The House of Favourite Newspapers

Mbosso Anakimbiza Mwizi Kimya Kimya

0

NI miaka kadhaa sasa tangu mwamba huyu asajiliwe kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), lakini mambo anayoyafanya kimyakimya ni ya kutisha. Mwamba anajua, anajua na anajua tena, kiukweli anayejitahidi na apewe sifa zake.Hapa ninamzungumzia kijana machachari kwenye tasnia ya muziki mtamu wa Bongo Fleva.

 

Jina lake halisi ni Yusuf Mbwana Kilungi ila kwa jina la kutafutia mkate kupitia Bongo Fleva anajulikana kama Mbosso Khan.Kwa sasa Mbosso anatamba na album yake ya Deffinition of Love yenye nyimbo kali 12 za Baikoko, Your Love, Yalah, Mtaalam, Kiss Me, Yes na nyingine kibao.

 

Album hiyo kwa sasa ina jumla ya streams (kusikilizwa na kutazamwa) zaidi ya milioni 100 kwenye mitandao yote na ndiyo albam namba moja kwa mwaka 2021.

IJUMAA limezungumza na Mbosso katika mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo anafunguka mambo mengi ikiwemo kushika nafasi za juu kwa kusikilizwa duniani;

IJUMAA: Habari za muda mwingine tena Mbosso?

MBOSSO: Kheri kabisa Mungu anasaidia uzima upo.

IJUMAA: Hongera sana tunaona umekuwa balozi wa kapuni ya simu.

MBOSSO: Ahsante sana na nashukuru kwa hilo pia naushukuru uongozi kwa kuniamini na kuona kwamba mimi naweza kuwa balozi wao.

IJUMAA: Umejisikaje baada ya kutafutwa na kupewa dili hilo la ubalozi wa simu?

MBOSSO: Nimejisikia faraja sana kwa kuona kwamba kampuni kubwa kama ile imeniamini na kutaka kufanya
kazi nao.

IJUMAA: Na wamekupa mkataba wa muda gani?

MBOSSO: Kiukweli ni muda mwingi sana.

IJUMAA: Unaweza kutuambia ni wa muda gani maana mashabiki wako wanapenda kufahamu juu ya hilo?

MBOSSO: Hayo ni mambo private (binafsi) kati yangu mimi na kampuni.

IJUMAA: Haya bwana Mungu azidi kukupa madili mengi zaidi ya hayo..

MBOSSO: Ameen sana nashukuru sana.

IJUMAA: Kwenye Mtandao wa Boomplay pekee umekuwa na streams zaidi ya milioni 40, hongera sana, labda unazungumziaje juu ya hilo?

MBOSSO: Kwanza nawashukuru sana mashabiki wangu kwa sapoti yao nzuri kwangu, maana idadi hiyo imenifanya kuwa msanii wa pili mwenye idadi kubwa ya streams kwenye ukanda
wetu huu wa Afrika Mashariki,
lakini hakuna mtu anajua kwa sababu mimi siyo mtu wa kuongea sana, labda kutokana na asili yangu.

IJUMAA: Kwa Dunia nzima umeshika namba ngapi kwani mashabiki wanatamani kufahamu?

MBOSSO: Nimeweza kukamata nafasi ya 15 kwa wasanii wote duniani, siyo jambo dogo kwa kweli, ni jambo kubwa sana kwangu.

IJUMAA: Hongera sana. MBOSSO: Ahsante.

IJUMAA: Tukirudi pia kwenye album yako, tumeona imeweza kufikisha stream milioni 100 kwenye miandao mbalimbali, unazungumziaje mafanikio hayo makubwa?

MBOSSO: Ndiyo ni kweli imeweza kufikisha idadi hiyo, ni mafanikio makubwa sana na hiyo yote ni pesa.

IJUMAA: Diamond alikomenti kwa kusema kwamba wanasubiri siku ya uzinduzi wa album yako ya
Definition of Love kwa hamu
kubwa mno, mbona kimya?

MBOSSO: Ndiyo na mimi nataka kumwambia asijali, mambo yote yatakuwa poa.

IJUMAA: Mbona albam ina muda sasa tangu imetoka na hujafanya uzinduzi?

MBOSSO: Nimependa kufanya hivyo.

IJUMAA: Nina imani siku ya uzinduzi watu wazito watakuwa ndani ya nyumba…

MBOSSO: Ndiyo tena sana tu, mashabiki wangu wakae mkao wa kula maana mambo ni mengi sana, suprise zitakuwa kama zote.

IJUMAA: Na wasanii wa nje watakuwepo?

MBOSSO: Ndiyo maana nikasema suprise zitakuwa za kutosha siku hiyo, lakini kubwa ni watu waendelee kusikiliza na kutazama muziki wangu kwenye mitandao yote.

IJUMAA: Ahsante sana Mbosso.

MBOSSO: Asante na karibu tena na tena.

Leave A Reply