The House of Favourite Newspapers

Matola: Nawataka Yanga niwanyooshe tena

Kikosi cha timu ya Yanga.

BAADA ya kikosi cha Lipuli FC kutinga Hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Samora, wameibuka na kusema wanatamani Yanga ipenye nusu fainali ili wainyooshe.

 

Kocha wa Lipuli FC, Selemani Matola, amesema wanatambua kwamba mshindi wa mechi ya Alliance dhidi ya Yanga ndiye watacheza naye ila hasira zake bado zipo kwa Yanga na anawaombea washinde wapewe wanachostahili.

 

Matola, kiungo na nahodha wa zamani wa Simba, amesema kuwa wamecheza na timu zote mbili kati ya Alliance na Yanga, wanatambua mbinu zao, hivyo hawana hofu na yeyote watakayekutana naye nusu fainali lazima achapwe.

 

“Wachezaji wangu wamejituma na tumepata matokeo, tunamsubiri mshindi kati ya Yanga ama Alliance tucheze naye ila dua zetu ni kuona Yanga anashinda ili aje hapa Samora apigwe nyingine kisha sisi tusonge mbele.

 

“Tumebakiwa na mchezo mmoja ili kutinga fainali, sasa hapo sioni timu ya kuiogopa, wao kwenye ligi walitufunga bao moja kwao, nasi pia tukawafunga bao moja nyumbani hivyo naamini wakishinda Yanga mchezo wetu utakuwa mzuri na wenye kuvutia, ila natamani washinde nikutane nao,” alisema Matola.

 

Alliance na Yanga zitacheza kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba hatua ya robo fainali na timu itakayoibuka kidedea itamenyana na Lipuli ambayo imeshajikatia tiketi ya nusu fainali Uwanja wa Samora.

Stori: Lunyamadzo Mllyuka, Dar es Salaam

Comments are closed.