The House of Favourite Newspapers

Mateso ya Mtoto Huyu… Mungu Tenda Miujiza  

0

MUNGU tenda muujiza! Ndiyo maneno unayoweza kutamka kutokana na mateso anayopata mtoto Musa Abel (2) ambaye anasumbuliwa na tatizo la njia ya haja kubwa.

Mtoto huyo anaishi na bibi yake, Rahabu Malugu (40), mkazi wa Mtaa wa Shinyanga B, Kata ya Nyakafulu Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.

 

Akizungumza kwa huzuni, Malugu alisema mjukuu wake huyo alizaliwa na tatizo la njia ya haja kubwa yaani hana kabisa kutokana na utumbo mpana kukomea njiani hivyo anakuwa akipata matso makubwa.

Aliendelea kueleza kuwa kutokana na tatizo hilo madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando iliyopo jijini Mwanza walimwekea mrija tumboni ambao anautumia kwa kujisaidia.

 

“Mjukuu wangu hajisaidii haja kubwa kwa njia ya kawaida kama binadamu wengine, tangu azaliwe anasumbuliwa na njia ya haja kubwa, baada ya kuona mtoto hajisaidii kama ilivyo kwa watoto wachanga ndipo alipimwa katika Hospitali ya Somanda Mkoa wa Simiyu, lakini tatizo halikuonekana,” alisema bibi wa mtoto huyo na kuongeza;

“Alipopewa Rufaa kwenda Bugando madaktari bingwa walimpima na kugundua kuwa utumbo mpana ulikomea njiani na utumbo mwembamba ambao hausaidii chochote ndiyo ukaendelea, walichukua uamuzi wa kumfanyia upasuaji mdogo pembeni ya tumbo na kumwekea mpira ili aweze kujisaidia wakati wanatafuta njia nyingine ya kumsaidia,” alisema kwa Rahabu.

 

Rahabu alisema, mwanaye Pendo Buyamba ambaye ndiye mama mzazi wa Musa hana chochote huku baba wa mtoto naye akiwa haeleweki ambapo zinahitajika shilingi milioni mbili ili mtoto aweze kufanyiwa upasuaji wa kumrejesha kujisaidia kwa njia ya kawaida.

“Mwenyewe sina kazi maalum badala yake naokota mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu nikiuza ndipo nakula na familia yangu,” alisema.

 

“Kiukweli mateso anayopitia mtoto huyu ni makali mno. Nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidi ili mjukuu wangu aweze kuwa kama binadamu wengine, kwa chochote walichonacho ili niweze kupata fedha hizo za matibabu,” alisema Rahabu.

Kwa yeyote aliyeguswa na tatizo la mtoto huyu na una chochote cha kumsaidia wasiliana na bibi yake kwa simu namba, 0759 035 779.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Shinyanga B, Musa Bukwimba alikiri mwanamke huyo kuteseka na mtoto huyo ambaye ananyanyapaliwa na watoto wenzake hadi watu wazima kwa kuona kinyaa pindi anapojisaidia haja kubwa hasa anapoachwa na wenzake wakati mwanamke huyo akiwa ameenda kusaka tonge.

 

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa jamii kuona tatizo hilo kubwa na waungane kwa pamoja kuokoa uhai wa mtoto huyo ambaye anaumia kutokana na hapo anapotumia kujisaidia siyo mahali pake na kuongeza kuwa anaungana na mtoto huyo kuwaomba Watanzania waguswe na hali yake ili awezekupata matibabu na awe kama watu wengine.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi anasema kuwa ofisi yake ipo bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa matibabu ya mtoto huyo yanapatikana huku akimwandikia kibali kitakacho mruhusu bibi wa mtoto kuzunguka na kibakuli kuomba msaada kwa wasamaria wema na wenye huruma ya Mungu katika wilaya nzima ya Mbogwe.

 

“Tumuombee kwa Mungu mtoto wetu atarejea katika hali yake, atajisaidia kwa njia ya kawaida kabisa nahisi kiwango cha fedha kilichohitajika kwa madaktari hao kitapatikana. Mungu ni mwema, sisi Watanzania ni watu wenye huruma. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ipo pamoja na familia yako, Watanzania wakikusaidia usiitumie kwa matumizi yako,” alisema DC Mkupasi akimweleza bibi huyo wa mtoto huyo.

STORI: PAUL KAYANDA, SHINYANGA

Leave A Reply