The House of Favourite Newspapers

Masauni Amuagiza IGP Sirro Kumsimamisha Kazi Mkuu wa Chuo

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro kufanya mabadiliko ya uongozi kwenye Chuo cha Polisi Dar es Salaam kutokana na kukiuka maagizo yake katika ujenzi wa mabweni chuoni hapo.

 

Pia, Masauni amemuelekeza IGP Sirro kumuondoa Mkuu wa Chuo hicho, Antony Ruttashuburugukwa na kumshusha cheo kutokana na kosa hilo.

 

Akizungumza leo Jumatano Novemba 27, 2019 akiwa chuoni hapo, Masauni amesema alielekeza katika ujenzi huo watumike wafungwa kufanya kazi za vibarua ili kuokoa fedha lakini mkuu huyo wa chuo hakutekeleza agizo hilo.

 

“Rais alikubali kutupatia Sh700 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, tuliangalia na kuona tunaweza kuokoa Sh210 milioni za kuwalipa vibarua kwa kuwatumia wafungwa.”

 

“Nilizungumza na kamishna wa magereza akasema hilo linawezekana hivyo nikamuelekeza mkuu wa chuo kufanyia kazi suala hilo lakini leo nimekuja nakuta hali hii hakuna wafungwa,” amesema Masauni.

Wakati Masauni anakagua ujenzi huo alikuta vijana wakifanya kazi na alipowahoji walimuleza kuwa wao ni vibarua wanaolipwa kwa siku.

 

Katika maelezo yake mmoja wa vibarua hao alionekana kutokuwa na utaalam wowote na alipelekwa hapo na mtu aliyemtoa gereji. Majibu hayo yalionekana kumkasirisha Masauni, “Ina maana wewe umechukuliwa huko hufahamu chochote umeletwa hapa, haya ni mambo gani.”

 

Comments are closed.