The House of Favourite Newspapers

MASTAA BONGO WANAOISHI NYUMBA ZA GHOROFA !

MASTAA kumiliki magari na vitu vya thamani limekuwa ni jambo la kawaida kwani tumekuwa tukiona wengi wakifanya hivyo. Lakini pia kwa staa kufikia hatua ya kumiliki au kupanga jumba la kifahari la ghorofa limekuwa jambo la nadra na inapojulikana hivyo staa huyo huwa gumzo.

Tumeshaona mastaa wengi kama vile Nasibu Abdul ‘Diamond’ akimiliki jumba la kifahari maeneo ya Madale jijini Dar, yupo Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ na wengineo.

Lakini pia wapo mastaa wanaoishi na kumiliki maghorofa. Hawa ni wale ambao wametumia mkwanja wao kujenga nyumba hizo au wamepanga ili kusaka heshima.

Wapo mastaa ambao wamekuwa wakitupia picha mitandaoni wakiwa wamepozi kwenye majumba ya ghorofa lakini mwisho wa siku inabainika aidha wametembelea tu marafiki au ndugu zao wanaoishi kwenye mijengo hiyo ama wanaenda kwa jirani, wanapiga picha kisha wanatupia Insta ili kuwarusha roho watu.

Katika toleo hili maalum, tunakupa listi ya mastaa wa Bongo ambao imethibitika wanaishi kwenye nyumba za kupanga au wanazimiliki wao kwa kujenga ama kununua ambazo ni za ghorofa.

Nyumba hizi nyingi zipo jijini Dar licha kuwepo taarifa kuwa, wapo ambao wanazo zipo mikoani na wengine wanazimiliki jijini Dar lakini hawataki watu wajue kuwa ni zao.

AUNT EZEKIEL

Ni miongoni mwa wakali wa filamu Bongo akiwa amezaa mtoto mmoja wa kike na dansa maarufu wa Diamond, Moze Iyobo.

Aunt na mzazi mwenzake huyo, wanaishi kwenye jumba la kifahari la ghorofa moja lililopo Mwananyamala jijini Dar. Awali staa huyo alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kawaida tu lakini hivi karibuni aliamua kuhamia kwenye ghorofa hiyo.

IRENE UWOYA

Kama ilivyokuwa kwa mastaa wengine, Uwoya naye amepanga jumba la kifahari la ghorofa moja lililopo Makongo juu jijini Dar. Kabla ya kuhamia kwenye mjengo huo, alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kawaida tu iliyopo Sinza jijini Dar.

AY

Ukisema ni mkongwe kwenye Bongo Fleva huwezi kuwa unakosea kwani jamaa huyu ambaye jina lake kamili ni Ambwene Yesaya alianza kitambo kama msanii wa kujitegemea na baadaye akaingia kwenye Kundi la East Coast Team (ECT).

Baada ya ECT kuvunjika, AY aliendelea kufanya muziki kivyake japo wakati mwingine alikuwa akionekana na MwanaFA.  Kwa sasa AY, amehamishia makazi yake nchini Marekani ambapo miezi michache iliyopita alianika mjengo wa kifahari wa ghorofa anaoumiliki ambao anaishi na familia yake uliopo Calabasas, California nchini Marekani.

KIBA

Mjengo wa Kiba ambao upo Tabata-Segerea, maeneo ya Kwetu Pazuri, jijini Dar ni moja kati ya mijengo ya maana ambayo ni gumzo kubwa katika mitaa hiyo.

Ghorofa hiyo ni matunda ya kazi yake ya muziki pamoja na madili mengine na inasemekana aliamua kujenga nyumba hiyo ili angalau kuweka ‘gepu’ na msanii mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye ana mjengo wa maana kule Madale lakini wa kawaida tu.

ESTER KIAMA

Awali alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kawaida maeneo ya Kijitonyama jijini Dar. Dili zake ni za kuigiza na ujasirimali na katika kuonesha kuwa anachokifanya kinalipa, hivi karibuni alihamia kwenye nyumba ya ghorofa iliyopo pande za Mbezi Beach jijini Dar.

Alipozungumza na gazeti hili hivi karibuni staa huyo alisema kuwa, anapenda kuishi vizuri na yuko tayari kufanya kila linalowezekana ale vizuri, aishi pazuri na ikibidi huduma zote za msingi azipate.

EMMANUEL MGAYA ‘MASANJA’

Fani yake ya kuchekesha, uchungaji, kilimo na biashara vimepatia mafanikio makubwa sana. Naye ukirudi nyuma kwenye maisha yake utagundua alitokea familia isiyokuwa na uwezo lakini sasa mbali na kumiliki magari ya kifahari, jamaa ana nyumba zaidi ya moja jijini Dar ila kuna ya ghorofa ambayo ipo Tabata.

Mara nyingi sana mastaa hawa wamekuwa hawako wazi kwenye kuweka gharama walizotumia katika kujenga nyumba hizo na hata wale ambao wamepanga, huwa wagumu sana kutaja kiasi wanachotoa kila mwezi kumpa mwenye nyumba.

 LUCAS MUHAVILE ‘JOTI’

Ukijaribu kufuatilia historia yake unaweza kusema jamaa ni kati ya mastaa ambao hawakuwahi kuwaza kuwa watakuja kuishi maisha ya kishua kama aliyonayo sasa. Ameanzia kwenye maisha duni lakini sasa hivi mchekeshaji huyu asiyeshikika Bongo, anamiliki mjengo wa ghorofa moja uliopo Mtaa wa Nyakwale, Kata ya Kibada Wilayani Kigamboni jijini Dar.

DONGO KWA WALIOPANGA MAGHOROFA

Mara kadhaa imekuwa ikielezwa kuwa, baadhi ya mastaa wanaotumia pesa nyingi kwenye kupanga nyumba za ghorofa, hawawazi kabisa kumiliki nyumba zao, matokeo yake wengine hata viwanja hawana licha ya kuishi kifahari.

Elimu kutoka kwa wataalam wa mambo ya kimaisha imekuwa ikiweka wazi kwamba, hata kama leo unastahili kuishi sehemu nzuri na yenye heshima, bado hutakiwi kutowaza kumiliki nyumba yako.

Hivyo wito unatolewa kwa mastaa wanaoishi kwenye nyumba za kupanga, iwe za ghorofa au za kawaida, kuweka akilini mwao kwamba nao wanatakiwa siku moja kuitwa baba mwenye nyumba. Kuishi maisha yako mpaka unakufa ukiwa kwenye nyumba ya kupanga wakati uwezo wa kujenga nyumba yako unao haiwezi kuleta picha nzuri.

HAMISA MOBETO

Mwanadada huyu ambaye ni mzazi mwenziye na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ wakiwa wamezaa mtoto mmoja, naye ni miongoni mwa mastaa wanaoishi kwenye mijengo ya ghorofa.

Mjengo huo anaoishi Mobeto upo Mbezi Beach na inadaiwa aliyempangishia ni Diamond kwa ajili ya kuwa katika mazingira mazuri ya kumlea mtoto wao aitaye Daylan.

 

 

Stori: Mwandishi Wetu

Comments are closed.