ndani ya Hoteli ya Lamada, anasema ana uzoefu na kazi hiyo ambayo aliianza tangu akiwa na umri wa miaka 15, amewashauri Watanzania kuacha dhana kuwa masaji ni sehemu ya ngono na kushauri Serikali kuwa wakali kwa wale wote ambao wanachafua huduma hiyo kwa kufanya mambo ambayo yapo kinyume cha maadili.

 

“Unajua mtaalam wa masaji kama ilivyo kwenye kituo chetu kabla hajakupatia huduma lazima ajue afya yako na kukupa ushauri, mfano kuna watu wana presha nao wana masharti yao ya kupata huduma hiyo, lakini wale ambao hawazingatii weledi wamekuwa wakitazama fedha tu bila kujali afya ya mteja wao.”

 

Aidha, amewashauri wanamichezo, wasanii na watu wengine maarufu kuwa mfano wa kuigwa kwa kujitokeza kupatiwa huduma ya masaji, kwani kwa wao kufanya hivyo watakuwa sehemu nzuri ya kuhamasisha jamii kuondoa dhana potofu kuhusu masaji.

“Katika kituo chetu kitu cha kwanza kabla ya kumuajiri mtu tunazingatia taaluma yake, afya na nidhamu ya kazi kwa kuwa kama hautakuwa makini ni rahisi kuharibu kazi.

 

“Muhimu nashauri Serikali kutupa nafasi sisi wenye taaluma hii kuwa na vituo ndani ya hospitali, kwani kwa sasa mazingira hayaruhusu na nilishawahi kupeleka ombi hilo lakini likakataliwa wakidai wao wana wataalam wao, lakini ni vema tukapewa nafasi nafikiri tuna kitu tunaweza kusaidia jamii.

 

Happines anasema wwao wanaendelea kutoa huduma zao vizuri katika jamii na kumekuwa na watu wengi wakijitokeza kuhitaji huduma hiyo, ambapo kwa sasa anafikiria kuongeza idadi ya watoa huduma. “Kwa anayehitaji huduma, ushauri na tiba za Happiness Massage Clinic, tunapatikana kwa namba 0715343161 au afike Lamada Hoteli tunapatikana muda wote saa 24,” alisema Happiness.

 

Akizungumzia kuhusu masaji, Daktari wa Yanga, Edward Bavu, anasema: “Hii tunapowafanyia wachezaji inasaidia sana kwa njia mbalimbali. Kuufanya mwili wake kuwa kwenye hali nzuri kwa maana ya kulainisha misuli na kuufanya mfumo wa damu kuwa mzuri. Inasaidia sana kuufanya mfumo wa damu kufanya kazi yake vizuri.

 

“Tunawafanyia wachezaji katika mazingira mbalimbali, kipindi cha mechi, mazoezini au hata mapumziko na huwa tunamfanyia mtu ambaye anahisi hayupo sawa. Haifanywi mara kwa mara, lakini hufanywa pindi tu inapotokea uhitaji huo.”

Na Mwandishi Wetu.

Comments are closed.