The House of Favourite Newspapers

MGAMBO WAFANYA TUKIO LINGINE

MGAMBO  wanaosimamia operesheni ya usafi Mkoa wa Dar es Salaam  wamefanya tukio lingine baada ya lile la kudaiwa kuwapiga raia, Uwazi linakujuza.  

 

Mgambo hao wanadaiwa kusababisha varangati baada ya kuwahenyesha baadhi ya wazee akiwemo Rashidi Shitondi, mkazi wa Mabibo-Kanuni wilayani Kinondoni.

Katika tukio hilo lililoshuhudiwa na Uwazi lililojiri mwishoni mwa wiki iliyopita maeneo hayo, Mzee Shitondi alijikuta akipata msukosuko kutoka kwa mgambo hao hadi kufikia hatua ya kukosa nguvu na kushindwa kuongea huku wenzake watatu ambao majina yao hayakufahamika nao wakikamatwa.

 

Mzee huyo alikamatwa na Mgambo wa Makonda waliomtaka kulipa kiasi cha shilingi 50,000 kama faini baada ya mazingira ya nyumbani kwake kukutwa ni machafu. Shitondi ambaye alionekana kukosa nguvu baada ya vuta nikuvute kutoka kwa mgambo hao, alijikuta akiishia kubebwa msobemsobe na wenzake hali iliyoibua taharuki kubwa mtaani hapo.

Katika tukio la Mzee Shitondi na wenzake, hali ya sintofahamu ilibuuka katika mtaa huo baada ya mgambo hao kuibuka eneo hilo na kuanza kukamatakamata wazee wasiojiweza kwa madai kuwa mazingira yao ni machafu.

Akizungumza na Uwazi kwa taabu, Mzee Shitondi alisema alishangaa mgambo hao kutumia nguvu ya kumtoa nyumbani kwake hadi ofisi za Serikali za mtaa kwa madai kuwa alikutwa mazingira yake ni machafu na kutakiwa kulipa kiasi cha 50,000 ambazo hakuwa nazo.

“Hao mgambo walipita nyumbani kwangu, walipofika, walisimama na kujitambulisha kuwa ni mgambo wanaosimamia masuala ya usafi wa mazingira ya jiji zima la Dar. “Kwa hiyo wakaniambia mazingira yangu ni machafu hivyo ninatakiwa kulipa shilingi 50,000 wakati huohuo na kama sina, niondoke nao hadi ofisi za Serikali ya mtaa,” alisema mzee huyo na kuongeza:

 

“Nilipinga kwa kuwa niliona nipo katika mazingira masafi, lakini waliamua kutumia nguvu na kunibeba kisha kunibwaga Serikali ya mtaa kama mzigo. “Kama unavyotuona tupo hapa Serikali ya mtaa na hatujui ni nini hatma yetu kwa sababu mimi hata hiyo 50,000 sina.

“Walichokisema mgambo hao ni kwamba kama sitalipa, nitafikishwa katika mahakama ya jiji.” Mzee huyo aliomba kilio chake kimfikie Makonda kuwa wazee wananyanyaswa kwa kukamatwa kwa nguvu na kudaiwa faini ambayo ni vigumu kwao kuwa nayo.

Hata hivyo, Uwazi lilitaka kujua undani wa tukio hilo ambalo lilisababisha wananchi wa mtaa huo kuandamana na kumvamia mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Salehe Lugaila hivyo lilimvaa na kutaka kujua kilichojiri.

Mwenyekiti huyo alianza kwa kusema kuwa; kwenye mtaa wake kuna changamoto ya zoezi la usafi wa mazingira iliyotokana na miundombinu kutokuwa katika hali nzuri. Alisema miundombinu ya mtaa wake ni mibovu, hali inayosababisha mtaa kuonekana ni mchafu hata kama usafi wa nguvu umefanyika.

“Unajua miundombinu ya mazingira ya huku kwetu (Mabibo-Kanuni) siyo mizuri. Ukiangalia sehemu kubwa, hata ukitaka kuchimba kidogo unakutana na maji au takataka hali inayosabisha mtaa kuonekana mchafu.

“Hata mvua ikinyesha kidogo, maji yanakosa mwelekeo hivyo ukizungumzia suala la usafi wa mazingira ni changamoto kubwa sana na ndicho kilichowapata wazee hawa,” alisema mwenyekiti huyo. Akifafanua kuhusiana na kukamatwa kwao, mwenyekiti huyo wa mtaa alisema kuhusu mgambo hao kukamatakamata, wanatakiwa kutumia hekima hasa kwa wazee.

Juni 5, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Makonda alitangaza kuanzisha oparesheni ya usafi katika Jiji la Dar itakayokuwa ikisimamiwa na vijana waliotoka kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wapatao 400 waliopachikwa jina la Mgambo wa Makonda.

Baadaye zoezi hilo lilianza kuingia dosari baada ya vijana hao kudaiwa kutumia nguvu na ubabe katika utekelezaji wake.

STORI: ZAINA MALOGO NA RICHARD BUKOS, UWAZI

Comments are closed.