MASTAA WANAORUDISHA WALICHOKIPATA KWA JAMII

WASWAHILI wanasema, “kutoa ni moyo si utajiri”. Hiyo humaanisha kwamba si kila anayetoa msaada kwa jamii ana fedha nyingi sana kuliko wengine, bali ni moyo wake wa upendo na kujali furaha ya wengine.

 

Katika jamii yetu kuna watu wengi wa namna hiyo; unaweza kuwaweka katika makundi mbalimbali. Mfano wafanyabiashara, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, wasanii nk. Unashangaa mtu anaishi maisha ya kawaida kabisa, lakini akikutana na mwingine ana uhitaji, anakuwa na moyo wa kusaidia. Huo ndiyo unaoitwa moyo, si utajiri!

 

Kwa upande wa mastaa wapo wenye moyo wa kusaidia na wengine hawana. Hata hivyo wakati fulani, kusaidia huwa kunatokana na namna mtu alivyoguswa na uwezo alionao mhusika. Ijumaa limeangazia kwa kina wasanii wa fani mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine, wanaonekana kuguswa sana na jamii na kurudisha sehemu ya mafanikio yao kwao.

 

Ukiachana na wasanii kadhaa wakiwemo Jacqueline Wolper, Wema Sepetu, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, Aunt Ezekiel (wote wa filamu) na wengine kadhaa kushiriki maadhimisho ya siku zao za kuzaliwa katika vituo vya watoto yatima na kutoa misaada mbalimbali, wapo mastaa ambao wamekwenda mbali zaidi.

 

Mastaa hao ni mfano tu wa wengi kutoka fani mbalimbali ambao huamua kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum katika siku zao za furaha. Mbali na mastaa, hata watu wasio maarufu wengi siku hizi wamejenga utamaduni huo, jambo ambalo ni zuri.

 

Kwa hakika wapo mastaa wengi ambao ama wanajishughulisha na kuisadia jamii au wanarudisha sehemu ya walichopata kwa jamii lakini hapa nimewataja wachache ambao wanajulikana zaidi na misaada yao imekuwa wazi na moja kwa moja kwa jamii.

 

HOYCE TEMU

Ni Miss Tanzania 1999, ambaye ni miongoni mwa warembo wachache kutoka Miss Tanzania walioweza kutunza umaarufu wao kwa muda mrefu. Ni mwanamitindo msomi, akiwa na Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano ya Umma.

 

Amepata kufanya kazi katika taasisi mbalimbali nchini, lakini mwaka 2011 aliamua kuanzisha kipindi cha televisheni kiitwacho Mimi na Tanzania ambacho huibua matatizo ya watu wenye uhitaji na kusaidia kupatiwa misaada na watu mbalimbali.

 

Kupitia kipindi chake hicho, Hoyce ameokoa maisha ya Watanzania wengi ambao wamepatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mwaka 2014 katika Siku ya Wanawake Duniani, Taasisi ya MISA ilimtangaza kama mwanamke mashuhuri kutokana na mchango wake katika kuisaidia jamii.

DIAMOND PLATNUMZ

Staa huyu wa Bongo Fleva, ambaye jina lake halisi ni Nasibu Abdul, yupo mstari wa mbele katika kusaidia jamii. Imekuwa kawaida kwake kusomesha watoto, kusaidia yatima, kutoa mitaji kwa wanawake wajasiriamali wadogo na watu wa jamii yake aliokua nayo Tandale, jijini Dar es Salaam.

 

Machache kati ya mengi aliyofanya ni kugawa zawadi katika Sikukuu ya Idd, mwaka huu, nyumbani kwao, Tandale. Tukio jingine ni lile la kutoa misaada katika siku yake ya kuzaliwa, mwaka huu. Aligawa bima za afya kwa watoto 300, mitaji ya biashara kwa kina mama 200, bodaboda kwa vijana 20 na ukarabati wa Shule ya Msingi Tandale, ambayo alisomea hapo zamani.

 

Kwa upande wa matibabu amewasaidia wengi, lakini wa karibuni kusaidiwa ni msanii Hawa Said ‘Hawa wa Nitarejea’ ambaye alimsadia matibabu ya ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua, nchini India. Hawa aliambatana na Meneja wa Diamond, Babu Tale.

FARAJA NYALANDU

Alitokea Miss Tanzania mwaka 2004, wakati huo akijulikana kama Faraja Kotta. Ni mume wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu kabla ya kujiuzulu. Tangu amevua taji lake la urembo mwaka 2004 amekuwa akijiweka karibu na jamii.

 

Kwa sasa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Shule Direct inayodili na kuwasaidia wanafunzi. Mwaka 2014, Faraja alizindua kitabu chake cha Unaweza chenye lengo la kumsaidia mwanafunzi wa shule ya msingi kuweza kujisomea. Asilimia 50 ya mauzo ya kitabu hicho alisaidia Chuo cha Ualimu Korogwe kukarabati chumba cha Teknohama.

JACQUELINE MENGI

Ni mshindi wa taji Miss Tanzania mwaka 2000, ambaye pia alijiingiza kwenye muziki wa Bongo Fleva baadaye. Kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Amorette ya jijini Dar es Salaam. Anayo matukio mengi ya kusaidia jamii, lakini tukio la hivi karibuni katika birthday ya Diamond linaweza kuwa mfano.

 

Katika hafla hiyo, Jacqueline aliahidi kujenga maktaba katika Shule ya Msingi Tandale. Yapo matukio mengi ya kusaidia jamii ambayo Jacqueline amekuwa akifanya.

 

WENGINE

Mastaa wengine ambao wamekuwa wajihusisha kusaidia jamii ama moja kwa moja au kupitia mifuko mbalimbali wanayoiendesha ni pamoja na Miss Tanzania mwaka 2001, Millen Happiness Magese, mwanamitindo Hamisa Mobetto, Miss Tanzania namba 2 mwaka 2006, Jokate Mwegelo na wengineo.

Toa comment