The House of Favourite Newspapers

MDEE, BULAYA KUSHTAKIWA Kwa Kuvamia GEREZA -Video

0

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa upelelezi dhidi ya wafuasi 27 wa Chadema wakiwemo viongozi wawili ambao ni mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda mjini, Ester Bulaya wanaodaiwa kufanya fujo kutaka kuingia katika gereza  la mahabusu la Segerea umekamilika na jalada litatua kesho Jumatatu kwa mwanasheria wa Serikali.

 

Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es salaam, SACP Lazaro B. Mambosasa leo Machi 15, 2020 amezungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam na amesema Machi 13, 2020 mchana jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa maofisa wa gereza hilo kuwa kuna kundi la wafuasi wa Chadema limekusanyika katika geti la kuingilia gerezani hapo huku likiandamana na kufanya fujo.


Amesema wafuasi hao walifanya vurugu hizo walipokuwa wakienda kumtoa mwenyekiti wao Freeman Mbowe ambapo walikwenda kufanya vurugu kutaka kumtoa kabla ya kukamilisha taratibu.


“Tulifika eneo la tukio na kukuta askari wa magereza wakiendelea kuwadhibiti wanachama hao ndipo polisi walipowakamata watuhumiwa 27 na kuwapeleka katika kituo cha polisi Stakishari kwa mahojiano,” amesema.

“Baada ya mahojiano watuhumiwa wote 27 walidhaminiwa kwa mujibu wa sheria na watafikishwa mahakamani hivi karibuni kwani upelelezi wa shauri hili umeshakamilika,” ameongeza.

 

 

Leave A Reply