The House of Favourite Newspapers

Mashine ya Korosho ‘Yachinja Mtu, Afariki, Yajeruhi Wawili

SADA Juma (28) ni mkazi wa Kata ya Msinjahili, Manispaa ya Lindi mkoani hapa ambaye hivi karibuni alifariki dunia kwa ‘kuchinjwa’ na mashine ya kubangulia korosho na kuacha simanzi nzito.

Tukio hilo lilijiri Aprili 13, mwaka huu wakati Sada akiwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Jengo la Viwanda Vidogo-Vidogo (SIDO) mjini Lindi.

 

Mbali na Sada kuaga dunia kwenye eneo la tukio, pia watu wengine wawili walijeruhiwa vibaya wakiwa ndani ya jengo hilo wakiendelea na mafunzo kwa vitendo.

Meneja wa SIDO Mkoa wa Lindi, Chacha Mwita hakuwa tayari kuzungumza kwa undani juu ya ajali hiyo kwa kile alichoeleza kuwa suala hilo lipo mikononi mwa Polisi.

 

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Pudensiana Protas, mbali na kutaja jina la marehemu, pia aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Almandus Urio (27), mkazi wa Wilaya ya Nachingwea na Aisha Ahmadi (30), mkazi wa Kata ya Nyangao, Lindi-Vijijini.

Kamanda Protas alisema kufuatia tukio hilo majeruhi wote pamoja na mwili wa marehemu walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine kwa ajili ya matibabu na mwili kuhifadhiwa. Majeruhi mmoja, Aisha alitibiwa na kuruhusiwa huku Urio akilazwa na kuendelea kupatiwa matibabu.

 

Alisema mafunzo hayo ya ubanguaji korosho yanayoendeshwa na (SIDO) kwa kushirikiana na wataalam kutoka Wizara ya Kilimo na Chakula yalijumuisha washiriki wajasiriamali wapatao 13 kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Lindi ambazo ni Nachingwea, Lindi, Ruangwa, Liwale na Kilwa.

 

Kamanda huyo alisema baada ya uchunguzi, mwili wa Sada ulikabidhiwa kwa ndugu na jamaa zake kwa ajili ya mazishi.Katibu wa Afya wa Hospitali ya Sokoine, Boniface Lyimo alikiri kupokelewa kwa majeruhi hao na kueleza kuwa Aisha alipata majeraha sehemu ya jicho la mkono wa kulia ambapo alitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani kwake.
Lyimo alisema Urio alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo miguu, mapajani kifuani na tumboni.

“Kifo cha Sada kimechangiwa zaidi na kupoteza damu nyingi baada ya kukatwa shingoni na kooni na kitu chenye ncha kali,” alisema Lyimo. Alisema tayari mwili wa Sada ulichukuliwa na ndugu zake kwa ajili ya mazishi. Kutokana na maumivu makali yaliyokuwa yakimsumbua majeruhi Urio alishindwa kuzungumza na mwandishi wetu hospitalini hapo.

 

Meneja wa Shirika la SIDO Mkoa wa Lindi, Kasisi Mwita alipoombwa kupata kauli yake, hakuwa tayari kuzungumzia namna ilivyotokea kwa kile alichokieleza amebanwa na sheria. “Hapana, siruhusiwi kuongea kitu, sheria imenifunga, ukitaka maelezo zaidi muone RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) au RC (Mkuu wa Mkoa),” alisema Mwita.

 

Ndugu na jamaa wa Sada walieleza kusikitishwa na taarifa ya kifo cha ndugu yao, kwani alikuwa kiungo muhimu kwa upande wao. Hata hivyo, baadaye ilijulikana kuwa mwili wa Sada ulichukuliwa na ndugu zake na kuzikwa kwenye makaburi yalipo Sabasaba katika Manispaa ya Lindi.

Stori: SAID HAUNI, Lindi

USHUHUDA: WASTARA ALIVYOKATIKA MGUU, MSAADA WA SHIGONGO NA WEMA

Comments are closed.