The House of Favourite Newspapers

Mashabiki Simba, Yanga Jumapili Muonyeshe Si Wale Kama Wa Jana

Kikosi cha Yanga.

KESHOKUTWA Jumapili shughuli nyingi sana zitasima­ma, kama itakuwa ni rasmi au kimyakimya lakini kwa kuwa watani wa jadi Simba na Yanga wanakutana, kwa anayependa mpira, lazima atakuwa anataka kufuatilia kwa ukaribu.

 

Simba na Yanga maarufu kama Kulwa na Dotto wa­takuwa wanakutana katika mechi ambayo itaamua mam­bo mengi ya Ligi Kuu Bara ambayo kama mmoja ata­poteza, atakuwa amekuwa ametengeneza jambo ambalo litakuwa linatengeneza ugu­mu kwake.

Kikosi cha Simba SC.

Kama Simba itashinda, maana yake itakuwa imefiki­sha pointi 62 na kuifanya Yanga izidi kukata tamaa kupambana na kuipata, hivyo itakuwa imejiwekea mazin­gira mazuri ya kutangaza ubingwa kama itaendelea kucheza karata zake vizuri katika mechi nyingine mbili tu za mbele.

 

Yanga nayo ikishinda, itakuwa imetengeneza mam­bo mawili muhimu kwao, kwanza ikiwa ni kujiweka ka­tika nafasi nzuri ya kuikamata Simba na pili, kuamsha pre­sha upande wa pili ambayo kama wakishindwa kuidhibiti, basi wapoteze mwelekeo.

Hizo zikawa hesabu za kila upande kwa timu kwa maana watakuwa wanataka kushin­da kwa gharama yoyote ile. Hivyo lazima wako makini sana katika maandalizi yao kabla ya mchezo huo wa ke­shokutwa.

Wakati hao wanafanya hivyo, suala linafuatia kwa wale ambao watakuwa wana­kwenda uwanjani kwa ajili ya kushuhudia burudani hiyo ya watani wa jadi.

 

Mechi ambayo itakuwa na uamuzi wa mambo mengi sana kuhakikisha yanak­wenda kuonekana hadharani. Mashabiki watakaokwenda uwanjani ndio ninaotaka ku­zungumza nao leo kwamba wanakwenda kwa ajili ya bu­rudani.

 

Wao wanachokifuata ni kuburudika pia kuziunga mkono timu zao ili kuhak­ikisha zinaibuka na ushindi kwa kuwa kila mmoja anajua faida za ushindi ni ipi baada ya mchezo huo kama nilivy­okutajia hapo mwanzo.

Kazi ya kushangilia si laz­ima kutukanana, wala kazi ya kushangilia si lazima ku­umizana. Mashabiki wengi wa mpira hapa nyumbani, wamekuwa na tabia ambazo si za kiungwana ambazo hu­sababisha wengine kuumia au kupata matatizo.

 

Shabiki anayeamini kum­tukana mwenzake ndiyo ush­abiki, au kumpiga na kumuu­miza mwingine ndiyo furaha, ni ujinga wa kupindukia am­bao tumekuwa tunaendeke­za na unapoteza maana ya upenzi wa mpira.

 

Kumbuka kila aliye uwan­jani hapo ni mwanadamu muhimu kama si kwako basi kwa ndugu zake.

Kumbuka kila aliyekuja uwanjani ana haki ya kufura­hia na kurejea nyumbani aki­wa salama. Hivyo, kila mmoja anapaswa kuheshimu utu wa mwenzake.

 

Ushabiki mnaweza kuzo­doana, kutaniana na baada ya mechi mkakumbatiana, kumpoza aliye na majonzi ya kupoteza, kumpongeza aliyeibuka na ushindi au ku­peana pole na hongera baada ya sare.

 

Nimeeleza mara nyingi sana kuhusiana na mashabiki kuonyesha wao wanazipenda timu nyingine huku wakitaka na wengine waone kwamba wanazipenda kweli.

Ushabiki unakuwa si kwa sababu ya mhusika, badala yake hata furaha yake, ana­taka ionekane kwa wengine ndiyo ikamilike.

 

Hivyo, kama ni shabiki wa Simba, akimtukana wa Yanga mbele ya mashabiki wengine wa Simba anaona kama ame­fanya jambo kubwa sana la kusifiwa, hali kadhalika wa Yanga akifanya hivyo kwa yule wa Simba.

Unaona Afrika Kusini, mashabiki wa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates wanach­anganyika siku ya mechi, tu­naona Rwanda, Rayon Sports na APR wanakuwa pamoja na hakuna kutukanana badala yake ni ubishi wa mpira.

 

Sisi hatufanyi hivyo, haina maana ni utamaduni kupi­gana. Badala yake hatukuwa sahihi na tunapaswa kubadi­lika.

Kwenda uwanjani na ku­rudi salama ni jambo jema, kushinda au kupoteza na hata ikiwa sare ni mambo ya mpira. Itakuwa vizuri kama mtaonyesha nyie ni mashabiki wa timu kongwe na mna mawazo chanya kuhusiana na mpira na up­endo badala ya mpira kuwa uadui tu.

Hoja Yangu Na SALEH ALLY

Comments are closed.