The House of Favourite Newspapers

MGOGORO WA RAMBIRAMBI, MKE ASUSIA 40 YA MAJUTO!

NI tafrani! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mke wa aliyekuwa msanii wa vichekesho nchini, Amri Athuman ‘King Majuto’, Aisha Yusuf kuamua kususia arobaini (40) ya mumewe huyo itakayofanyika Septemba 15, mwaka huu.  

Majuto alifariki dunia Agosti 8, mwaka huu. Aisha alidai kususia arobaini hiyo, kisa kikielezwa kuwa ni mgogoro uliotokana na rambirambi alizokuwa akipewa na watu mbalimbali waliofika kwenye msiba nyumbani kwake, Tanga wakati wa msiba wa nguli huyo wa vichekesho.

Katika mahojiano maalum na Gazeti la Risasi Mchanganyiko, Aisha alieleza kwamba, kuliibuka mambo mengi ikiwemo kukosa huduma muhimu tangu alipofikisha mwili wa mumewe Tanga kutoka Dar kwa ajili ya mazishi na msiba uliokuwa nyumbani kwake.

Alisema aliamua kurejea kwa wazazi wake jijini Dar ambapo atakaa eda hadi atakapoamua kurudi kwake, lakini hatarajii kushiriki dua ya arobaini itakayofanywa na watoto wa mumewe na ndugu zake jijini Tanga.

“Nitafanya arobaini mwenyewe chumbani hapa nyumbani kwa wazazi wangu na watoto wangu. “Nijuavyo mimi dua ya arobaini huwa inapokelewa popote na siyo lazima tukae pamoja. Mtu anaweza kusomewa arobaini (kisomo) hata akiwa nje ya nchi na kisomo kikamfikia.

“Nimerudi kutoka Tanga kuja kukaa eda kwa wazazi wangu kwa sababu walinifanyia mambo ambayo sikuyapenda ikiwa ni pamoja na kuninyima huduma muhimu hasa ya chakula tangu msiba ulipotokea,” alisema mke huyo wa Majuto.

FEDHA ZA JPM

Mke huyo wa Majuto alikwenda mbali zaidi na kufungukia jinsi ambavyo fedha za rambirambi alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ zilivyozua tafrani. Alisema kuwa fedha hizo zilisababisha kadhia kufuatia baadhi ya wanafamilia kumtaka ajihudumie nazo. Alisema anaona yote hayo yalijiri kwa sababu ya fedha hizo alizopewa na mkuu huyo wa nchi ambazo hakuziwasilisha kwenye mfuko wa rambirambi za pamoja.

“Unajua mimi nilipewa fedha na Rais Magufuli. Zile fedha rais alinipa hadharani, sasa tangu nimefika pale msibani (Tanga) walikuwa wakiwapa chakula watu wote, lakini mimi na familia yangu hawakuwa wakitufikia. “Au unakuta tumekaa watu wengi kwenye chumba kimoja, zinaletwa kama sahani mbili za chakula kwa watu wote pamoja na watoto. “Nilikuwa nikiona hivyo naamua kutoa fedha napika na familia yangu.

“Siku moja alikuja wifi yangu kuniuliza ni kwa nini napika mwenyewe, nikamwambia amuite shemeji (kaka wa Majuto) ndiyo nitaeleza ya moyoni. “Nilimweleza shemeji yangu hali halisi, lakini bado waliendelea kunihudumia chakula ndipo mimi nikaendelea kujihudumia kwa kupika na familia yangu kwa kutoa fedha mfukoni mwangu,” alisema Aisha.

WAWEKA KIKAO

Mama huyo aliendelea kudai kuwa, baada ya kuona visa vinaendelea, yeye na familia yake waliamua kuomba kikao ambacho kilihudhuriwa pia na upande wa marehemu mumewe. Alisema katika kikao hicho, ndugu hao wa mumewe waliuliza atakaaje eda na kuomba huduma ya kukaa eda kwa miezi minne atakapokuwa ndani?

“Katika kikao kile mjomba wa marehemu mume wangu, Hamza Kasongo alidai kuwa atawasiliana na kaka yangu kumueleza jinsi gani watanihudumia, lakini cha kushangaza hakuwasiliana naye, aliishia kumtuma mtu na kumwambia kuwa nijihudumie kwa fedha za rambirambi nilizopewa na rais,” alisema Aisha.

GARI LA KUSAFIRIA

Aisha alidai kuwa, mbali na kumwambia ajihudumie kwa fedha za rambirambi, lakini pia alinyimwa gari la kusafiria aina ya Toyota Noah la marehemu Majuto walilokuwa wakilitumia siku zote hivyo alilazimika kusafiri kwa basi yeye na familia yake. “Nilipoomba gari la kunirejesha Dar, nilinyimwa, nikasikia kuwa wanasema nikipewa nitaling’ang’ania halitarudi mikononi mwao,” alimalizia kudai mama huyo.

Baada ya gazeti hili kupata habari hizo liligeukia upande wa pili kwa kaka wa mke wa Majuto, Waziri Mbwana ambaye alikuwa karibu na marehemu Majuto na msibani alikuwepo ambapo alithibitisha maneno aliyoyasema dada yake.

Mbwana alisema kuwa, waliamua kumchukua Aisha kwa ajili ya kumfariji kwani alikuwa kama ametengwa. “Tuliamua kumchukua kwa ajili ya kumfariji, lakini pia anachokisema kuhusiana na kauli ya yeye kutumia rambirambi wahusika walisema kweli kabisa. “Sisi tutamhudumia mpaka atakaposema anarudi kwake kwani hatushindwi,” alisema Mbwana.

MSIKIE MJOMBA

Gazeti hili halikuishia hapo kwani lilimsaka mjomba wa marehemu Majuto, ambapo alisema kuwa, hawezi kuzungumza lolote kuhusiana na mambo ya rambirambi wala mke huyo wa Majuto kunyimwa huduma.

“Sitaki kuongea lolote kuhusiana na mambo ya rambirambi wala huyo mwanamke. Kama mnataka kujua lolote subirini siku ya arobani ya marehemu itakayofanyika Septemba 14 na 15, mwaka huu ndiyo mtajua kila kitu hapa nyumbani kwa marehemu (Tanga) maana familia nzima itakuwepo,” alisema Hamza Kasongo.

TUJIKUMBUSHE

Tangu kifo cha Majuto kumekuwa na maneno mengi hasa juu ya ugawaji wa mali kwani mbali na watoto wanne wa Aisha, wapo wengine ambapo jumla yao ni kumi.

STORI: Waandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.