The House of Favourite Newspapers

Mbadala wa Mkude Apata Majanga Simba

0

IMEFAHAMIKA kuwa kiungo mkabaji wa Simba raia wa Uganda, Taddeo Lwanga, hataonekana uwanjani akivalia jezi nyekundu na nyeupe kutokana na kukabiliwa na majeraha ya enka aliyoyapata katika timu hiyo.

 

Mganda huyo alisajiliwa na timu hiyo hivi karibuni katika dirisha dogo la usajili litakalofungwa Januari 16, mwaka huu kwa lengo la kumpa changamoto Jonas Mkude ambaye hivi karibuni alisimamishwa uongozi wa Simba kwa utovu wa nidhamu.

Kiungo huyo aliukosa mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC na ule wa Kombe la FA waliocheza dhidi ya Majimaji FC ya Songea.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kiungo huyo amekosa michezo hiyo kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa katika mazoezi ya timu hiyo wanayofanya Uwanja wa Simba Mo Arena, uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Benchi la Ufundi na viongozi wa timu hiyo wanafanya siri kuumia kwa kiungo huyo kwa hofu ya kubezwa baada ya kumfanyia usajili bila ya vipimo.

 

“Usiri mkubwa umefanywa na benchi la ufundi na viongozi juu ya majeraha ya Lwanga ambayo aliyapata akiwa mazoezini tukijiandaa na michezo ya ligi na FA.“

 

Mengi yalizungumzwa kuhusiana na kutoonekana kwake katika mechi ikiwemo kukosa kibali cha kucheza ligi na mashindano mengine, hivyo hivi sasa anaendelea vizuri tofauti na awali.

 

“Leo (jana), alitakiwa kurudi hospitali kwa ajili ya kufanya vipimo kuona maendeleo yake na majibu yatakayotoka ndiyo yatampa mwongozo wa lini atarejea uwanjani, kama atakuwa sawa huenda akawepo sehemu ya kikosi kitakachocheza dhidi ya Platinum lakini ni asilimia chache sana,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Dk Arnold Kashembe kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Suala hilo lipo katika benchi la ufundi na siyo uongozi.”Imeelezwa kuwa, kiungo huyo alikuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita bila ya kucheza soka baada ya kukosa timu kabla ya kutua Simba, awali alikuwa timu ya Tanta Sport Club ya Misri.

NA WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

 

Leave A Reply