The House of Favourite Newspapers

MBOWE AZIDIWA, AKIMBIZWA SAUZI KUTIBIWA

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe ni mgonjwa mahututi na leo amesafirishwa kwa dharura kwenda nchini Afrika Kusini (Sauzi) kwa ajili ya matibabu kutokana na ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu vinavyomsumbua.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Novemba 1, 2018 na mdhamini wa Mbowe, Grayson Celestine, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wakili wake aliyesema amepewa taarifa za ugonjwa wa Mbowe na mke wa mwanasiasa huyo.

Kufuatia maelezo hayo, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi,  ameiomba mahakama mbele ya Wilbard Mashauri  kutoa amri ya kumkamata Mbowe ili ajieleze kwa nini dhamana aliyopewa na mahakama isifutwe kwa kushindwa kufika mahakamani huku akidai anachokifanya ni visingizio.

Wakili anayemwakilishi Mbowe, Peter Kibatala,  alianza kwa kuiarifu mahakama kuwa mdhamini wa mwanasiasa huyo yupo mahakamani hapo.

“Kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, Mbowe anasumbuliwa na moyo na presha (shinikizo la damu) na familia imemsafirisha kwa dharura lakini mimi sijaonana naye,” amesema Celestine na kuongeza kuwa mshtakiwa akirejea atawasilisha nyaraka za safari na matibabu na kwamba anaendelea kufanya mawasiliano ili azitume nyaraka kwa njia ya mtandao.

Naye Nchimbi alisema waliomsindikiza walipaswa kumdhamini na kwamba upande wa mashtaka wanaona ni mwendelezo wa dharau ya mshtakiwa huyo kwa mahakama na kwa kuwa alishapewa onyo, ameamua kwa utashi wake kukiuka amri ya mahakama.

Kwa upande wake, hakimu Mashauri amesema endapo mshtakiwa hatopeleka kielelezo atatoa amri ya kumkamata ili ajieleze kwa nini asifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa mahakamani hapo.

Comments are closed.