The House of Favourite Newspapers

Mauya: Nilishuhudia Mwenzangu Akichomwa Kisu Alipofunga Bao

0

MBIO za usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu Bara 2020/21 zimeanza kwa kasi ndani ya klabu mbalimbali ambazo zimeonyesha nia ya wazi ya kutaka kuboresha vikosi vyao kutokana na upungufu ulioonekana msimu uliopita wa 2019/20.

 

Miongoni mwa klabu ambazo zimeonekana kupania kurejesha heshima kwa kuboresha vikosi vyao ni Yanga ambao Ijumaa iliyopita walitangaza rasmi usajili wao wa kwanza msimu huu kwa kumsainisha kiungo mkabaji wa Kagera Sugar, Zawadi Peter Mauya.

 

Mauya amejiunga Yanga kama mchezaji huru na kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo mpaka mwaka 2022. Championi Jumatatu linakuletea mahojiano ‘Exclusive’ na Mauya ambaye amefunguka mambo mengi baada ya kutua Yanga kama ifuatavyo;

 

KWA KIASI GANI MALENGO YAKO YAMEBADILIKA BAADA YA KUJIUNGA NA YANGA?

“Kila sehemu unapokuwa kuna malengo yake, mfano ni vigumu kukuta timu za daraja la kati zikiwa na malengo ya kutwaa ubingwa kutokana na bajeti ambazo kiuhalisia ni ndogo.

 

“Lakini unapokuwa mchezaji wa Simba, Yanga au Azam lazima kitu cha kwanza ambacho utawaza ni kutwaa ubingwa hivyo hata mimi natamani kutwaa na naamini nitatwaa mataji ndani ya Yanga.

 

JEZI NAMBA SABA INAVALIWA NA BALAMA, UPO TAYARI KUBADILI?

“Kwa kawaida mimi huwa siamini katika suala la namba za jezi, hivyo naweza kutumia jezi yoyote ambayo nitaikuta haivaliwi.

 

UMEJIANDAAJE KUHIMILI PRESHA YA KUCHEZA YANGA?

“Kwanza kujiandaa kisaikolojia kwa kutambua kuwa hali hiyo haiepukiki kwani unapozungumzia klabu za Yanga, Simba na hata Azam bila ubishi unakuwa unazungumzia klabu zenye mashabiki wengi hapa nchini jambo linalozidisha presha ya kupata matokeo.

 

ULIKUWA UNATAMANI KUCHEZA NA MCHEZAJI GANI WA YANGA?

“Siwezi kusema mmoja, kwa sababu Yanga ni timu kubwa na imekusanya wachezaji wengi wa daraja la juu. Mimi huwa nafuraha kubwa pale ninapokuwa sehemu ya mafanikio ya kikosi chochote hivyo nitajisikia furaha kucheza na mchezaji yeyote nitakayecheza naye.

 

UMEJIANDAAJE KUKABILIANA NA USHINDANI WA NAMBA NDANI YA YANGA?

“Mimi ni mchezaji na ili mchezaji yeyote uwe bora ni lazima ukumbane na changamoto, naamini katika eneo ninalocheza wapo wachezaji bora hivyo naamini kuwa ushindani hautakuwa wa mchezomchezo lakini nitapambana kupata nafasi.

 

NINI KINAKUFANYA KUWA BORA?

“Ukiachana na masuala muhimu kama vile msukumo wa familia, chakula na vinginevyo nadhani suala linalonibeba zaidi katika maisha yangu ya soka ni ile hali ya usikivu na kupenda kusikiliza maelekezo ya mwalimu.

 

VIPI KUHUSU MAISHA YAKO BINAFSI?

“Nimeoa na nimejaaliwa kupata mtoto mmoja anayeitwa Lightness Gift Mauya, kwa upande wa mke wangu yeye hapendi kujulikana na ameniwekea ngumu kutaja kwenye vyombo vya habari hivyo kwa kuheshimu hilo nisingependa kumzungumzia.

 

MUDA WAKO WA MAPUMZIKO UNAUTUMIAJE?

“Napenda kupumzika na familia yangu, kusikiliza muziki, kuangalia tamthilia na kusoma sana vitabu vya siasa.

 

KWA NINI SIASA, UNA MPANGO WA KUINGIA KWENYE SIASA BAADA YA KUSTAAFU?

“Ndiyo, unajua mimi nimefanikiwa kupata Elimu ya Masuala ya Utawala na siwezi kuiacha hiyo taaluma iende bure, hivyo nina ndoto ya kuiishi taaluma yangu kwa siku za usoni, kuhusu nafasi gani nitagombea hilo linabaki kuwa siri yangu.

 

TUKIO GANI AMBALO HUWEZI KULISAHAU KWENYE MAISHA YAKO?

“Nisingependa kutaja mahali wala mwaka kutokana na uzito wa tukio lenyewe lakini nakumbuka niliwahi kushuhudia mchezaji mwenzangu akichomwa kisu uwanjani jambo lililopelekea apoteze maisha muda mchache baada ya kufikishwa hospitali.

 

“Chanzo cha tukio hilo ni bao la tatu lililofungwa na huyo mwenzetu ambaye baada ya kufunga alienda kushangilia kwa mashabiki ambao walionyesha kuchukizwa na tukio hilo na ndipo mmoja wao akamchoma kisu, licha ya jitihada za kumpeleka hospitali lakini jamaa alipoteza uhai.

 

UNAMZUNGUMZIAJE KOCHA MECKY MAXIME?

“Ni miongoni mwa makocha bora hapa nchini, anafanya kazi kwa juhudi pia anajua kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati sahihi.

 

UHUSIANO WAKO NA IBRAHIM AJIBU UPOJE KWA SASA?

“Sina ubaya naye, yaliyotokea ilikuwa sehemu ya mchezo na tayari tulishayamaliza (Ajibu alimpiga mabuti kwenye mechi mkoani Kagera), licha ya kwamba hatuna mahusiano ya karibu sana lakini tunapokutana kwenye matukio ya kimichezo huwa tunaongea na kucheka.

 

MALENGO YAKO KIMATAIFA YAKO VIPI?

“Kila mchezaji anatamani kupata nafasi ya kucheza nje, hivyo hata mimi nataka kutumia nafasi yangu ndani ya Yanga kujitangaza kimataifa ili kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa.”

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply