The House of Favourite Newspapers

Mashabiki wa Man U Wakinukisha, Mechi na Liverpool Yaahirishwa

0

MAELFU ya mashabiki wa Manchester United wamevamia kwenye Uwanja wa Old Trafford huku mashabiki wapatao 200 wakiingia uwanjani na kuvamia eneo la kuchezea kwa ajili ya kushinikiza mmiliki wa timu hiyo, familia ya Glazers kuachia timu yao.

 

Mashabiki hao wenye hasira pia walizuia basi la wachezaji kuondoka kwenye Hoteli ya Lowry kwenda uwanjani kwa ajili ya kuvaana na Liverpool ambapo mchezo huo ulipangwa kuanza majira ya saa 12:30 jioni ya jana pale Olds Trafford.

Mashabiki waliokuwa wakiandamana kwa amani walijikusanya nje ya uwanja huo wenye jina la utani la ‘Theatre of Dreams’ kwa ajili ya kushinikiza, wakati Kocha Ole Gunnar Solskjaer akitaka maandamano yao yawe ya amani.

 

Lakini ghafla hasira ilionekana kupanda kwa mashabiki hao, walijikuta wakianza kurushiana makondo, wakati wengine wakirusha vitu vilivyofanana na fataki.

Maandamano hayo yamekuja baada ya uamuzi wa wamiliki wa United, pamoja na vilabu vingine vitano vya Ligi Kuu ya England, kujiunga na European Super league mapema mwezi uliopita kabla ya vilabu vyote kujitoa katika mashindano hayo.

 

Katika picha za video, mashabiki hao walionekana wakilazimisha kuingia hadi katika eneo la kuchezea wakirusha fataki katika majukwaa huku wakipiga kelele kushinikiza familia hiyo ya Marekani kuachia timu yao.

 

Fataki hizo pia zilionekana kurushwa katika stuidio za matangazo za Sky Sports, eneo ambalo alikaa mchambuzi na mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher.

 

Mwamuzi wa mchezo huo Michael Oliver na nahodha wa zamani wa Man United, Gary Neville walikuwa miongoni mwa wale ambao magari yao yalizingirwa na mashabiki walipokua wanaingia uwanjani, lakini hakuna taarifa yoyote ya watu kujeruhiwa wala uharibifu wa mali.

 

Sky Sports ilieleza katika matangazo yake kwamba kamera zao zilikuwa hatarini, kwani zilisukumwa na hata vibendera vya kona na vinasa sauti vingine vilichukuliwa na waandamanaji.

 

 

The Manchester Evening News iliripoti kwamba takribani mashabiki 10,000 walikuwa katika kampeni hiyo ya kuwaondoa Glazers, wakati wimbi kubwa la mashabiki likiwachoka wamiliki hao raia wa Marekani.

 

Kwa mujibu wa Sky Sports, mchezo huo umeahirishwa kutokana na vurugu hizo mpaka siku nyingine utakapopangwa tena. 

Leave A Reply