Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Shanty Town mjini Moshi, Mghwira alikumbuka karaha aliyoipata baada ya furaha ya kuaminiwa na Rais na kupewa wadhifa huo.Alisema kama si ubabaishaji wa kisiasa Tanzania, asingeondolewa kwenye uenyekiti wa ACT-Wazalendo.
“Changamoto niliyokutana nayo ACT-Wazalendo kama mwenyekiti ni kukosa wigo sahihi wa kisiasa kwa sababu kama tungekuwa tunafanya siasa sahihi, nisingeondolewa uenyekiti,” alisema.
Mghwira alisema, “Naapishwa tu kuwa RC (mkuu wa mkoa) kesho yake naondolewa tena tukiwa tumepanga kukutana kwenye kikao na mpaka leo hatujawahi kukutana.
“Nimesoma kwenye magazeti kuwa mrithi wa Mghwira kutembelea mikoa saba, yaani na mrithi ameshapatikana. Hizo si siasa, huo ni ubabaishaji. Ubabaishaji wa kisiasa Tanzania ni tatizo,” alisema.
Aliongeza, “Sisi kina mama tukisimama imara tunaweza kuondoa dhana hii ya siasa za ubabaishaji. Ni siasa za kipuuzi kabisa. Mmekubaliana mkutane muongee, hamuongei wenzako wanakaa pembeni. Umechaguliwa na mkutano mkuu unaondolewa na kamati ndogo. Watu 370 karibu 400 hivi walikuchagua, siku ya kuondolewa unaondolewa na watu watatu au wawili au mmoja. Hiyo si siasa ni dalili tosha kuwa hakuna siasa.”
Alisema mbaya zaidi ni kuwa watu wanaokuondoa hawakutumwa na mkutano mkuu, wala hawakukaimishwa na kamati kuu.
Hakuna upinzani nchini
Baada ya kujumuisha yote hayo na hasa alivyotimuliwa kwenye uongozi, mkuu huyo wa mkoa akawa na jibu moja kuhusu siasa za upinzani, “Hakuna siasa za upinzani, bali zilizopo ni za kurudishana nyuma maendeleo.
“Siasa ni kitu kizuri kwa maana ya ile mijadala, kubadilishana mawazo na kuzungumzia masuala ya itikadi, mipango ya kijamii… hakuna hiki kitu Tanzania.”
Badala yake alisema, “Tumeweka siasa kama ni uhasama kati ya chama tawala kilichoshinda kihalali na vyama hivi vingine. Kila siku watu wanatafuta makosa ya wenzao (Serikali) hata kama inafanya vizuri. Hiyo sio siasa.
“Vyama vya upinzani hapa hatuendeshi siasa. Awali, chama chochote kitakachoibuka na siasa inayoeleweka kinaweza kutawala nchi hii kwa miaka 100 ilimradi tu kitoke na siasa inayoeleweka.”
Mghwira alisema, “Vikitokea vyama vitatu vinaendesha siasa inayoeleweka tunakuwa mahali pazuri zaidi. Kwa maana kwamba wale wakiongea jambo lao, hata kama hawatawali, mtawala asikie na kuthamini.
“Sisi hapa Tanzania kuna aina ya siasa za kudidimizana. Kwa sisi wanawake wanaharakati tunaziita PhD (pool her down). Unavutwa tu chini hutakiwi kukua. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.”
Alisisitiza, “Kuna watu wanafikiri kwamba ili kitu kiwe sahihi ni lazima wao wakifanye (upinzani) lakini kikifanywa na watu wengine hakiko sahihi. Hiyo ni kutokuwa mwanasiasa. Kuwa mwanasiasa si kugombana ni kuwa na uwezo wa kujenga hoja, kuitetea na kuisimamia. Mwenzako akija na hoja kubwa zaidi kubali.”