The House of Favourite Newspapers

Mdee, Bulaya, Jacob Watuhumiwa kwa Makosa 7

0

VIONGOZI na wafuasi 27 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiwemo wabunge  watatu:  Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Jesca Kishoa (Viti Maalumu), Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na Patrick Assenga, Diwani wa Tabata, wamepandishwa kizimbani wakituhumiwa kutenda makosa saba, ikiwamo kuharibu lango la Gereza la Segerea na kumchania shati askari Magereza, kufanya mkusanyiko na kutotii amri halali katika geti la gereza la Segerea.

Watuhumiwa hao wamepandishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, leo tarehe 23 Machi 2020, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, ambapo washtakiwa 15 kati ya 27, wamesomewa mashtaka yao.  Shtaka la kwanza limesomwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude, ambalo ni kutotii amri halali.

Washtakiwa wote wamedaiwa tarehe 13 Machi 2020 , eneo la gereza la Segerea, Ilala jijini Dar es Salaam kwa makusudi, waligomea amri halali iliyotolewa na askari  namba P3648, Sajenti John ambaye ni mlinzi wa geti la gereza hilo. Shtaka la pili limesomwa na Wakili wa Serikali, Mkunde Mshana,  ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali linalowakabili watuhumiwa wote ambapo  inadaiwa tarehe 13 Machi, 2020, walikusanyika kwenye geti la gereza la Segerea visivyo halali na kusababisha hali isiyo ya kawaida iliyosababisha hofu.

Shtaka la tatu  linadai kuwa, tarehe 13 Machi 2020, watuhumiwa walifanya uharibifu kwenye geti la gereza la Segerea ambalo ni mali ya Serikali ya Jamhuri.   Mashitaka ya nne,  tano na  sita yamesomwa  na Wakili wa Serikali, Ester Martin dhidi ya Mdee, Bulaya na Jacob kwa kutoa matusi na lugha ya kuudhi  tarehe 13 Machi 2020,  kwa nia ya kuwadhalilisha askari wa Magereza waliokuwa eneo hilo.

Shtaka la saba linamkabili Jacob aliyedaiwa siku hiyo ya Machi 13, 2020, kumshambulia  Sajenti John, na  kumchania shati lake akiwa anatekeleza majukumu ya ulinzi kwenye geti la ngome ya Segere.

Washtakiwa wamekana mashtaka hayo na upande wa serikali umedai umekamilisha upelelezi na wameiomba mahakama kupanga terehe ya usikilizwaji wa awali. Washtakiwa wamedhaminiwa kwa mdhamini mmoja kila mmoja aliyesaini bondi ya shilingi milioni nne.

Kesi imeahirishwa hadi tarehe 23 Aprili 2020.

 

Leave A Reply