The House of Favourite Newspapers

Mgawanyo wa mapato ya Muungano upatiwe ufumbuzi

0

shamsi-vuai-nahodha-15Shamsi Vuai Nahodha

Na Elvan Stambuli, UWAZI

Waziri Kiongozi Mstaafu wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambaye pia ni Mbunge wa Kijito Upele,  Shamsi Vuai Nahodha amelitaka Bunge la Muungano kumaliza mara moja matatizo yanayoikumba Zanzibar. Katika mahojiano haya maalum kati ya kiongozi huyo na gazeti hili yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar, Nahodha amezungumzia mengi kama vile uchumi, mambo ya kitaifa na kadhalika. Ungana nasi ufahamu alichokisema:

Mwandishi: Unaweza kueleza historia yako kifupi ili wasomaji wetu waweze kukufahamu vizuri?

Nahodha: Mimi nilizaliwa Novemba 20, 1962 Makunduchi Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja na kupata elimu yangu katika Skuli ya Msingi Kiongoni huko Makunduchi na kuendelea Sekondari katika Skuli ya Ben Bella kisha kufanikiwa kujiunga katika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni. Shahada ya kwanza niliipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya elimu na pia stashahada niliyoipata katika Chuo cha Diplomasia, Dar.

Mwandishi: Kisiasa, umewahi kushika yadhifa gani nchini?

Nahodha: Mwaka 2000 nikiwa na umri wa miaka 38 nilikabidhiwa cheo cha juu katika nchi ya Zanzibar kwa kuteuliwa na rais wa wakati huo Dk. Aman Abeid Karume kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Nilijishangaa kwa kuteuliwa lakini niliyapokea maamuzi ya rais kwa mikono miwili na kuingia kazini katika Ofisi ya Waziri Kiongozi Vuga, Zanzibar.

Kisiasa niliwahi pia kuwa Mwakilishi wa Mananchi (Mbunge) wa Mwera mwaka 2000 hadi 2005 kisha Mwanakwerekwe 2005 hadi 2010. Niliwahi kuingia katika kinyan’ganyiro cha kugombea urais mwaka 2010 ambapo jina langu  lilivuka Ofisi ya CCM, Kisiwandui Zanzibar na kuweza kufika Makao Makuu ya CCM Dodoma lakini kwa bahati mbaya halikurudi.

Kabla ya hapo nilikuwa mwakilishi na mwaka huo niligombea tena uwakilishi na kushinda kwa kishindo. Baadaye nikateuliwa kuwa Mbunge na Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika Serikali ya Muungano kisha nikaingia katika Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupewa wadhifa wa waziri wa mambo ya ndani ya nchi baadaye nikahamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mwandishi: Hivi sasa hakuna siri kwamba kuna mgogoro  unaohusu Muungano wa nchi mbili hizi, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, unashauri nini kuhusu tatizo hili?

Nahodha: Suluhu ya Zanzibar imeshindwa kupatikana kwa misingi ya kisiasa hivyo basi viongozi wa Zanzibar na viongozi wa Jamhuri wa Muungano lazima wafikirie njia nyingine kumaliza tatizo linaloikumba Zanzibar. Uchache wa rasilimali na hali ya uchumi ya Zanzibar unachangia sana hali ya mitafaruku isiyokwisha inayoikumba Zanzibar. Naiomba Serikali ya Tanzania ambayo ina uchumi mkubwa lazima ichukue dhima kusaidia uchumi dhaifu wa  Zanzibar. Suala la mgawanyo wa mapato ya Muungano limezungumziwa kwa muda mrefu bila kupatikana suluhu, basi suala hilo lazima limalizike mara moja kama watu wanaipenda Tanzania na Zanzibar kwani amani ya Tanzania inategemea sana mustakabali wa uchumi wa Zanzibar. Kadiri  tunavyochelewa kulishughulikia suala la mgawo na kuisaidia Zanzibar basi maadui wasioutakia mema Muungano na Tanzania wanaongezeka.

 

ASICHOKISAHAU AKIWA WAZIRI KIONGOZI

Mwandishi: Wewe ni mtu pekee hadi sasa uliyeshika nafasi ya uwaziri kiongozi kwa miaka mingi kuliko watangulizi wako. Kitu gani ambacho huwezi kukisahahu wakati upo katika wadhifa huo?

Nahodha: Kuhusu jambo ambalo sitalisahau ni mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar katika kipindi cha miaka 10 mimi nikiwa waziri kiongozi chini ya Rais Dk. Amani Karume kabla ya kuibuliwa mpango wa kuanzisha mazungumzo ya kusaka upatanishi uliozaa mwelekeo wa kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Wakati mwingi moyo wangu ulikuwa ukisononeka hasa nilipoona vyombo vya dola vinatumia nguvu kupambana na ghasia zilizokuwa zikijitokeza ili kuhakikisha vinaweka mazingira ya utulivu. Matokeo ya vurugu na mapambano ya kutafuta amani ndiyo yaliyonisononesha kwa sababu wengi walioathirika kwa njia moja ama nyingine ni wananchi wa kawaida. Hata hivyo, Rais Karume alikuwa akitumia busara sana kukabiliana na kila hatua hatarishi, moyo wangu haukuwa ukipenda yatokee mazonge na hasama.”

Mwandishi: Nani ambaye unaweza kumsifu kwa wazo la kuanzisha ushirikiano wa kisiasa kati ya Chama Cha Mapinguzi (CCM)  na Chama Cha Wananchi (CUF) Zanzibar?

Nahodha: Namsifu aliyekuwa Rais Dk. Jakaya Kikwete kwa kuibua wazo la kuanzishwa kwa mazungummzo ya kusaka upatanishi wa kisiasa kati ya CCM na CUF, lakini siwezi kumsahau aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Karume kwa kuyasimamia mazungumzo hayo na kuyafanikisha kwa njia za kiungwana.

Wiki ijayo atazungumzia mambo mengi likiwemo suala la Katiba Inayopendekezwa, Usikose nakala ya gazeti hili.

Leave A Reply