The House of Favourite Newspapers

Miaka 43 imepita tangu uamuzi wa kuhamia Dodoma!

0

dodomaKWA anayesoma safu hii akiwa na umri ulio chini ya miaka 43 ajue kwamba alizaliwa baada ya uamuzi wa serikali ya Julius Nyerere kuamua kuhamisha makao makuu ya serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma!

Uamuzi huo aliutangaza Nyerere mwenyewe mwaka 1973 akisema mji huo ulifaa kuwa makao makuu ya nchi hii kwa vile ulikuwa karibu, katikati ya nchi, hivyo ungeweza kuhudumia kirahisi kwa kila ‘kona’ ya nchi hii kubwa ambayo ni mara tatu kwa ukubwa kuliko Uingereza.

Ilipita miaka 12 tangu uamuzi huo hadi Nyerere anaondoka madarakani mwaka 1985 uamuzi wa kuhamia Dodoma ukiwa bado kitendawili, kwani hata ofisi yake yeye mwenyewe – ikulu – haikuweza kuhamia katika mji huo ulioko eneo la watu wa Kabila la Wagogo.

Kitu pekee kilichoonesha juhudi za kutimiza uamuzi huo ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yaani Capital Development Authority (CDA) chombo ambacho kwa ‘mamiaka’ kibao hakisikiki tena na wachache wanakifahamu!  Kiuhalisia, hakuna watendaji wa ngazi za juu serikalini waliohamia Dodoma au waliokuwa na hamu ya kuhamia Dodoma, maamuzi yote yameendelea kutolewa kutoka Dar es Salaam.

Baada ya Nyerere ulikuja utawala wa Ali Hassan Mwinyi hadi ukaondoka madarakani, hakuna kilichofanyika kuonesha dhamira ya kuhamia Dodoma.  Akafuata Benjamin Mkapa, mambo yakawa yaleyale, huku hata kauli za kuhamia Dodoma zikizidi kufifia.

Wahusika wakawa wanakwenda Dodoma bungeni na kwa shughuli za Chama Cha Mapinduzi (CCM) tu, zikimalizika ‘wanapotelea’ Dar es Salaam.  Hakuna aliyetaka kubakia Dodoma.  Wamefanya hivyo hadi Julai mwaka huu — 2016

Ukafuata utawala wa Jakaya Kikwete, suala la kuhamia Dodoma likabaki ‘kimya’, likiwa  jinamizi lililoanzishwa na kuachwa na Nyerere.

Ni majuzi tu Rais John Magufuli ‘alipolizindua’ jinamizi hilo–baada ya miaka 43 kupita–na kuamua kulipatia sura ya kueleweka, tofauti na watangulizi wake walioliweka kando suala hilo.

Kwa vile Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameamua kuhamia huko mwaka huu, huenda ‘ndoto’ za Rais Magufuli zikatimia na kuwalazimu waliokuwa wanapenda ‘nyama-choma’ za mji huo lakini hawataki kuishi huko, wakasalimu amri na kuamua kuishi huko moja kwa moja.

Leave A Reply