The House of Favourite Newspapers

Mateso Juu ya Mateso!

0

NI mateso juu ya mateso! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kusoma habari ya mama huyu ambaye amekatwa miguu yote na kujikuta akiishi maisha ya mateso makuu hapa duniani.

Bibi Estina George (65), mkazi wa Mbezi-Msumi jijini Dar, amejikuta akimwaga machozi baada ya kukatwa miguu yake yote kufuatia kushambuliwa na magonjwa mazito matatu.

 

Akilisimulia Gazeti la Risasi Mchanganyiko mkasa mzima wa nini kilichotokea, bibi huyo anasema tatizo lake lilianza kidogokidogo miaka kadhaa iliyopita.

Anasema miguu yake hiyo ilianza kuvimba, kutoa funza kisha kuoza ambapo alizunguka hospitali mbalimbali kabla ya kwenda muhimbili kuchukuliwa vipimo.

 

Baada ya vipimo ilibainika kuwa alikuwa akisumbuliwa na presha, kisukari na moyo kuwa mkubwa.

“Walisema magonjwa hayo ndiyo chanzo cha mimi kuvimba miguu, kutokwa funza na kuoza, hivyo madaktari wakalazimika kunikata mguu mmoja.

 

“Baada ya mguu mmoja kukatwa, tatizo lilihamia mguu mwingine ndipo na wenyewe ukakatwa na sasa kama unavyoniona, sina miguu, siwezi kufanya chochote bila kubebwa na mjukuu wangu,” anasema mama huyo huku akimwaga machozi mengi.

 

Anasema katika familia yao, walizaliwa watoto tisa, lakini wote walishafariki dunia hivyo amebaki peke yake.

Anasema katika maisha yake, alifanikiwa kupata watoto wawili, lakini mmoja alifariki dunia, akabaki na mmoja ambaye naye alimtelekeza kutokana na matatizo yake hayo.

 

Tangu mtoto huyo amtelekeze mama yake huyo, yapata miaka mitatu sasa bila mawasiliano naye na wala hajui alipo.

“Ila yule mwanangu aliyefariki dunia, aliniachia mtoto mmoja (ndiye huyo mjukuu anayemsaidia) ambaye naye kama unavyotuona, hatuna kipato chochote, tunategemea tu wasamaria wema watakaoguswa na tatizo langu,” anasema bibi huyo na kuongeza;

 

“Najua Rais Magufuli ni kiongozi mwenye huruma kwa wananchi wake, namuomba baba anisaidie angalau nipate chakula na matibabu.

“Vivyo hivyo namuomba Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar), naye najua ni mtu anayesaidia wengi wenye shida kama mimi, namuomba mwanangu, atakaposoma au kutazama habari yangu kwenye Global TV, basi anihurumie maana ninapita kwenye mateso juu ya mateso.”

 

Angela Swai ni mjukuu wa bibi huyo anayeishi naye akimsaidia kwa kila kitu.

Kwa upande wake, Angela anasema hana ndugu yeyote wa kuwasaidia, kwani hamfahamu hata baba yake kwa kuwa alimkataa tangu akiwa mdogo na hajawahi kumuona.

 

Angela anasema kuwa, yeye na bibi yake huyo wanapitia mtihani mkubwa kwa sababu kuna wakati anashindwa kumuinua bibi yake akiwa mwenyewe na hana mtu yeyote wa kumsaidia.

 

“Naombeni ndugu zangu mtusaidie maana tumekwama kwa kweli,” anasema Angela akilia kwa uchungu.

Kwa yeyote anayeguswa na habari hii, anaweza kumsaidia bibi huyu kwa kuwasiliana na namba 0788 413 625 iliyosajiliwa kwa jina la ANGELA SWAI.

Kwa video ya habari hii, tembelea Global TV kwenye YouTube.

Anna Mbawala, Risasi

Leave A Reply