The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 39

0

“Hatuwezi kupumzika kidogo,” Faiza akauliza alipoona nilivyokuwa nikitweta.
“Hapapumzikiki dada’ngu. Bora tujitahidi hivyo hivyo,” mtu
mmoja akamwambia Faiza.

SASA ENDELEA…
Lakini hapo hapo tukaona mwanga ukimweka kama umeme. Ulimweka mara moja tu kisha tukamuona Kaikush amesimama mbele yetu.
“Hamtaweza kutoroka na mke wangu,” alituambia kwa hasira kisha akaongeza.
“Nitawaua nyote!”

Askari mmoja wa kikosi cha zimamoto na uokoaji ambaye tulikuwanaye na ambaye alikuwa karibu na Kaikush alidakwa ghafla.

Uzoefu ulishatuonesha kuwa risasi zilikuwa hazimuingii jini huyo. Bunduki aliyokuwa nayo yule polisi ilikuwa kama upuuzi mtupu. Nilimuona akiitupa na yeye mwenyewe akaanza kukimbia.

Mimi nilikuwa nimemshika mkono Faiza nikamuachia na kutimua mbio. Faiza akalishika shati langu mgongoni, nikawa namkokota kwa nyuma.

Wenzetu wengine nao wakaanza kukimbia. Sasa ilikuwa ni mbio kwa mbio kwani yule jini alikuwa akizuka tu mbele yetu na kutusababishia tafrani.

Tulikuwa tumechoka lakini tulikuwa tunajikokota tu ili tusiuawe. Nilihisi kwamba wakati wowote ningeweza kuanguka na kuzirai au kufa kutokana na kuishiwa nguvu kabisa.

Jinsi tulivyokuwa tunakimbia katika njia ile nyembamba tulikuwa tunayumba na kugongana kama walevi kutokana na kuchoka.

Kulikuwa na wakati nilikwaa jiwe nikaanguka chini. Wenzangu waliokuwa nyuma walinipita na kunikanyaga kwa bahati mbaya wakaendelea kukimbia. Faiza akasimama na kunishika mkono kuniinua.
“Inuka,” aliniambia.

Nikajitahidi kuinuka. Tulikuwa tumeshapitwa na wenzetu wote.
Goti langu la mguu wa kulia ambalo lilipiga chini lilikuwa likiuma sana. Nikasega suruali yangu na kulitazama. Lilikuwa limechanika na lilitiririsha damu kwa wingi.
“Oh pole sana,” Faiza akaniambia alipoona ile damu.

Nilijaribu kutembea. Sikuweza kabisa. Goti lilikuwa limekaza na mguu haukuweza kukunja.“Huwezi kutembea?” Faiza aliniuliza kwa fadhaa.
“Siwezi, goti halitaki kukunja kabisa.”

Faiza alichutama akaifuta ile damu iliyokuwa ikitoka kwenye goti langu kwa mkono wake.“Mbona unajipakaza damu mkononi?” nikamuuliza.
Nilipomwambia hivyo Faiza alijifuta kwenye gauni lake.
“Hebu kaa chini,” akaniambia.

Nikakaa. Kukaa kwenyewe pia kulikuwa ni kwa tabu.
Faiza akaushika mguu wangu na kuanza kuupindisha kwenye goti kama aliyekuwa akiufanyisha mazoezi. Alipofanya hivyo alikuwa akinisababishia maumivu makali.
Nilikuwa nimekunja uso wangu. Nikamwambia.
“Faiza unaniumiza!”

“Vumilia. Bila kukunyoosha hili goti, tutakwama hapa hapa.”
“Faiza unajitahidi lakini haitasaidia, kwani wewe si unaweza kukimbia?”
“Una maana gani?” Faiza akaniuliza.
“Kimbia uwafuate wenzetu.”

“Halafu wewe?”
“Mimi naona safari yangu itaishia hapa hapa.”
“Yaani nikuache hapa?”
“Ndiyo niache, wewe kimbia uende zako.”
“Kaikush si atakuja kukuua hapa hapa!”
“Sasa nitafanyaje?”

“Bora tufe sote, mimi sitaondoka hapa!”
Wakati Faiza akilikunja goti langu na kulikunjua damu ilikuwa ikizidi kunitoka. Ilikuwa ikimuingia mikononi mwake.

Baada ya kuunyoosha mguu wangu kwa sekunde kadhaa aliniambia.
“Hebu jaribu kuinuka.”
Nikajifanya nainuka haraka haraka ili kumpa moyo.

“Utaweza kutembea?” akaniuliza huku akinitazama kwenye macho yangu.
Ili kumridhisha yeye nikamwambia.
“Nitajaribu.”

Ukweli ni kuwa maumivu ya goti sasa yalikuwa yamezidi ingawa goti lilikubali kukunja.
Nikajaribu kutembea kwa kuchechemea nikiwa nimeuweka mkono wangu kwenye bega lake.

“Dakika chache zilizopita ulinibeba lakini mimi siwezi kukubeba.”
Sikumjibu kitu. Niliendelea kuchechemea.
Mara kwa mara nilikuwa natazama nyuma.

“Unatazama nini?” Faiza akaniuliza.
Badala ya kumjibu nilimwambia.
“Hivi sasa wenzetu wamefika mbali.”
“Wameshindwa hata kutusubiri lakini kutangulia siyo kufika, sisi twende hivi hivi polepole.”

“Unajua Faiza, mimi sijapenda ubaki nyuma pamoja na mimi. Mimi ndiyo mwenye matatizo ungeniacha tu wewe uwafuate wenzetu. Unaweza kusalimisha maisha yako.”
Faiza akatikisa kichwa.

Siwezi kukuacha peke yako. Kama Kaikush atakuja basi atuue sote.”
Nikatazama nyuma tena. Kwa upande wangu nilikuwa nimeshajitolea kuuawa lakini sikupenda yule msichana naye auawe ila alikuwa mbishi.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Leave A Reply