The House of Favourite Newspapers

MAZITO YAFUMUKAA JALI ZA VIONGOZI

SIKU chache baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla kuje­ruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Mdori mkoani Manyara, wingu zito la ajali za viongozi limetanda, Uwazi linachimba kwa undani.

Uchunguzi unaonesha kuwa magari yanayoteketeza roho za vigogo wengi serikalini na kuwaje­ruhi baadhi kutokana na misafara yao kupata ajali, mengi ni aina ya Toyota Land Cruicer yanayotajwa kuwa ni magari ya kifahari yenye uimara wa kutosha.

Hoja ya kipi kinachosababisha misafara mingi kupata ajali na kui­sababishia Serikali hasara ya fedha na rasilimali watu imechipuka upyaa baada ya tukio la Waziri Kig­wangalla kuzua mshtuko uliosaba­bisha mijadala mingi mitaani na kwenye mitandao ya kijamii.

Mapema baada ya ajali ya waziri huyo iliyosababisha kifo cha mwandishi wa habari Hamza Temba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ‘Ninja’ alikuwa mbogo na kuagiza viongozi na ma­dereva wao wanaokiuka sheria za usalama barabarani wachukuliwe hatua kali.

GUMZO LAIBUKA

Kufuatia kauli hiyo, gumzo kubwa liliibuka mitaani na mitandaoni ambapo wengi walita­ka Serikali ije na majibu ya yatakay­owahakikishia viongozi usalama wao wawapo barabarani. “Tuna ajali nyingi sana, viongozi wanakufa, taifa linapata hasara ya kupoteza nguvu kazi, kuwauguza majeruhi na kuyatengeneza magari yanayopata ajali, ishu hii ni nyeti sana.

“Kuijadili kama kitu kidogo ni makosa makubwa, leo hii waziri mchapakazi yuko kitandani, maju­kumu yake yamesimama, hali hii ikiachwa bila tiba inaota mizizi,” mtu mmoja (jina linahifadhiwa) aliandika maneno haya kwenye ukurasa wake wa Instagram.   MADEREVA WACHAMBULIWA

Huku orodha ya viongozi walipata ajali na kupoteza maisha ikiwekwa kuchombeza mijadala, uwezo wa madereva wanaow­aendesha viongozi nao ukahojiwa. “Tunazungumzia mwendo kasi na wakati mwingine tunafika hadi kwenye ushirikina mawazo ya mwaka 47, lakini je tumeshajiuliza hawa madereva wanaopewa kazi za kuwaendesha viongozi wana uwezo wa kumudu kazi zao?

“Wana uzoefu, elimu wanayo au wanaajiriwa kwa kupewa kazi kama asante maadamu wanajulikana na wakubwa?” alihoji kijana mmoja aliyefika ofisi za Uwazi kwa lengo la kujionea uzalishaji wa magazeti  na kukutana na hoja ya ajali ya Waziri Kigwangalla ikijadiliwa na baadhi ya wahariri na yeye kupata nafasi ya kutoa mawazo yake.

LUGOLA AUNGWA MKONO

Agizo la kuwataka Polisi kuwa­chukulia hatua madereva na viongozi wanaowaendesha lililotolewa na Waziri Lugola lilionekana kuungwa mkono na wengi huku hoja ya kupiti­wa kwa leseni za madereza na uwezo wao ikikaziwa zaidi. “Tunaona, kuna vijana wadogo wanawaendesha viongozi, hata kama hoja si kuwabeza kuwa hawawezi lakini ukiwauliza ujuzi wao, uzoefu wa kazi mpaka kufikia hatua ya kum­wendesha waziri au mbunge kuna vitu unaweza ukakwazika navyo.

“Huwezi kuupata uzoefu wa gari huku unamwendesha mkuu wa mkoa, hili siyo sawa, tufike mahali thamani ya viongozi na uhai wao ulindwe kwa nguvu na uwezo wa kila mwananchi, tusiache vitu nyeti viende ovyoovyo,” alisema Joel John mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alipozungumza na Uwazi kuhusu ajali za viongozi.

GHARAMA ZA KUTUMIA V8 YAIBUKA

Kutokana na hoja za wengi kutetea matumizi ya magari haya ya kifahari yanayokadiriwa kuuzwa kwa karibu shilingi milioni 200 na kutumia mafuta mengi na hivyo kuisababishia Serikali kuwa na matumizi makubwa katika kuyaendesha, mchangiaji mmoja mtandaoni aliandika: “Mlisema ni mazuri, imara na ni mara chache kupata ajali, sasa mbona mambo ni mabaya tu, kama tumeshindwa turudi kwenye matumizi ya Land Lover 109 zilikuwa hazituui namna hii.”

Mara baada ya kuandika hivyo majibizano yalikolea kati ya watu waliokuwa wakichangia posti hiyo ambapo mmoja alidiriki kuandika: “Tukishindwa kutumia akili zetu kuna siku tutataka viongozi wetu wa mabasi ya enzi za Nyerere, dunia ina­badilika nasi tubadilike hizi changa­moto za ajali zinatiba yake.”

Ikumbukwe kwamba mara kadhaa baadhi ya wabunge hasa wa upinza­nia wamekuwa wakiishauri Serikali ia­chane na matumizi ya magari haya ya kifahari ili kubana matumizi jambo am­balo limekuwa likipingwa na watetea hoja kuwa magari hayo ni muhimu kwa viongozi kwa maana mbili moja ni hadhi yake na pili ni imara.

AJALI ZILIZOTAJWA SANA

Wakati wa mijadala ajali iliyoongoza kwa kuwa na wachangiaji wengi mitandaoni ni iliyochukua uhai wa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Regia Mtema, alifariki Januari 14 2011, ambapo inaelezwa kuwa alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Land Cruiser VX Limited (V8) lenye namba za Usajili T296 BSM, kinyume na sheria inayomtaka mbunge kuendeshwa na dereva.

Wengine waliotajwa kwa kusiki­tikiwa kuwa walipoteza maisha yao kwenye ajali ni pamoja na Salome Mbatia (Naibu Waziri wa Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto), Clara Mwatu­ka (Mbunge wa Viti Maalum Cuf), Mkurugenzi wa Wilaya ya Kongwa, Izengo Ngusa, Chacha Wangwe (Mbunge wa Tarime).

Ajali nyingine iliyosikitisha wengi ni ile iliyotwaa roho za wafanyakazi wa kituo cha uwekezaji ‘TIC’ ambao ni Said Amir Moshi, Zacharia Kingu na Martin Masalu. Matukio ya viongozi kupata ajali yamekuwa yakileta mshtuko mkubwa kwa jamii na kufanya uwe mjadala mkubwa kwenye mitaa huku watu wasiokuwa na maadili wamekuwa wakitumia ajali hizo kuzusha taarifa za kuwepo kwa vifo wakati si kweli.

Mfano wa matukio haya ya ajali ni hiyo ya Waziri Dk. Kigwangalla na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbunge wa Mbeya Mjini) aliyepata ajali hivi karibuni eneo la Kitonga mkoani Iringa ambapo uvumi wa awali uli­eleza kuwa viongozi hao wamefariki, jambo ambalo lilizua simazi kwa tukio lisilokuwa la kweli.

Wakati huo huo dereva wa Dk. Kig­wangalla, Juma Saleh jana ameach­iwa kwa dhamana mjini Arusha na ametakiwa kuripoti polisi mpaka hapo uchunguzi wa ajali hiyo utakapoka­milika.

 Stori: MWANDISHI WETU, Dar

Comments are closed.