The House of Favourite Newspapers

Mawaziri Hawa wa JPM Tunawakumbuka… Nape, Kitwanga, Muhongo na Maghembe

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye.

 

WE Miss Them! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais Dk. John Magufuli kufunga mwaka 2017 kwa utimilifu wa mambo mbalimbali, ikiwemo kushughulikia maeneo yaliyoonesha udhaifu kwa kuwaondoa baadhi ya watendaji wake wakuu wakiwemo mawaziri, naibu mawaziri na baadhi ya watumishi wengine wa umma.

 

Kuondolewa kwa baadhi ya mawaziri hakumaanishi uzembe binafsi wa viongozi hao bali ni utiifu wa kanuni za uwajibikaji ambao umekuwa ukifanywa na watumishi wa umma.

Hata hivyo, duru za kisiasa zinaonesha mawaziri walioondolewa kwenye nafasi wanakumbukwa kwa utendaji wao na kilichotokea ni ajali za kisiasa walizopata bila kutarajia na kwamba zimeandika historia kwa mwaka 2017.

 

Mawaziri na manaibu mawaziri walioondolewa na sasa jamii inawakumbuka (miss them) na wizara zao kwenye mabano ni pamoja na Charles Kitwanga (Mambo ya Ndani), Prof. Jumanne Maghembe (Malisili na Utalii) na George Simbachawene (Tamisemi).

Charles Kitwanga

Wengine ni Mhandisi Gerson Lwenge (Maji), Nape Nnauye (Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni), Prof. Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) na manaibu mawaziri ni Lamo Makani (Maliasili na Utalii), Anastazia Wambura (Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni) na Edwin Ngonyani (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).

 

KITWANGA

Waziri wa kwanza kuonja makali ya Rais Magufuli kwa kutumbuliwa ni Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kitwanga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi alijikuta akiondolewa katika nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa ni kuingia bungeni akiwa amelewa.

 

Kutokana na hali hiyo, alishindwa kujibu kwa ufanisi swali la mmoja wa wabunge lililotaka ufafanuzi kuhusu uboreshaji wa makazi ya askari magereza, hivyo Kitwanga akawa anajibu kwa maneno yasiyoeleweka huku utani ukiwa mwingi, jambo lililosababisha Rais Magufuli kutengua uteuzi wake na kisha nafasi hiyo kuchukuliwa na Dk. Mwigulu Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi, akitokea Wizara ya Kilimo na Mifugo.

 

NAPE

Rais hakuishia kwa Kitwanga, bali aliendelea na fyekeo lake  kwa kumtumbua aliyekuwa Waziri wa Habari, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Machi 23, 2017, ilieleza kuwa rais amefanya mabadiliko kidogo katika Baraza la Mawaziri.

Mabadiliko hayo yalikuwa ni pamoja na kumteua Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi na kumteua Dk. Harrison Mwakyembe kuongoza wizara ya habari.

Kabla ya mabadiliko hayo, Dk. Mwakyembe alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

LWENGE, MAGHEMBE

Mawaziri wengine waliokumbana na fyekeo la Rais Magufuli ni pamoja na Gerson Lwenge aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Ilielezwa kuwa Lwenge na Maghembe waliondolewa katika wizara hiyo kwa kushindwa kwenda na kasi ya rais kiutendaji.

 

MUHONGO

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliondolewa kwenye nafasi hiyo kutokana na sakata la biashara ya madini kuonesha nchi kuibiwa kiwango kikubwa cha madini.

Hatua ya kutumbuliwa kwa Muhongo ilikuja saa chache, baada ya Rais Magufuli kupokea taarifa ya kamati maalumu aliyoiunda kuchunguza mchanga ulio katika makontena ya madini (makinikia) yaliyopo maeneo mbalimbali nchini.

 

Akionesha namna alivyokuwa akimpenda Prof. Muhongo, Mei 24, 2017, Rais Magufuli alisema;

“Nampenda sana Prof. Muhongo, lakini pia ni rafiki yangu, lakini kwa hili akae ajifikirie na bila kuchelewa aachie madaraka.”

Nafasi ya Muhongo ilichukuliwa na Dk Medard Matogolo Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato.

 

SIMBACHAWENE

Rais aliendelea na utumbuaji na panga la kufyeka lilimkuta aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene.

Aliondolewa katika nafasi hiyo baada ya matokeo ya uchunguzi wa kamati zilizoundwa kuchunguza biashara ya madini kuonesha hakusimamia vizuri majukumu yake.

Kwa upande wa Edwin Ngonyani na Anastazia Wambura, nafasi zao zilisitishwa kutokana na kile ambacho rais aliona kinafaa ili kuharakisha zaidi maendeleo ya nchi.

Stori: BRIGHTON MASALU, Dar

Comments are closed.