The House of Favourite Newspapers

Mawaziri wa JPM Waliotumbua Majipu Watetemesha Nchi

0

Waziri Mkuu  aongoza kwa maamuzi magumu

Na Elvan Stambuli

MAWAZIRI wa Serikali ya Awamu ya Tano yenye umri wa miezi miwili wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wameendelea kuzuru maeneo mbalimbali nchini huku ‘wakitumbua majipu.’

Majipu hayo ni yale ya watendaji na viongozi wa taasisi walioshindwa kudhibiti ufisadi au kutuhumiwa kwa ubadhirifu. Hatua hizo za kuwasimamisha kazi watendaji hao na bodi kuvunjwa zimechukuliwa kwa nyakati na mikoa tofauti nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameongoza kwa kutoa maamuzi magumu na ameshatumbua majipu Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania na kusababisha baadhi ya watumishi kufunguliwa mashtaka ya ubadhirifu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar.

Kama hiyo haitoshi, akiwa mkoani Ruvuma wiki iliyopita, Waziri Mkuu Majaliwa aliwasimamisha kazi viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Songea (Sonamcu) kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za wakulima wa tumbaku na kusababisha kiwanda cha kusindika zao hilo kusitisha uzalishaji.

Majaliwa pia alimsimamisha kazi Meneja Shughuli wa Kiwanda cha Kusindika Tumbaku (Sontop), mkoani Ruvuma, Paul Balegwa akidaiwa kushiriki kufanya ubadhirifu wa fedha za wakulima akishirikiana na mhasibu wake, Nurdin Ponela, ambaye inadaiwa amekimbilia kusikojulikana.

Mkoani Iringa, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba ameamuru viongozi tisa wa vyama vya ushirika Mfyome, Magubike, Kiwemu, Kitai, Mhanga na Kampuni ya Umoja wa Wakulima wa Tumbaku Iringa (ITCOJE Ltd), wakabidhi ofisi zao kutokana na tuhuma za kutapeli trekta zilizokopeshwa kwa vyama hivyo pia amemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Audax Lutabazibwa kuvunja Bodi ya ITCOJE.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliyetembelea Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), alisema ubadhirifu unaotokea hapo, uchunguzi wa Takukuru umeshaanza na kusisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahalifu wote bila kujali wanatoka upande gani wa nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako naye ametumbua jipu kwa kutoa siku saba kwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limpe sababu za kubadili mfumo wa kutunuku viwango vya ufaulu wa awali (Division) na kwenda wa wastani wa pointi (GPA) unaotumika sasa kidato cha nne na sita. Mfumo wa GPA ulianza kutumika kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa mwaka 2014 ambao matokeo yao yalitoka mwaka jana.

Ndalichako aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa baraza hilo kwa miaka tisa, alitoa maagizo hayo wiki iliyopita.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amemuagiza mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala, Dennis Mrema kuanzia Januari 7, 2016 kwa kosa la kusababisha upotevu wa mapato ya serikali kutokana na urasimu wa kukusudia, mazingira ya rushwa na uzembe katika utoaji leseni za biashara.

Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amefanya ziara ya kushtukiza katika Manispaa ya Morogoro na kutoa siku saba kwa halmashauri hiyo kuhakikisha imetenga maeneo yatakayotumiwa na vijana kuendesha shughuli za kiuchumi na uwekezaji.

Waziri wa afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amefanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo na kukuta madaktari walioajiriwa kutokuwepo na kukutana na madaktari wanafunzi huku wale waliojiriwa waliokuwa zamu wakiwa hawakujulikana walikokuwa.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk.Marcel Clemence alisema madaktari hao wamefanya makosa hivyo lazima watawajibishwa.

Leave A Reply