The House of Favourite Newspapers

Matarajio Yanapoenda Tofauti, Migogoro Huibuka

0

HAKUNA siku ambayo huwa najisikia furaha kama inapofika Ijumaa, unajua kwa nini? Kwa sababu napata nafasi ya kujumuika na wewe msomaji wangu katika ukurasa wetu huu mzuri. U hali gani msomaji wangu? Bila shaka u mzima wa afya.

 

Kwa wewe ambaye afya inaleta mgogoro, au unasumbuliwa na masaibu ya hapa na pale, nakupa pole na kukuombea kwa Mungu akufanyie wepesi. Yote kwa yote, nakukaribisha kwenye zulia jekundu, tuzungumze, kujadiliana na kuelimisha na mambo mbalimbali ya kimapenzi.

 

Ipo dhana moja ambayo sidhani kama wengi wetu tunaielewa, ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo inayochangia uimara au udhaifu wa uhusiano wa kimapenzi. Kimaumbile, kuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume na hilo halipingiki lakini tofauti hizo zinaenda mbali zaidi na kugusa pia kwenye uhusiano wetu wa kimapenzi.

 

Leo sitaki kuzungumzia tofauti hizo kwani ni mada inayojitegemea lakini kidogo ningependa tujadiliane kuhusu tofauti za matarajio na mahitaji zinazokuwepo wakati mwanaume na mwanamke wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi.

 

Swali jepesi kwako msomaji wangu; wakati unaanzisha uhusiano na mwenzi wako, nini yalikuwa matarajio yako ya baadaye? Kama wewe ni mwanamke, ulitegemea mpenzi wako, mchumba wako au mume wako atakuja kukufanyia nini baadaye?

 

Kwako mwanaume je, ulitegemea mpenzi wako, mchumba wako au mke wako atakuja kukufanyia nini kwenye uhusiano wenu wa kimapenzi? Baada ya kuingia kwenye uhusiano sasa, je, yale matarajio uliyokuwa nayo wakati mkianzisha uhusiano, yametimia, yanatimia au yana dalili za kutimia au ndiyo yameota mbawa?

Bila shaka kila mmoja atakuwa na jibu lake na kubwa zaidi, wanaume watakuwa na majibu yanayoshabihiana na wanawake vivyo hivyo!

 

Tukianza kwa upande wa wanawake, ipo wazi kwamba huwa wanakuwa na matarajio kemkemu kwa wanaume wanaoanzisha nao uhusiano wa kimapenzi lakini kubwa, huwa wanatarajia kutimiziwa mahitaji yao yote muhimu, ya lazima na yale yasiyo ya lazima.

Huwa wanatarajia kuheshimiwa, kupewa ulinzi muda wote, kuoneshwa kwa vitendo kama wanapendwa, kupewa maisha mazuri kama kuishi kwenye nyumba nzuri, kuwa na usafiri wa kutembelea (ingawa si wote), kuwa na watoto wanaosoma shule nzuri na mambo mengine ya kifahari.

Anatarajia kwamba utakuwa ukimpa fedha nyingi za matumizi (hata kama na yeye ana kazi yake) na utamshirikisha kwenye mambo makubwamakubwa ya maendeleo.

Hata kama mwanamke wako hajawahi kukwambia, elewa kwamba haya ndiyo matarajio yake. Akikwambia atakuvumilia, anaamini kwamba japokuwa leo mnaishi kwa shida lakini ipo siku utafikia kiwango cha kumpa maisha hayo anayoyaota. (Kama yupo mwanamke ambaye huwa hatarajii haya kutoka kwa mwenzi wake, basi ni mmoja kati ya milioni moja).

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply