The House of Favourite Newspapers

Mauaji ya Askari Kinyogoli kwa Risasi… 15 Mbaroni Akiuwemo Mkewe

0
1Marehemu, Sajenti Ally Salum Kinyogoli.
Watu 15 akiwamo mke wa marehemu, Sajenti Ally Salum Kinyogoli wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na tukio la kuuawa kwa askari huyo wa kikosi cha usalama barabarani usiku wa kuamkia jana.
Kinyogoli aliyezikwa jana saa 10 jioni kwenye Makaburi ya Mzambarauni, Kitunda, Dar es Salaam alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kutoa taarifa kuhusu hali ya usalama barabarani katika vyombo vya habari.
Kinyogoli aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, Chatembo Kata ya Mwandege, Mkuranga mkoani Pwani mbele ya mtoto wake, mwenye umri wa miaka kumi na moja.
Akizungumzia kukamatwa kwa mjane huyo, Kamanda wa Kipolisi Temeke, Gilles Muloto alisema:
“Sidhani kama mnaweza kuzungumza naye kwa sababu hao waliomshikilia ni polisi na wanakwenda naye kituoni. Hata hivyo, mimi siyo msemaji wa hili anayeweza kulizungumzia ni Kamanda wa Mkoa wa Pwani.”
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi ambaye hakuwapo msibani alipopigiwa simu ilipokewa na mpambe wake ambaye alisema: “Mkuu leo amebanwa na vikao vingi kuna Mwenge mkoani kwake na hili tukio la kusikitisha.”
Mgogoro wa kifamilia 
Mama mlezi wa marehemu, Coletha Ndima alisema mara ya mwisho kuonana na Kinyogoli ni juzi wakati marehemu alipopeleka baadhi ya samani zake kwa kile alichodai mke wake mkubwa alikuwa akiziuza.
“Hatujui kama kuna mgogoro lakini Kinyogoli aliwahi kutuambia kuwa anataka kuoa mke wa pili, sijui alishaoa, kwa sababu alisema atakuja kumtambulisha mchumba lakini hakufanya hivyo,” alisema.
Ndima alisema marehemu aliwahi kumwambia kuwa ana mgogoro na mkewe mkubwa lakini hajui ni wa nini.
Mmoja wa polisi ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema polisi wanamshikilia mama huyo kwa kuwa yeye ndiye aliyemuita Kinyogoli aende nyumbani kwake na mauti kumfika.
“Marehemu alitengana na mke wake mkubwa, lakini siku moja kabla ya kifo, mama huyo alimuita akimwambia watoto wamemkumbuka, usiku huohuo, ndipo walipomuua,” alisema.
Mtoto asimulia mauaji yalivyotokea
Mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Ebenezer iliyopo Mwandege alieleza kuwa watu wawili walifika nyumbani hapo na kumtaka amuite baba yake.
“Nilipoingia ndani kumuita baba, nilimkuta anatandika kitanda, baba akaniambia waambie nakuja, wakati natoka, baba naye alikuwa nyuma yangu, lakini niliwakuta wale watu safari hii wamevaa ninja (mask) lakini kabla ya hapo walikuwa hawajavaa,” alisema.
Alisema watu wale walianza kumkaripia baba yake wakimtaka awape funguo ya gari lakini alikuwa akibishana nao na kisha kuanza kupambana nao lakini walimpiga bastola ya kichwani na mbavuni.
 
“Wakati baba anapambana nao alikuwa anawauliza nimefanya nini, lakini hawakumjibu, alianza kupiga kelele, wanangu nakufa, wanangu nakufa,” alisimulia kuongeza:
“Ujue baba alishawaweza wale, lakini walivyoona anawashinda nguvu waliamua kumpiga bastola.”
Baba wa marehemu, Salum Kinyogoli aliwataka polisi kufuatilia suala hilo ili wahalifu hao wapatikane.
Dada wa marehemu, Zainab Kinyogoli aliyeonekana kuchanganyikiwa kutokana na msiba huo alikuwa akilia mfululizo huku akisema: “Ally aje nimbebe, nimemuachia ziwa, nimembeba.” 
Maelezo ya polisi 
Awali, Kamanda Mushongi aliwaambia waandishi wa habari mjini Kibaha kwamba wauaji hao walifika nyumbani kwa askari huyo wakitumia pikipiki aina ya Boxer na waliingia ndani kwa kuruka uzio.
Hata hivyo, wauaji hao walipofika kwenye gari hilo hawakufanya lolote bali walitelekeza ufunguo huo na kutokomea.
“Naweza kusema ni tukio la kushtukiza kwa kweli kwa sababu ilikua ni muda mfupi tu toka askari aliporudi nyumbani kwake akitokea kazini na hawa wauaji hawakuchukua kitu maana hata ufunguo wa gari waliouchukua pale nyumbani walitoka nao nje na kuuacha,” alisema Mushongi.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: Global TV Online

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE:@shigongotz

Leave A Reply