The House of Favourite Newspapers

Mhandisi Mshauri Wa Umeme Aishauri Jambo Zito Tanesco Kuhusu Changamoto Ya Uhaba Wa Umeme Na Majanga Ya Moto

0
Mhandisi Ester William alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari leo.

Dar es Salaam, 7 Oktoba 2023: Mhandisi Mshauri wa masuala ya umeme, Mhandisi Ester William leo amelishauri jambo shirika la kusambaza umeme la taifa nchini (Tanesco) kuwashirikisha wataalamu mbalimbali katika kukabiliana na kupatikana kwa umeme wa uhakika na majanga ya moto.

Mhandisi Ester amesema Tanesco licha ya kupambana wenyewe kutatua shida ya kupatikana kwa umeme wa uhakika na majanga ya moto yanayotokea mara kwa mara wangewashirikisha wataalamu ili wajadiliane kwa pamoja namna bora ya kumaliza  changamoto hizo.

Akizungumza na wanahabari jijini leo Mhandisi huyo alisema;

“Ndugu waandishi wa habari, kwa majina naitwa Injinia Ester William, ni mhandisi mshauri kwenye tasnia ya umeme kwa takribani miaka 20.

Ndugu waandishi wa Habari, kutokana na barua ya TANESCO, ya Jumatano Tarehe 27, Septemba 2023 imeutarifu umma rasmi kwamba kuna changamoto ya upungufu wa umeme.

Sababu zinazopelekea upungufu huo zimetajwa nyingi, lakini leo mimi nitaongelea sababu ya kwanza kabisa iliyotajwa “ONGEZEKO LA MAHITAJI YA UMEME KUTOKANA NA KUKUA KWA SHUGHULI ZA KIUCHUMI”

Nchi yetu inakua na shuguli za kiuchumi zinakua, shughuli nyingi za kiuchumi zinafanyika kwenye majengo ambapo tunahitaji umeme wa uhakika.

Majengo yanajengwa kwa utaratibu kulingana na matumizi yake, kuna viwanda, hospitali, ofisi, nyumba za kuishi n.k. Ili jengo likamilike linahitaji miundombinu tofauti tofauti ukiwemo umeme wa uhakika. Majengo mengi hasa makubwa kawaida yanafanyiwa miundombinu ya umeme ili kujua kiasi cha umeme kitakachohitajika (Power Demand Projection).

Kwa uzoefu wangu, kawaida tukimaliza usanifu(design), baada ya kupatikana kwa Mkandarasi, ujenzi unaendelea. Mwisho wa mradi, kwa kupitia Mkandarasi, TANESCO wanafunga umeme kwenye mradi, na jengo linatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Ukiungalia mtiririko huo, TANESCO amepewa taarifa baada ya kila kitu kufanyika, kwa maana nyingine miradi mingi kama siyo yote inakuwa kama Surprise kwa TANESCO.

Hiyo ikiwa inamaanisha kwamba design au maamuzi ya kujenga mradi maeneo tofauti yanafanywa kama vile kuna “Infinity Sources of Power” yaani umeme mwingi bila kikomo.

Nafikiri utaratibu huu ndo umefanya ukuaji wa uchumi uwe changamoto kwa upande wa umeme, kwani ni kama mpishi alikuwa na chakula bila kuwa na idadi kamili ya wageni.

Ukuaji wa uchumi upo na kwa kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinazokua na tunaona jinsi serikali yetu tukufu ya Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassani, inavyowekeza kwenye miradi mbalimbali na pia inakaribisha wawekezaji. Kwa mtazamo huo, ukuaji huo unatakiwa kuwa fursa kwa TANESCO kuuza umeme wa kutosha na siyo kusababisha upungufu wa umeme ambao unaathiri umma na pia wao wanaathirika na kupelekea athari kwa uchumi wa nchi.

Kwa maana hiyo basi naomba wataalamu tushirikishwe vizuri, ili ukuaji wa uchumi isiwe changamoto, kwani uchumi haukui kwa siku moja, mara nyingi miradi inaweza kuisha baada ya mwaka au zaidi, ushirikiano huo utawezesha shirika letu la umeme kujipanga na kufurahia ongezeko la wateja.

MATUMIZI NA TABIA UMEME

Baada ya kumfungia umeme mtumiaji hasa watumiaji wakubwa, nikimaanisha wateja wa T2 na T3, tabia za umeme zinabadirika kutokana na vifaa vilivyofungwa, mfano viwanda, vyanzo vya maji na vifaa vingi hasa vyenye mota.

Tabia za umeme zina vitu vingi sana ambavyo havionekani kwa macho, ikiwemo kitu kinaitwa Power Factor, hiki kitu kinaathiri sana mifumo ya umeme. Waathirika wakubwa ni wateja wakubwa, Power Factor ina viwango vyake, ikiwa chini ya kiwango, jengo husika litatumia umeme mkubwa na kusababisha upotevu wa umeme.

Kwa tafiti nilizofanya kwa takribani miaka kumi, wateja wengi wako chini ya kiwango, kwa maana nyingine kuna umeme mwingi unapotea kutokana na hiyo Power Factor.

Ombi langu kwa Serikali, Wataalamu tupo, tutumike kufanya research, tutoe maoni yetu, naamini yakifanyiwa kazi ipasavyo tutaokoa kiasi kikubwa cha umeme ambacho kitatumika wakati TANESCO ikiwekeza ili kupata ufumbuzi wa kudumu,kuhusu upungufu wa Umeme”. Alimaliza kusema Mhandisi huyo.

Imetolewa na Eng. Ester William

MD – GEARED CONSULTING ENGINEERS LTD

INSTAGRAM ACCOUNT @wardaester

Leave A Reply