The House of Favourite Newspapers

ALIYEBOMOLEWA NYUMBA KWA JIWE LA MGODINI ALIA KUTOSWA!

WAZIRI Biteko upo? MZEE Boniphace Mhere Mgaya, (pichani) mkazi wa Kijiji cha Nyabichune, Kata ya Matongo- Nyamongo, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, ana miaka saba akihangaikia malipo ya madhara ya kuharibiwa nyumba yake ya bati katika eneo hilo yaliyosababishwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaochimbwa na Kampuni ya ACACIA.

 

Mgodi huo ulikiri kumharibia nyumba yake kutokana na jiwe lililotoka mgodini likiviringika, kuangukia na kubomoa paa la nyumba yake kutokana na ulipuaji wa baruti wakati wa uchimbaji wa dhahabu mwaka 2012 lakini tangu wakati huo, Mgaya hajawahi kufidiwa.

 

“’Baada ya mgodi kulipua baruti na jiwe kubwa kuangukia nyumba yangu ya bati na kubomoa, ningekuwepo ndani huende lingenipata kichwani na kufa lakini Mungu kaniokoa.
“Maofisa wa Mgodi wa North Mara walifika na kushuhudia uharibifu huo ambapo walisaini kwa kukiri kutokea madhara hayo.

 

“Nilifikisha taarifa kwa viongozi wa kijiji changu na kata kisha kwa mkuu wa wilaya yangu, mkoa wangu na hata kwa waziri wa madini na walisaini kwenye kitabu changu cha dispachi.
“Mgodi uliahidi kunifidia tangu nikiwa na umri wa miaka 63 hadi leo nina umri wa miaka 70 sijafidiwa na mgodi huo,” alilalamika mzee huyo.

 

Aprili 9, mwaka huu, mzee huyo alimfikishia taarifa na kumkabidhi kwa mkono wake vielelezo na barua za malalamiko yake hayo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Charles Francis Kabeho ambaye aliahidi kumshughulikia suala hilo lililochukua muda mrefu.

Uwazi lilifika kwa mkuu huyo wa wilaya na kumuuliza kuhusiana na madai hayo ambapo alikiri kuyapokea malalamiko ya Mgaya.

Alisema kuwa wakati anayashughulikia, alimtuma mzee huyo awafikishie tena maofisa wa mgodi barua ya madai yake hayo kwa kuambatanisha nyaraka na vielelezo vyote na amefanya hivyo.

 

“Ni kweli mzee huyo alinifikishia madai yake hayo dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wa ACACIA, nilimtaka awafikishie tena barua yake ya malalamiko hayo akiwaambatanishia vielelezo vyake vya vyote vya madai yake,” alisema Kabeho na kuahidi kufuatilia ili apate haki yake.
Aidha mzee huyo ameeleza kuwa, anaamini kwa malalamiko yake hayo, Waziri wa Madini, Doto Biteko atamsaidia.

STORI: IGENGA MTATIRO, MARA

Comments are closed.