The House of Favourite Newspapers

Mazembe Watua Mbeya, Simba Washtukia

Wachezaji wa Simba SC.

SIMBA wana zali sana. Mvua kubwa iliyonye­sha jana Jumatano mjini hapa iliwapa bahati ya aina yake na kuwaumbua wapinzani wao TP Mazembe ambao walitua Mbeya.

 

Simba ilikuwa icheze na JKT Tanzania jana mjini hapa kwenye kiporo cha Ligi Kuu Bara ambacho kingewafanya wapunguze gepu lao na Azam na Yanga.


Mechi hiyo iliahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia majira ya saa nane mpaka saa 10 kasoro. Kabla ya mvua hiyo maeneo ya pembeni ya mji yalikuwa na manyunyu kwa mbali lakini ghafla hali ikabadilika wakati ambapo mashabiki wengine walishaingia uwanjani ingawa siyo wengi.

 

Waamuzi waliingia uwanjani na kuangalia hali halisi wakajiridhisha kwamba kikanuni mpira hauwezi kuchezwa lakini wakarudi vyumbani na kujadiliana na viongozi wa pande zote mbili na kurudi tena kwenye nyasi kuhakiki.

 

Kila wakidunda mipira ilikuwa inagoma ndipo walipokubaliana kuahirisha mechi wachezaji wakarudi kwenye mabasi yao na kurudi kambini huku mashabiki wakipiga kelele kwamba wanataka viingilio vyao.

 

Lakini Mazembe ambao wanacheza na Simba Jumamosi kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Taifa, jana waliumbuka kutokana na hali hiyo.

Jopo la Mazembe chini ya Mkurugenzi wao wa Michezo, Fredrick Kitenge imeelezwa kuwa wapo Dar es Salaam kwa karibu wiki sasa na jana walikuwa wamekaa mkao wa kula.

 

Baadhi yao walionekana Morogoro, walipokuwa wamekuja kuangalia baadhi ya mambo kwenye mechi ya Simba lakini wengine walibaki Dar es Salaam ili timu ikiwasili waangalie mchezo huo ukiwa umerekodiwa kupitia televisheni wakiwa hotelini.

 

WATUA MBEYA

Kabla ya kutua Dar majira ya saa 1 usiku kikosi hicho kilitua Mbeya na kujaza mafuta kwa nusu saa baadaye ndiyo wakaja Dar.

 

Lakini kumbe Simba walikuwa wameshajua kwamba lazima Mazembe watafanya hivyo na kuweka watu wao kwenye Uwanja wa ndege wa Mbeya kujua nini kinaendelea ambapo walikaa kwa dakika kadhaa . Walipotua Dar straika wao, Tresor Mputu akaliambia Spoti Xtra kwamba ; “Tunajua ugumu wa Simba Dar na tumejiandaa.”

 

Mbinu nyingine za Mazembe zikavurugwa na mechi kuahirishwa na kujikuta wakihaha bila kujua cha kufanya huku Yanga nao waking’aka ndani ya Uwanja huo wa Jamhuri pamoja na kwenye mitandao ya kijamii wakidai kuwa Simba inabebwa makusudi.

Licha ya kuonekana dhahiri kwamba uwanja uko chepechepe lakini Yanga waliokuwa ndani na nje ya Jamhuri walikuwa wanadai kwamba kuna mbinu za kuizidishia Simba viporo ili wabebe ubingwa kiulaini.

 

Yanga inacheza na Ndanda leo Alhamisi mjini Mtwara jambo ambalo linamaanisha kwamba Simba itakuwa na viporo saba pamoja na cha jana jioni ambacho Kocha Patrick Aussems alikifurahia.

 

Aussems alisema; “Kuahirishwa huu mchezo ni nzuri kwetu kwa vile itatupa muda wa kupumzika na kujipanga na mechi ngumu ya Jumamosi, tulistahili kupumzishwa.”

 

Charles Mwakambaya ambaye ni msimamizi wa mchezo alisema wameuahirisha mpaka utakapopangiwa tena.

Comments are closed.