Mfu Aliyerudiwa na Uhai-4

ILIPOISHIA WIKIENDA

Huyo mtu atakuoa wakati huu unasoma au…”

“Anasubiri nimalize masomo.”

“Lini?”

“Hapo nitakapomaliza.”

“Kwa hiyo ukienda kidato cha tano na cha sita atakusubiri tu?”

SASA ENDELEA…

WAO wana imani kuwa mwisho wangu ni kidato cha nne.”

“Kwa hiyo ukifaulu huendelei na masomo?”

“Nani? Nitaendelea na masomo. Anayetaka kunisubiri atasubiri akikata tamaa shauri yake.”

“Mara nyingi uchumba wa hivyo si mzuri. Lolote linaweza kutokea hapo katikati.”

“Na litokee tu, unioe wewe mpenzi wangu.”

“Siwezi kushindana na huyo mzee. Labda ashindwe mwenyewe.”

Siku zote ninapokwenda kwa Macheo ninashinda kutwa nzima, siku ile niliondoka mapema kwa sababu ya Alhakim.

Nilimwambia macheo asinisindikize kwa kuhofia tungeweza kukutana na Alhakim akiendelea kuranda na mitaa kunisaka. Yule baba ana wivu si mchezo!

Nilitembea huku nikiangaza kila upande hadi nikafika kwenye kituo cha daladala nikasubiri. Daladala ilipofika nikaondoka.

Nikiwa ndani ya daladala nilikuwa nikimuwaza Alhakim, mtu ambaye alikuwa katika safari ya kuwa mume wangu. Tukiwa katika uchumba tu alikuwa tayari kupoteza muda wake kunichunguza mimi, atakaponioa itakuwa vipi? Nikawaza.

Kwa kweli alishaanza kunitia hofu. Nilichogundua ni kuwa Alhakim alikuwa na wivu mkali au niseme wivu uliopitiliza.

Niliwaza kwamba nitakapokuwa mke wake sitaruhusiwa kutoka nyumbani peke yangu. Na kama nitalazimika kutoka peke yangu ni lazima atakuwa akinifuata nyumanyuma ili kuona kama nilikuwa ninakwenda safari niliyomuaga au ninakwenda safari nyingine.

Hayo hayakuwa maisha yaliyokuwa akilini mwangu, maisha ya kufuatana na mume kila mahali. Nitakuwa kama mtumwa wake nisiye na uhuru wa kuamua pa kwenda.

Kibaya zaidi ni kuwa Alhakim huyohuyo ndiyo amekuwa tegemeo kwetu. Wazazi wangu wanaona akinioa yeye ndiyo watakwamuka kiuchumi, ndiyo tutapata maendeleo, ndiyo maisha yangu na yao yatakuwa mazuri. Sikuwa na shaka yoyote kwamba hayo masuala ya wivu wake hayakuwa na uzito kwao.

Wakati nafika nyumbani nikaliona gari la Alhakim lipo barazani. Nikashituka sana. Miguu ilinitepeta kwa hofu. Nusura ningeanguka chini.

Niliwaza Alhakim amefuata nini nyumbani kwetu baada ya kunikosa kule alikokuwa akinifuata? Amefika kwetu kunishitakia au kunisubiri aniulize ni kwa nini nilimchenga?

Makubwa! Badala ya kuingia nyumbani kwa kutumia mlango wa mbele, nilitumia mlango wa nyuma ambao Alhakim alikuwa hautumii.

Uani sikukuta mtu, nikaingia ukumbini ambako pia sikukuta mtu lakini nilisikia sauti ya baba akiongea sebuleni. Nikaingia chumbani kwangu kimyakimya.

Nilibana mlango kisha nikalala kitandani na kuendelea kuwaza.

Mara nikaisikia sauti ya mama ukumbini.

“Sikumbuki kama yumo au hayumo kwa sababu aliniambia anakwenda kwa mama yake mdogo anaumwa,” nikamsikia mama anasema uongo kunitetea.

Hapohapo mlango wa chumbani kwangu ukasukumwa nikafumba macho yangu kama vile nilikuwa nimelala.

Nikamsikia mama akiniita. “Esma…!”

Nikafumbua macho yangu na kumuitikia.

“Abee…!”

“Umelala muda huu?”

“Kichwa kinaniuma.”

“Basi lala kama kichwa kinakuuma. Alhakim alikuwa anakuulizia.”

Mama akafunga mlango. Nikamsikia akisema huku akitembea ukumbini.

“Kumbe amelala…kichwa kinamuuma.”

Baada ya hapo sikuisikia tena sauti yake.

Sikuweza kufahamu Alhakim alipoambiwa nipo alisema nini wakati aliniona kule Tabata.

Niliendelea kubaki chumbani mpaka nilipolisikia gari la Alhakim limewashwa, ndipo nikatoka chumbani.

Nilikwenda uani nikamkuta mama akifua nguo.

Kwanza nilikwenda msalani, nilipotoka nikachukua mbuzi ya kukunia nazi na kwenda kukaa karibu yake.

“Kichwa kimetulia?” akaniuliza akiamini kuwa kweli kichwa kilikuwa kinaniuma.

“Kimetulia.”

“Ulikuwa umekwenda wapi na ulirudi saa ngapi?”

Kwa kudhani kwamba huenda Alhakim aliwaambia kuwa aliniona Tabata, nikaona niseme ukweli kuwa nilikwenda huko.

“Nilikwenda Tabata kuchukua kitabu changu.”

“Kitabu cha nini?”

“Kitabu cha shule, nilimuazima mwanafunzi mwenzangu na kesho kinatakiwa shule.”

“Mbona hukuaga kama unakwenda Tabata?”

“Nilipoondoka hapa nyumbani sikuwa na wazo la kwenda huko. Nilikwenda mtaa wa pili kwa rafiki yangu. Sasa nikiwa huko ndiko nikapata wazo la kwenda Tabata.”

“Unazunguka sana mwanangu wakati umeshakuwa mchumba wa mtu.”

“Hata kitabu changu nisikifuate kwa sababu nimekuwa mchumba wa mtu?”

“Unadhani mwenyewe akikuona atafikiri nini?”

“Kwani amesema ameniona?”

“Hakusema hivyo lakini nakuuliza mimi kama akikuona atafikiri nini?”

“Afikiri nini, kwani ameshanioa?”

“Hata kama, inakupasa uweke heshima na heshima ya mwanamke ni kutulia nyumbani kwao.”

“Sasa subiri nikwambie kitu mama. Huyu mzee ana tabia ya kunifuatafuata anaponiona.”

“Alikufuata wapi?”

“Ni mara nyingi. Ninaweza kuwa natembea nikashitukia ananifuata na gari lake. Hii leo pia alinifuata hadi Tabata nikamchenga.”

“Unasema kweli?”

“Nasema kweli. Ana tabia ya kunifuatafuata.”

“Si nimekwambia acha tabia ya kuzururazurura. Anaweza kukuona. Sasa kama hivyo unavyosema amekufuata hadi Tabata na ndiyo maana alifika hapa na kukuulizia.”

“Lakini hakusema kama aliniona?”

“Hakusema, labda alitaka tu kufahamu kama umesharudi.”

“Sasa maisha haya ya kufuatana hadi lini?”

“Yule ni mwanaume lazima akufuatefuate, afahamu nyendo zako.”

“Sasa hapo atakaponiona si itakuwa shida.”

“Hakuna shida yoyote. Hakuna mwanaume atakayekupa uhuru unaoutaka wewe.”

“Mmh….!”

Nilipoona mama hakubaliani na mimi nikainuka na kumuacha aendelee kufua nikarudi chumbani kwangu.

Siku iliyofuata nilikwenda shule. Wakati ninatoka shule nilikuwa na wenzangu tumefuatana tukizungumza.

Ghafla nikaliona gari la Alhakim. Lilikuwa limeegeshwa mbali kidogo na geti la shule.

Upande lilipoegeshwa ulikuwa tofauti na barabara tunayotumia tukitoka shule. Sisi tulipita barabara nyingine tukaendelea na safari yetu ingawa nilifahamu kuwa Alhakim alifika pale kunitega mimi.

Niliwahi kukariri maelezo ya mtaalamu wa saikolojia aliyesema kwamba baadhi ya akili za watu wenye umri kuanzia miaka sitini na kuendelea hupungua na kutazama suala hilohilo kila wakati na kila siku. Alitoa maelezo mengi lakini mimi nilishika hayo.

Niliamini Alhakim alikuwa miongoni mwa watu hao wanaotazama suala hilohilo kila wakati na kila siku. Kunifuatilia mimi ilikuwa ni agenda yake kuu. Hakuwa na lingine.

Sikumlaumu kwa sababu yalikuwa ni maumbile. Kila binadamu ana tabia yake tofauti na mwenzake na kila rika lina tabia zake tofauti na rika lingine. Kama nitakuwa na kazi ya kulaumu watu kutokana na tabia walizonazo, mimi pia ningelaumiwa kwani kwa vyovyote vile siamini kwamba vitendo vyangu vyote vinawapendeza wenzangu.

Niliendelea kutembea na wenzangu huku tukizungumza hili na lile. Kwa vile tulikuwa kundi kubwa tukaanza kupungua. Wengine walishika barabara nyingine inayoelekea kwao.

Baadaye nikabaki peke yangu. Ili uone kama yule mzee ananifuatilia, nililiona gari lake mbele yangu. Hapo sikuwa na mbinu ya kulikwepa.

Nikaenda kwenye mlango wa dereva. Alhakim alikuwa ametoa kichwa. Sikutaka kusubiri aniite, kwa vile nilishamuona ikabidi nimfuate.

“Shikamoo,” nikamwamkia.

“Marahaba. Ingia garini twende,” akaniambia.

Nikazunguka upande wa pili wa gari nikafungua mlango na kuingia

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.v


Loading...

Toa comment