The House of Favourite Newspapers

Mbeya City Kuifunga Yanga Kengele Leo?

0

LEO Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam nyasi zitawaka moto pale vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga watakapoikaribisha Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili msimu huu ambapo Mbeya City nao wamekuwa wamoto wakikamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo huku wakiwa na rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga mabingwa watetezi Simba msimu huu.

Championi Jumamosi, linakuletea dondoo muhimu kuelekea mchezo huu unaosubiriwa kwa hamu kama ifuatavyo;

HUKU MAYELE KULE NG’ONDYA

Wakati Yanga na Mbeya City zinakutana katika vita ya kusaka pointi tatu muhimu, kutakuwa na vita nyingine kali ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo vita hii itakuwa kati ya straika wa Yanga, Fiston Mayele dhidi ya winga hatari wa Mbeya City, Richardson Ng’ondya.

Vita hii ni ile ya kusaka ufalme wa takwimu za kuhusika kwenye mabao mengi kwenye vikosi vyao msimu huu. Mpaka sasa kwa upande wa Yanga, Mayele ndiye mchezaji ambaye amehusika kwenye mabao mengi zaidi akifanya hivyo mara nane hii ni baada ya kufunga mabao sita na kuasisti mara mbili.

Kwa upande wa Mbeya City, Ng’ondya ndiye nyota ambaye amehusika kwenye mabao mengi zaidi akifanya hivyo mara sita kwa kufunga mabao manne na kuasisti mabao mawili, hivyo leo nyota hao wawili wana nafasi uya kuongeza takwimu zao.

TAKWIMU ZAO MSIMU HUU

Msimu huu mpaka sasa Yanga ndiyo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo wamefanikiwa kukusanya pointi 35 katika michezo 13 waliyocheza mpaka sasa wakiwa ndiyo timu pekee ambayo bado haijapoteza mchezo wowote wakishinda michezo 11 na kutoa sare michezo miwili pekee.

Yanga pia ndiyo timu ambayo imefunga mabao mengi zaidi msimu huu katika michezo 13 waliyocheza ambapo wamefunga mabao 23 na kuruhusu mabao manne pekee, idadi ndogo zaidi kulinganisha na timu yako.

Mbeya City tofauti na msimu uliopita, msimu huu wanaonekana kuanza kwa kasi ambapo wanakamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi zao 22 walizokusanya kwenye michezo 13 waliyocheza, wameshinda michezo mitano, sare saba na kupoteza mchezo mmoja pekee. Mabao ya kufunga ni 17 na mabao yua kufungwa 11.

MARA YA MWISHO WANAKUTANA

Mara ya mwisho timu hizo mbili kukutana ilikuwa katika mchezo wa mzunguko wa pili wa liGI Kuu msimu wa 2020/21 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Katika mchezo huo Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 84 ya mchezo kupitia kwa kiungo Deus Kaseke akimalizia asisti ya kichwa aliyekuwa mshambuliaji wao Mghana, Michael Sarpong.

Bao hilo halikudumu sana kwani Mbeya City walisawazisha dakika ya 90+3 kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na kiungo, Pastory Athanas baada ya beki wa Yanga, Yassin Mustapha kuunawa mpira ndani ya 18.

REKODI ZAO

Yanga na Mbeya City zimefanikiwa kukutana mara 14 ambapo katika michezo hiyo Yanga wamefanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo tisa huku Mbeya City wakishinda mchezo mmoja pekee na michezo minne ikiwa imemalizika kwa matokeo ya sare.

Katika michezo yao mitano mfululizo iliyopita rekodi zinaibeba zaidi Yanga ambao wameshinda michezo miwili na michezo mitatu ikiisha kwa matokeo ya sare. Katika michezo hiyo mitano mabao sita yalifungwa manne ya Yanga huku Mbeya City wao wakifunga mabao mawili pekee.

JE, MBEYA CITY KUMFUNGA YANGA KENGELE?

Swali kubwa ambalo wadau wengi wanatamani kupata majibu yake ni je, Mbeya City wataifunga Yanga kengele? Yaani baada ya timu 13 kushindwa kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Yanga kwenye Ligi Kuu msimu huu Mbeya City watafanikiwa kuvunja rekodi ya Yanga kutopoteza mchezo leo?

Swali hili kwa kiasi kikubwa linachagizwa na uhalisia kuwa Mbeya City hivi karibuni walitoka kuwatoa machozi mashabiki wa Simba kwa kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba wakifanya hivyo Januari 17, mwaka huu. Ni suala la kusubiri na kuona.

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply