The House of Favourite Newspapers

Zahera arejea tena Bongo, Simba Yatajwa

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alfajiri ya leo Jumatano, ametua Bongo huku akihusishwa kutakiwa kujiunga na Simba.

 

Inaelezwa kuwa Zahera anakuja nchini kwa ajili ya madai yake na Yanga baada ya kutimuliwa lakini taarifa kutoka ndani ya Simba zinadai kuwa baadhi ya viongozi wa Simba waliwahi kumtaja kwenye kikao kimoja kizito lakini wengi wakapinga.

 

Aussems na Simba kwa sasa hawapo katika wakati mzuri baada ya kocha huyo kusimamishwa na mtendaji mkuu wa timu hiyo kufuatia kuondoka nchini wiki iliyopita bila ya ruhusa kutoka kwa mabosi zake.

 

Zahera alitakiwa kufika jana Jumanne nchini akitokea kwao DR Congo alipokwenda kwa ajili ya majukumu ya timu ya taifa lakini haikuwezekana baada ya kuachwa na ndege kabla ya kuanza tena safari yake ya kuja nchini.

 

Kocha huyo ameliambia Championi Jumatano kuwa alitakiwa kutua nchini jana lakini alishindwa kufika kwa wakati baada ya kuchelewa ndege hali iliyopelekea kuanza utaratibu safari yake upya jana.

 

“Nilikuwa nifike huko leo (jana) lakini haikuwezekana kwa kuwa nilichelewa ndege kwa sababu ya foleni na huku kuna mvua zinanyesha ila nitaingia kesho alfajiri kwa kuwa ndiyo saizi naelekea uwanja wa ndege kwenda Kenya kabla ya kufika huko,” alisema Zahera ambaye hakuweka wazi kinachomleta Bongo ingawa anatajwa kuja Simba.

 

Championi lilimtafuta meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu kwa lengo la kutaka kujua ujio wa Zahera kutokana na kuhusishwa kutakiwa Simba alisema:

 

“Zahera hana uwezo wa kuifundisha Simba ni kitu ambacho hakiwezekani aliyekupa taarifa atakuwa amekudanganya.

 

“Zahera hajawahi kuwa na mkataba mpaka anakuja Yanga zaidi ya kufanya kazi kwa kujitolea sasa mtu kama huyo anawezaje kuifundisha Simba,” alisema Rweyemamu.

Comments are closed.