The House of Favourite Newspapers

MASTAA WA KIKE WANAVYOPIGA DILI ZA UBALOZI

ILI uwe balozi wa bidhaa fulani, msanii unatakiwa uwe na mashabiki wengi, uwe na heshima japo kila anayetaka kukupa dili la ubalozi anakuwa na vipaumbele vyake.

Kupitia wasanii hao, wamiliki wa bidhaa ama kampuni zenye bidhaa hizo, huamini kuwa itakuwa rahisi kuzitangaza kutokana na umaarufu, mvuto, na kukubalika kwa mastaa hao.

Mastaa mbalimbali wa kike wamekuwa wakipambana kusaka ‘connection’ za dili za ubalozi kwani zinawaongezea kipato nje ya fani zao japo Kibongobongo mikataba mingi hufanywa siri kati ya msanii na kampuni husika.

Makala haya yanakuletea orodha ya mastaa wa kike waliojinyakulia ubalozi wa bidhaa mbalimbali;

HAMISA MOBETO

Hamisa ni balozi wa kiwanda cha Prima Afro kinachotengeneza rasta zinazoitwa Prima Afro Hair.

Mwaka jana msanii huyu alisaini mkataba wa kuwa balozi katika kiwanda hicho, hata hivyo amekuwa akiziwakilisha vyema nywele hizo kwa kuzisuka kisha kutupia picha mitandaoni hasa kwenye ukurasa wake wa Instagram. Wafuasi wake hupendezwa na nywele hizo, hivyo kutaka wasusi kwenye masaluni kusukwa kama Mobeto.

Hamisa pia ni mwanamitindo anayemiliki duka liitwalo Mobeto Styles na ni mwanamuziki ambaye kwa sasa anakiki na wimbo wake wa Sensema aliomshirikisha msanii Whozu.

ZARI THE BOSSLADY

Ni mwanamama mwenye asili ya Uganda, ni balozi wa Kampuni ya Soft Care inayotengeneza taulo za kike (pedi) pamoja na pampers za watoto.

Mrembo huyo aliingia mkataba na kampuni hiyo mwaka jana ambapo lengo la kupewa ubalozi huo ni kuzitangaza bidhaa za kampuni, kutokana na yeye kuwa na mashabiki wengi Tanzania na nje ya Tanzania.

Zari alijipatia umaarufu mkubwa Bongo baada ya kuwa mama watoto wa staa mkubwa kunako Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ hivyo kutokana na umaarufu wa msanii huyo, naye alipata mashabiki wengi sana ndani na nje ya nchi. Zari ni mama wa watoto watano, lakini pia ni mfanyabiashara na mwanamuziki.

GIGY MONEY

Gigy ni balozi wa taulo za kike (pedi) za Soft Plus, amesaini mkataba na kampuni hiyo takriban wiki mbili zilizopita. Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Gigy amekuwa akitupia picha na video zinazoitangaza bidhaa hiyo yenye kaulimbiu inayosema ‘Rafiki wa Kweli.’ Msanii huyu ameonekana kuja kwa kasi kwani alikuwa mwanamuziki wa kawaida tu lakini baada ya hapo aliingia kwenye tasnia ya filamu na kuanza kuigiza kwenye Tamthiliya ya Kapuni ambako pia anafanya vizuri. Gigy ni mama wa mtoto mmoja (Mayra) na kwa sasa anatamba na wimbo wake wa Shoga.

NANDY

Nandy ni balozi wa kampuni za Azania zinazotengeneza sabuni za unga za King Limau na Marhaba, ameingia mkataba wa kuwa balozi katika kampuni hizo hivi karibuni (takriban wiki mbili zimepita). Nandy amekuwa akizitangaza sabuni hizo zenye kaulimbiu inayosema ‘Ni Zaidi ya Usafi’ kwa kuzitupia kwenye ukurasa wake wa Instagram mara baada na kuingia mkataba. Mbali na ubalozi huo, msanii huyu ni mmiliki wa Nandy Beauty Products na African Princess Music, lakini pia ni mwigizaji katika Tamthiliya ya Huba na mwanamuziki anayetamba na ngoma yake ya Kiza Kinene aliyowashirikisha Sauti Sol.

Makala: Irene Marango

Comments are closed.