The House of Favourite Newspapers

Maskini Rose Muhando, Baada ya Kutoka Hospitali Akutana na Mengine

DAR ES SALAAM: HAYA ni majanga tena! Siku chache baada ya mwimbaji wa nyimbo za Injili, Rose Muhando kutoka kwenye matibabu nchini Kenya huku akiwa amenawiri (shavu dodo), imeelezwa kuwa, msanii huyo atakutana na rungu la watu wanaomdai misala mbalimbali.

 

Kwa mujibu wa chanzo makini, Rose alikuwa akidaiwa madeni na watu mbalimbali waliokuwa wakiandaa matamasha ya Injili na kumlipa fedha lakini walishindwa kumdai alipokuwa mgonjwa lakini walipanga kumdai punde tu atakaporejea.

 

“Yaani walisema akiingia tu nchini wanaye, wanadai chao maana ilikuwa inawauma. Alichukua cha watu halafu akaingia mitini,” kilisema chanzo hicho makini.

Aidha, chanzo hicho kilizidi kuweka wazi kuwa, mbali na watu hao kumshitaki kwenye vituo mbalimbali vya polisi, baadhi yao wamemshitaki katika Chama cha Muziki wa Injili nchini ili kuweza kusaidia waweze kupata haki yao.

Baada ya kupata taarifa hizo, Amani lilimtafuta Katibu wa Chama cha Waimba Injili, Stella Joel ambapo alithibitisha kuwepo kwa mashitaka ya watu tofauti yanayomhusu Rose.

“Ni kweli hayo mashitaka yapo katika chama chetu na wahusika walisema watamdai pindi atakaporejea nchini. Kimsingi mimi nimsihi tu Rose kama amerejea salama, ahakikishe anajichunga asije akaangukia kwenye matatizo yaliyomsababishia alazwe kwa muda mrefu,” alisema Stella.

 

Amani lilijaribu kumtafuta Rose ambaye inasemekana yupo mbioni kurejea nchini kwa njia ya simu lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda hadi tunakwenda mitamboni.

Kwa takriban miezi minne iliyopita, Rose alilazwa jijini Nairobi baada ya kuonekana akiwa na majeraha makubwa na kuombewa na mhubiri wa Kanisa la Evangelism, James Nganga.

Stori: Mwandishi Wetu, Amani

Comments are closed.