The House of Favourite Newspapers

Mavugo atua Dar Usiku

0

mavugo-agiye-kugaruka-muri-kiyovu-_53f3764f70777Dar es Salaam

ILIBAKI kidogo Simba ilete straika mwingine kutoka Ivory Coast kwa ajili ya kumjaribu na kisha impe mkataba lakini mpango huo umeishia njiani ukiwa kwenye hatua za mwisho baada ya juzi usiku kutua kwa Mrundi, Laudit Mavugo.

Simba ilifikia makubaliano ya kumshusha Muivory Coast huyo kuja kuungana na mwenzake, Blagnon Fredric katika majaribio ya timu hiyo baada ya kuibuka kwa sarakasi nyingi za ujio wa Mavugo aliyekuwa akiichezea Vital’O ya Burundi.

Ujio wa Mavugo unaonekana kuwa unaweza kupoza machungu ya Wanamsimbazi wengi ambao walikuwa wakimsubiri mchezaji huyo kwa hamu lakini taarifa tata za ujio wake zikasababisha kuwepo na kigugumizi baada ya mara ya mwisho kuripotiwa kuwa alienda nchini Ufaransa kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

Mavugo alitua juzi usiku na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye ndiye aliyeondoka naye katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, lakini alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi hakupatikana.

Kutua kwa Mavugo kumekuja siku chache tangu Simba ilipokabidhiwa shilingi milioni 100 kutoka kwa mwanachama wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ kwa ajili ya kuchangia usajili, ikiwa ni mwendelezo wake wa kampeni ya kutaka kununua hisa asilimia 51 za klabu hiyo endapo kutakuwa na mabadiliko ya klabu kuwa kampuni.

Mtu wa ndani kutoka klabuni hapo amelieleza Championi Ijumaa kuwa awali mchezaji aliyekuwa akicheza katika moja ya timu za Misri alishazungumza na uongozi wa Simba juu ya ujio wake lakini sasa mpango huo haupo tena sababu ikiwa ni Mavugo.

“Kulikuwa na taratibu zimeshafanyika kwamba huyo Muivory Coast aje ndani ya siku mbili hizi lakini sasa baada ya kupata taarifa za ujio wa Mavugo na hatimaye akatua kweli ndiyo ikawa sababu ya kusitishwa kwa mpango huo lakini baada ya kuja, sasa amezima hiyo mipango,” alisema kigogo huyo kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Alipoulizwa juu ya Mavugo, Kocha wa Simba, Joseph Omog, alisema: “Niliagiza uongozi uniletee straika mwingine mwenye uwezo wa kufunga mechi nyingi, kama wamemleta huyo Mavugo ni vizuri, nashukuru kwa kutimiza ahadi, mimi simjui lakini naamini atakuwa mchezaji mzuri.” Alipoulizwa Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja naye alisema: “Naamini Mavugo atatusaidia.”

Leave A Reply