The House of Favourite Newspapers

Shigongo: Mh! Shikamoo Mdogo Wangu Makonda

Mkurugenzi wa Global Publishers Eric Shigongo

 

Na ERIC SHIGONGO| IJUMAA WIKIENDA| KUMBUKUMBU ZA KWELI ZA MAISHA YANGU- 186

SIPENDI kulala ninapokuwa mgonjwa, huzidiwa zaidi ninapofanya hivyo, hii huwafanya watu wengi kudhani pengine huwa siugui, hata baadhi ya wafanyakazi wenzangu ukiwauliza watasema:

“Nimefanya kazi na Shigongo miaka kumi na tano, sijawahi kusikia ameugua!”

Sio kweli, huwa naugua sana, lakini natembea na vidonge vyangu kwenye gari.

Malaria ya safari hii ilikuwa kumi kwenye damu, hakika ilinitesa,  nilichoma sindano kwa siku tatu nikamaliza kisha kuendelea na vidonge kwa siku nyingine tatu, kidonge kimoja cha Artesunate kila asubuhi na jioni pamoja na dawa za maumivu ambazo ni Panadol, kidogokidogo hali yangu ikaanza kurejea kawaida, nikifanya kazi kila siku.

Siku ya Februari 2, 2017, nikiwa ofisini  kwangu, niliwaona waaandishi na wahariri wamekusanyika mbele ya luninga ambayo iko ofisini, ndani ya ofisi yangu huwa hakuna luninga, naamini uwepo wake unaweza kunipotezea utulivu wa akili ili niweze kufikiria vyema.

Mara nyingi inapotokea waandishi wa wahariri wamekusanyika mbele ya luninga huwa kuna jambo kubwa limetokea, hii hunilazimu nitoke ofisini kwangu kwenda kuungana nao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Kushoto) na khalid Mohammed T.I.D

“Kuna nini tena?”

“Makonda.”

“Anafanya nini?”

“Anatangaza vita dhidi ya dawa za kulevya, hivyo anataja majina ya wasanii wanaotumia dawa ambao anataka waripoti Kituo cha Polisi cha Kati Siku ya Ijumaa kwa mahojiano naye pamoja na Kamanda Sirro!”

“Duh! Aibu, kwa nini hakuwaita kwa njia nyingine badala ya kutumia vyombo vya habari?”

“Hata sijui kwa nini!”

“Sasa kuanzia leo mpaka Ijumaa si watakuwa wameshajipanga?”

“Tusubiri tuone!”

Majina yalianza kutajwa, Wema Sepetu, Petit Man, Babu wa Kitaa, Dairekta Joan, TID, Recho, Mr Blue na Rommy Jones! Ulikuwa ni mshtuko mkubwa mno, hakika ilikuwa ni aibu, baadhi yao tulishasikia habari za kujihusisha kwao na matumizi ya Cocaine, akiwemo Wema, mara kadhaa nilimuuliza lakini alikataa kabisa! Swali moja likanijia kichwani mwangu,

“Sasa kwa nini anakamata wagonjwa? Badala ya waambukizaji wa ugonjwa?”

Hata hivyo, nikasema acha nisubiri hiyo siku ya Ijumaa ili nione kitakachoendelea, maana kwa kweli kutoka ndani ya moyo wangu nazichukia sana dawa za kulevya, zinaharibu maisha ya vijana wetu wengi, watu wachache wenye tamaa ya utajiri wanaharibu vijana wetu ili wajipatie fedha, dhambi kubwa! Bila kujali nilikuwa sijaridhishwa vizuri na utaratibu ambao Mheshimiwa Makonda aliutumia kutangaza majina ya watu hadharani, niliahidi kumuunga mkono katika vita dhidi ya dawa za kulevya! Kama kulikuwa na kosa lolote lingerekebishwa mbele ya safari lakini ujasiri peke yake wa kuingia katika vita hii kubwa na ya hatari iliyowashinda watu wengi, ulitosha kabisa mimi kupuuza makosa yaliyofanyika na kuamua kumuunga mkono mkuu wa mkoa.

Ulikuwa ni mjadala mrefu sana baada ya Mheshimiwa Makonda kumaliza kuongea na waandishi wa habari, ofisi ilikuwa imegawanyika mara mbili, wengi wakiamini hakuwa amefanya jambo sahihi kuwatangaza, ilionekana kama alikuwa anataka kutafuta ‘kiki’ kwenye suala hatari kama dawa za kulevya, kwa hakika wengi walisema kwa mtindo huo alishashindwa vita kabla haijafika mwisho kwa sababu alikuwa ametoa nafasi kwa watuhumiwa kujiandaa.

Wachache waliunga mkono juhudi zilizochukuliwa huku wakikubaliana na mtazamo kuwa kulikuwa na udhaifu katika hatua ambazo Makonda alizichukua kama kweli alikuwa na nia ya kupambana,

“Hakuna ambacho huanza kikiwa kimekamilika, cha muhimu ni kuanza kisha kuendelea kurekebisha kadiri mnavyozidi kusonga mbele, dawa za kulevya ni lazima zipigwe vita kwa nguvu zote!”

Niliwaeleza Mhariri Mtendaji, Saleh Ally, Mhariri Kiongozi, Oscar Ndauka na baadhi ya wahariri na tukakubaliana kuanza matangazo kwenye magazeti kupiga vita dawa za kulevya.

Siku ya Ijumaa ilipowadia mastaa mbalimbali walianza kuwasili Kituo cha Polisi cha Kati mmoja baada ya mwingine, tukio zima lilikuwa likionyeshwa mubashara (live) na kituo kimoja cha televisheni nchini, watu wengi walikuwa wamefurika kuwashuhudia, walitia huruma, hasa kwa sababu kwangu mimi niliwaona hao ni wagonjwa waliohitaji tiba, lakini upande mwingine moyoni mwangu nikajua palikuwa ni mahali pa kuanzia. Nchi ilikuwa imeganyika baada ya tukio hilo, kila mtu alikuwa akisema la kwake, baadhi walimuunga mkono mkuu wa mkoa lakini wengi, kama ilivyo kwetu Watanzania walionekana kuanza kusahau vita, hasa tuliyokuwa nayo, dhidi ya dawa za kulevya na kujikita kwenye suala la kuwakamata wasanii, mioyo ya huruma ya watu wengi iliwafanya waone kama vile walikuwa wakionewa.

“Kwa nini Makonda asiwakamate waagizaji na mapapa? Badala yake anakamata vidagaa? Kama mkuu wa mkoa lazima anawafahamu wauzaji, atashangaa siku moja kukuta ni watu wa karibu yake kabisa ambao wamekuwa wakimsaidia baadhi ya mambo, sijui atawashughulikiaje?” aliniambia mmoja wa watu nilioongea nao.

Maneno ya mtu huyo yalikuwa na maana kubwa sana kwangu, sikutaka kuyapuuza kwani tangu mkuu wa mkoa aingie madarakani pamekuwa na maneno kuwa ana ukaribu na baadhi ya wafanyabiashara pengine bila kufahamu utajiri walionao ambao wanaweza kuwa wanautumia kumsaidia baadhi ya majukumu yake kama mkuu wa mkoa unaweza kuwa unatokana na mambo haramu.

Mtu mmoja aliwahi kusema:

“Wanasiasa hutumia  utajiri wa wafanyabiashara kupata madaraka, kisha wafanyabiashara huwatumia wanasiasa kupata utajiri!” Kwa kauli hii humpasa kila mwanasiasa kuwa makini sana baada ya kupata madaraka kwa msaada wa wafanyabiashara.

Jacob Zuma wa Afrika Kusini ni miongoni mwa wanasiasa walioponzwa na wafanyabiashara. Kitendo cha Mheshimiwa Makonda kuwataja wasanii peke yake na kuacha majina ya vigogo kilizua minong’ono mingi kwamba huenda alikuwa amepata kigugumizi kuwataja vigogo hao kwa sababu ndiyo waliokuwa wakimfadhili katika baadhi ya mambo, wakati minong’ono hiyo ikiendelea, ujumbe ulianza kusambaa mitandaoni  kutoka kwa Makonda akidai awamu ya pili ya vita ilikuwa imekaribia na kwamba sasa angetaja majina mazito.

“Hapo sawa…” nilijisemea moyoni mwangu na kubaki nikiisubiri siku hiyo. Nchi nzima ilikuwa ikimuongelea Mheshimiwa Makonda, Rais akimuapisha Mkuu wa Majeshi mpya, Generali Venance Salvatory Mabeyo alipigilia msumari alipomsifia Mheshimiwa Makonda kwa kazi nzuri tena akisema:

“Hata kama mke wangu Janeth anafanya kazi hiyo akamatwe… ”

kwa mara nyingine tena Makonda alikuwa amefanikiwa kuvikamata vyombo vya habari, jambo ambalo mimi huwa nasema ana utaalam mkubwa sana wa kulifanya.

Nikabaki kimya nikisubiri saa ya kutajwa majina ya vigogo  watuhumiwa wa dawa za kulevya zifike, kichwani mwangu nikifikiria maneno yaliyowahi kuvuma huko nyuma kwamba baadhi ya wafanyabiashara  waliokuwa wakiingiza sukari na saruji kutokea Pakstani ndani yake walibeba dawa za kulevya na kwa ushawishi mkubwa waliokuwa nao, hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaambia lolote.

Kwa madai hayo, dawa hizo nyingi zilizokuwa zikiingizwa hapa nchini kwa mtindo huo ziliigeuza nchi yetu kuwa njia kuu au soko kuu la dawa za kulevya katika Afrika, Watanzania wengi walikamatwa katika nchi mbalimbali wakisafirisha dawa za kulevya kutokea hapa kwetu, jina la Tanzania likachafuka, hati ya kusafiria ya kijani yenye jina Tanzania ambayo huko nyuma iliheshimika ikaanza kutiliwa shaka, upekuzi kwa Watanzania katika viwanja vya ndege ukawa mkubwa.

Miaka michache iliyopita nikiingia kwa ndege Los Angeles, kwenye Uwanja wa LAX, nilichukuliwa kutoka kwenye mstari na kwenda kuwekwa kwenye chumba maalum kwa saa mbili nikiulizwa maswali mengi kwa sababu tu nilikuwa na hati ya kusafiria ya Tanzania, siku hiyo ni miongoni mwa siku ambazo nimewahi kuchukia kupindukia.

Jina la nchi yetu limechafuliwa mno, afya za vijana wetu zimeharibiwa sana, ukienda Mbagala, Temeke, Mwananyamala na Kinon

doni ndiyo utaelewa ninachokizungumza! Nguvu ya taifa inateketea kwa sababu ya watu wachache wasiojali ilimradi wao wanatajirika, hapana! Lazima Makonda aungwe mkono hata kama kuna makosa machache katika operesheni hii yatarekebishwa lakini mapambano lazima yaendelee.

Hatimaye muda ukafika, majina yakatajwa! Dunia ikatikisika jina la Yusuf Manji lilipotajwa, kila mtu ofisini kwetu akasema “Mungu wangu!” maana siku zote bilionea huyu alionekana mtu asiyeguswa, alishapambana vita na wanasiasa pamoja na matajiri wenzake wengi na kushinda, kifupi alikuwa ni mtu

“Mpenda kutetea haki yake mahakamani.”

Kitendo cha Mheshimiwa Makonda kumtaja tu kama asingekuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani lazima ingesababisha mlolongo wa kesi

“Kama amemtaja lazima atakuwa na ushahidi”

baadhi ya watu walisikika wakisema hivyo. Majina mengine yaliyoshtua watu ni ya Askofu Gwajima, Idd Azzan na Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema.

“Mbowe?”

Nilijiuliza bila kupata majibu, sikuwa na haki ya kusema chochote kwa sababu nilikuwa sijafanya utafiti, nikachagua kukaa kimya. Jambo jingine lililokuwa limenishangaza kabisa  na kunisikitisha ni kukamatwa kwa  Majay, Mkurugenzi wa Radio E-FM, inayotamba sana hivi sasa jijini Dar es Salaam!

Huyu ni miongoni mwa vijana ambao navutiwa sana na mafanikio yao, mchapakazi, ameanzia kwenye dhiki nyingi kama mimi, sitaki kusema chochote, nawaacha wataalam wa kuchunguza wamchunguze na kujiridhisha. Katika maisha haya ya biashara kila mtu ana siri zake, lakini ungeniuliza mimi kuhusu Majay kabla ya kukamatwa, ningekueleza wazi kwamba

“Majay? Unga? No!”

Na pengine nitaendelea kusema hivyo mpaka itakapothibitika, nadhani sitamwamini mtu tena baada ya hapo. Kama alivyosema Makonda mwenyewe,  kutajwa kwa majina ya awamu ya pili kulisababisha mtikisiko mkubwa zaidi, mpaka bungeni, wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa

likuja juu mno kwa kauli aliyoitoa kwamba:

“Huwa wanakwenda bungeni kusinzia.”

Kauli hii ilikuja baada ya Mbunge wa Geita, Mheshimiwa Msukuma kumjia juu Makonda akidai ilikuwa ni lazima na yeye aelezee utajiri wake mkubwa aliokuwa nao aliupataje ndani ya muda wa mwaka mmoja.

Vyombo vya habari vikaanza kusahau vita dhidi ya dawa za kulevya na kuelekeza nguvu zake kwenye suala la Makonda, Msukuma, Mbowe, Bunge, Wema! Huko ndiko mijadala ikahamia, tukiwa tumesahau kabisa kwamba pengine katika muda ambao tuliendelea kulumbana juu ya watu niliowataja hapo juu, tani nyingi za dawa za kulevya zilikuwa zikiingia nchini! Rais John Pombe Magufuli akawa kama ameyasoma mawazo ya Watanzania walio wengi, mara moja akamteua Rogers William Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa  Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, hii ikathibitisha kabisa kwamba, rais alikuwa amedhamiria kukomesha biashara hii iliyoharibu maisha ya watu wake.

Hofu ilikuwa imetanda mioyoni mwa watu wengi, hasa wafanyabiashara, lolote lingeweza kutokea, miongoni mwa watu waliokuwa na hofu sana ni mimi! Maana kwa chuki tu sababu pengine mtu amewahi kuandikwa gazetini na kuwa na chuki na mimi angeweza kusema:

“Huwa nauziwa na Shigongo,”

Ambacho kingefuata baada ya hapo ingekuwa ni mimi kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kati kwa mahojiano huku nikipigwa picha na kutangazwa kila mahali.

Jambo hili ndilo ambalo lilikuwa likiwasikitisha watu wengi na kupingwa na watu wengi nikiwemo mimi, watu wengi wanaunga mkono juhudi za Mkuu wa Mkoa lakini wanapinga kabisa utajaji hadharani wa majina ya watu sababu tu wametuhumiwa, inaumiza sana heshima na utu wa watu wengi.

Hili ndilo jambo ambalo Mkuu wa Mkoa anatakiwa kulibadilisha katika vita hii, mimi ninafanya kazi kwenye chombo cha habari, zilishakuja tuhuma nyingi sana dhidi ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa lakini huwa hazichapishwi gazetini kwa sababu tu katuhumiwa, kimyakimya uchunguzi huwa unafanyika na ikibainika ni majungu huwa habari hizo zinatupwa kabla ya kuchapishwa.

Hivi tungezichapisha na baadaye ikaonekana alisingiziwa, heshima  yake katika jamii ingebaki palepale? la hasha ingeporomoka mno.

Kama hivyo ndivyo ni kwa nini sasa yeye anaporomosha heshima za watu wengine kwa tuhuma tu? Je, hapakuwa na njia nyingine ambayo ingetumika kufikia lengo lilelile bila kubomoa majina ya watu waliyoyajenga muda mrefu?

Lazima tuzungumze wazi kuwa hii inawaumiza watu. Ni vyema tukapigana vita dhidi ya adui mkubwa dawa za kulevya bila kuwaumiza watu wengine, jambo hili ndilo mkuu wangu wa mkoa anatakiwa kulifanya.

Baada ya vigogo kutajwa siku iliyofuata, Yusuf Manji alifika Kituo Kikuu cha Polisi ikiwa ni siku moja kabla ya ile iliyokuwa imepangwa, vivyo hivyo Askofu Gwajima, kichwani mwangu nilijua wanakwenda kuhojiwa halafu watatoka! Cha kushangaza mpaka leo ninapoandika kumbukumbu hii, Februari 11,2017, siku ya Jumamosi, bado Yusuf Manji na ubilionea wake yuko mahabusu, Gwajima peke yake ndiyo ameachiwa muda mfupi uliopita! Shikamoo mdogo wangu, Makonda…

Comments are closed.