The House of Favourite Newspapers

MAUMIVU WANAYOPATA WATOTO HAWA… NI ZAIDI YA MATESO

WATOTO wawili wanaogua maradhi tofauti wapo katika mateso makubwa na wanahitaji msaada wa wasamaria wema ili waweze kupona.

Mtoto Mudasili ambaye amezaliwa Septemba 2016 katika Kijiji cha Nampemba wilayani Nachingwea mkoani Lindi, anasumbuliwa na tatizo la uvimbe katika jicho la kushoto.

Mama mzazi wa mtoto, Hadija Said aliliambia Uwazi: “Mwaka jana mwanangu alianza kuwashwa jicho, hali hiyo ilinilazimu kwenda hospitalini huku jicho la mtoto likiwa jekundu mithili ya damu.

 

“Tulipewa dawa, tukarejea nyumbani. Hata hivyo, hazikusaidia. Kadiri siku zilivyosonga, hali ya jicho la mwanangu ilizidi kuwa mbaya huku jicho likitoka nje. Tulikwenda Hospitali ya Ndanda (Masasi-Mtwara) nako tukaambiwa tuende Nyangao (Lindi).

“Siku chache baadaye, tulipewa rufaa ya kwenda Muhimbili huko tuliambiwa mtoto ana saratani ambayo imeenea mwilini, hivyo turejee nyumbani, hakuna tiba mbadala zaidi ya kupata dawa za kupunguza maumivu tu.

 

“Hali ilivyozidi kuwa mbaya, baba wa mtoto alimkana. Mwanangu anapita kwenye maumivu makali mno. Anahitaji msaada wa kiroho na pesa za chakula, huu ni mwaka wa pili sina hata nafasi ya kushika jembe kwa kukosa muda wa kufanya shughuli za uzalishaji, hali inayosababisha familia kukosa mahitaji muhimu.”

Kwa wanaoguswa na habari hii wanaweza kumsaidia mtoto huyu, wawasiliane na mama yake, Hadija Said kwa namba 0654 197 916.

 

Wakati huo huo, Michael Kadungala (15) mwenye ulemavu wa kutoona amewaomba wasamaria wema akiwemo Rais Dk. John Magufuli wamsaidie aweze kupata matibabu ya tumbo kujaa maji.

Kadungala ambaye mpaka sasa ameshatoa zaidi ya lita 100 za maji katika tumbo lake lakini maji bado yamejaa katika tumbo hilo.

Akizungumza kwa taabu na mwandishi wetu, nyumbani kwa mjomba wake, Joshua Msemwa eneo la Ipagala mkoani Dodoma, Kadugula alisema anapenda kusoma lakini anashindwa kutokana na tumbo lake kujaa maji.

 

Alisema alikuwa akisoma katika Shule ya Wasioona ya Buigiri wilayani Chamwino, Dodoma lakini alirudishwa nyumbani kutokana na tumbo kujaa maji.

“Mheshimiwa Rais mimi sioni na wewe ni rais wa wanyonge nataka kurudi shuleni, naumia sana ninapoona wenzangu wanaenda shule, naumia sana naomba nisaidie niweze kupata matibabu, lakini hata wasmaria wengine nawaomba msaada,”alisema huku akilia.

 

Kwa upande wake jomba wake, Joshua Msemwa alisema Kadugula alianza kuumwa 2014 na walimpeleka katika Hospitali ya St Gasper ya Itigi na kutoa lita 28 za maji tumboni na mwaka 2015 walimpeleka katika Hospitali ya St Gemma ya mkoani Dodoma ambapo alipimwa na kuonekana hasumbuliwi na ugonjwa wowote na mwaka jana, 2017 ilibidi wampeleke Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili na kupimwa kila kitu lakini hakuna kitu chochote kilichoonekana.

 

“Zaidi ya kupewa dawa za TB, lakini kila siku amekuwa akitolewa maji tumboni na zimeshafikia lita 100, namuonea huruma sana mjomba wangu kwani haoni. Hivi karibuni tulimpeleka katika Hospitali ya Benjamin Mkapa walipima kila kitu lakini hakuna kilichoonekana,” alisema.

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Wasioona ya Buigiri, Happines Mgombela alithibitisha kuwa Kadugula alishindwa kuendelea na masomo mwaka 2014 akiwa darasa la nne kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa tumbo kujaa maji.

 

Mbunge wa Jimbo la Kilolo ambaye pia ni Balozi wa Wasioona nchini, Venance Mwamoto kutokana na hali ya mgonjwa, amemuomba Rais Dk.John Magufuli na wadau mbalimbali wamsaidie mtoto huyo ili aweze kupatiwa matibabu.

Kwa yeyote anayetaka kumsaidia mgonjwa huyu awasiliane na mjomba wake, kwa namba 0755 09 02 43.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Comments are closed.