The House of Favourite Newspapers

Matola Asimulia Alivyopewa Laki Tano na Mkapa

0

KUFUATIA kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, familia ya michezo imesema kuwa itamkumbuka rais huyo kwa mengi ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Taifa, pamoja na kuwa karibu na watu wa michezo na jamii kwa jumla wakati wa utawala wake.

 

Mkapa alidumu madarakani kwa muda wa miaka 10, kuanzia 1995 hadi 2005 ambapo alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi Ijumaa jijini Dar es Salaam.

 

Seleman Matola, Kocha Msaidizi wa Simba, amesema: “Wanamichezo tunamkumbuka kwa juhudi zake ikiwa ni pamoja na kutengeneza Uwanja wa Taifa na wengi wanautumia kwa sasa. Pia wakati nikiwa timu ya Taifa enzi za utawala wake tulichukua ubingwa, alitualika katika Ukumbi wa Karimjee, kila mchezaji alipewa shilingi laki tano kama zawadi.

”Juma Abdul, Nahodha Msaidizi wa Yanga alisema: “Tutamkumbuka kwa kutuongoza Watanzania vizuri na kuibakisha amani ndani ya nchi pamoja na Uwanja wa Taifa ambao mpaka sasa tunautumia.

 

Mungu ailaze roho yake pema peponi, Amen.” Salum Kimenya, kiraka wa Prisons, alisema: “Familia ya michezo na Tanzania kwa jumla tunakumbuka mchango wake namna alivyokuwa akiongoza bila upendeleo pamoja na kujali michezo. Ameacha alama kubwa kwetu ya upendo na uongozi bora.

 

”Daruwesh Saliboko, mshambuliaji wa Lipuli, alisema: “Zama za uongozi wake nilikuwa mdogo sana, lakini nilikuwa ninaona juhudi zake hasa kwa kuwa karibu na jamii, pia nimekuwa mkubwa nimeuona Uwanja wa Taifa na nimeutumia pia, ni juhudi zake. Kuondoka kwake ni pengo kubwa, lakini sisi sote ni wa Mungu.

 

Jacob Massawe, Nahodha wa Gwambina FC, alisema: “Kiukweli ni msiba wa Afrika nzima, kwa wanamichezo tutamkumbuka kwa sapoti yake, lakini tutaendelea kumuenzi kwa mambo makubwa aliyofanya kwani alikuwa ni kiongozi bora muda wote.”

 

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, naye amesema: “Rais Mkapa ametuachia majonzi makubwa wadau wa michezo hapa nchini kutokana na mchango wake mkubwa katika kuhamasisha maendeleo ya michezo.

 

“Nakumbuka wakati nikiwa Katibu Mkuu wa FAT (sasa TFF), Tanzania ilifutwa uanachama wa Fifa kutokana na mgogoro uliokuwepo kati ya FAT na serikali, lakini Rais Mkapa alisuluhisha mgogoro ule na tukarudishiwa uanachama wetu. Yapo mengi ambayo ameyafanya yatazidi kukumbukwa ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Taifa.

STORI: LUNYAMADZO MLYUKA NA HUSSEIN MSOLEKA, DAR

Leave A Reply